Sheikh Farid Katikati ya Askari Magereza.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hellen Liwa amejitoa
kusikiliza kesi ya ugaidi inayowakabili viongozi 23 wa Jumuiya ya Uamsho
na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI).
Hakimu huyo amefikia uwamuzi huo baada ya wakili wa washtakiwa hao wa ugaidi, Abubakar Salim kumtaka ajitoe
kuisikiliza kesi hiyo ili iweze kupangiwa hakimu mwingine ambaye atatoa
uamuzi juu ya hoja zao walizozitoa mahakamani hapo Septemba 19,2014.
Salim
aliiambia mahakama kuwa baada ya kushauriana na wateja wao na uamuzi
uliotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu, Dk Fauzi Twaib wakaona kuwa ni
ukweli kuwa Hakimu Liwa alikwisha toa uamuzi wake juu ya hoja zao Oktoba
Mosi, 2014 kuwa mahakama hiyo ya kisutu haina mamlaka ya kusikiliza hoja hizo.
Alidai
Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Twaib umeelekeza kuwa
Mahakama ya Kisutu inayo mamlaka ya kuzisikiliza hoja za washtakiwa hao
wa ugaidi na hata kuzitolea uamuzi.
"Mahakama
Kuu imeelekeza mawakili wa upande wa utetezi kama tutakuwa na hoja mpya
ama zile za awali tuzitoe kwenye mahakama hii ya Kisutu ili ziweze
kutolewa maamuzi hivyo naona ni bora ujitoe tupate neno kutoka kwa
hakimu mwingine."Alisisitiza kusema wakili huyo mahakamani hapo.
Wakili wa
Serikali Mkuu, Benard Kongola alimuomba Hakimu Liwa asijitoe katika
kuisikiliza kesi kwa madai sababu zilizotolewa na upande wa utetezi za
kumtaka ajitoe hazina msingi.
Kongola
alieleza kuwa uamuzi uliotolewa na Jaji Twaib aliamuru utekelezaji wa
hoja za upande wa utetezi katika kesi hii ya ugaidi zisikilizwe na
kutolewa uamuzi katika Mahakama ya Kisutu.
"Tukiendekeza
hii tabia tutamaliza mahakimu wote wa mahakama hii tunasisitiza upande
wa utetezi utoe sababu za msingi za wewe kujitoa."Alisema Kongola.
Akijibu
hoja hizo, Wakili Salim alieleza kuwa ili haki ionekane inatendeka wewe
Hakimu Liwa ujitoe ili hakimu mwingine atoe maamuzi wa hoja zetu.
Hakimu
Liwa alisema ni kweli nilikwisha toa uamuzi wangu juu ya maombi ya
washtakiwa lakini Mahakama Kuu imeona kivingine kuwa sijatumia mamlaka
yangu vizuri nakubaliana na uamuzi huo.
Lakini
uamuzi huo wa Jaji Twaib haukufafanua nini kifanyike, umetuacha hoi, ila
alitoa angalizo kuwa ushahidi wa kesi hauwezi kutoka hewani na kwamba
maelezo yaliyomo katika hati ya mashtaka ya kesi hiyo yapo sahihi.
"Kitu
ambacho hata mimi nilikuwa nakishangaa ni hii hati ya mashtaka kuletwa
Tanzania Bara badala ya Visiwani, lakini nilipoisoma sheria ya ugaidi
nikabaini mtu anaweza kushtakiwa mahali popote." Alisema Hakimu
Liwa.Alisisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria Mahakama Kuu ndiyo yenye
uwezo wa kuisikiliza kesi hii na siyo mahakama ya Kisutu hivyo yeye
hawezi kusema kitu labda kesi ingekuwa imefikia kwenye mwenendo wa
uhamishaji shauri (Committal Preceding).
Hatua
hiyo inafikiwa baada ya upelelezi wa kesi kukamilika inahamishwa kutoka
mahakama ya Kisutu kwenda Mahakama Kuu ambayo inamlaka ya kusikiliza
kesi hizo.
"Mimi
nimejifunza kitu hapa, kuwa mimi najua nini na wenzangu wanajua nini
hivyo siwezi kuendelea na kesii haitakuwa haki najitoa."Aliongeza kusema
Hakimu Liwa na akajitoa na kuiahirisha hadi Januari 13,2015 ili ipangwe
kwa hakimu mwingine.