Nairobi.
Mahakama ya Juu (Supreme Court) ya nchini Kenya imeagiza kuchunguzwa
kwa fomu 34 za matokeo ya uchaguzi wa rais kutoka katika vituo vyote
34,400, vilivyotumika kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo
uliofanyika Machi 4, mwaka huu.
Kadhalika
mahakama hiyo jana iliagiza kuhesabiwa upya kwa kura za urais katika
vituo vya kupigia kura 22 kati ya elfu 33 vilivyolalamikiwa na aliyekuwa
mgombea urais wa Muungano wa Cord, Raila Odinga.
Katika
malalamiko yake yaliyowasilishwa katika mahakama hiyo kupinga Uhuru
Kenyatta kutangazwa mshindi wa urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika
Machi 4, Odinga alidai kuwa vituo hivyo 22 kura zilizopigwa zinazidi
idadi ya wapigakura walioandikishwa.
Akisoma
uamuzi huo kwa niaba ya majaji wenzake watano, Jaji Smokin Wanjala
alisema kwamba uhesabuji kura wa vituo hivyo utafanyika leo kuanzia saa
2.00 asubuhi kwa lengo la kubaini ukweli kuhusu madai hayo.
“Matokeo
ya kura zitakazohesabiwa katika vituo hivyo 22 yawasilishwe katika
mahakama hii Jumatano, saa 10.00 jioni,” alisema Jaji Wanjala.
Kikao hicho, ambacho Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Othman Chande amealikwa kama mwangalizi, ni cha awali kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa rasmi keshokutwa (Alhamisi) na kuendelea kwa mfululizo hadi kufikia uamuzi ikiwa madhumuni yake.
Lengo ni kupitia madai yaliyowasilishwa mahakamani hapo na pande zote zinazohusika na kuamua mwenendo wa kesi utakavyofanyika.
Ukiachilia
mbali kesi iliyofunguliwa na Odinga kupinga Kenyatta kutangazwa mshindi
wa uchaguzi huo wa tano tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa
Kenya, kuna kesi nyingine ambayo imefunguliwa na muungano wa mashirika
yasio ya kiserikali, `The African Centre for Open Governance’ (Africog).
Katika
kesi hiyo inayorushwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni
nchini Kenya, Africog inahoji uhalali wa uchaguzi huo.
“Kesi yetu haihusiani na nani ameshinda au kushindwa bali jinsi umma ulivyoshindwa, tumepoteza ahadi ya uchaguzi uliowazi,” alisema Gladwell Otieno, Mkurugenzi Mtendaji wa Africog.
Kesi
ya tatu ambayo imefunguliwa na wajumbe wa timu ya kampeni ya Kenyatta,
mwanaharakati katika mitandao ya kijamii Dennis Itumbi na Moses Kuria
wanaopinga uamuzi wa Tume Huru ya uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya
kujumuisha kura zilizoharibika wakati wa kujumlisha kura za wagombea
urais.
Katika
uamuzi wake, mahakama iliamua kwamba kesi zote tatu zitaunganishwa kuwa
moja, huku ile iliyowasilishwa na Odinga ikiwa ndiyo kinara wa kesi
zote.
Pia
mahakama iliamuru Muungano wa Vyama vya Siasa wa Cord na Jubilee kuteua
mawakala 10 kila mmoja ambao watakula kiapo mahakamani hapo kabla ya
kuanza kuhesabu upya kura hizo.
Katika
uamuzi wake jana jioni, mahakama hiyo ilikubali ombi la Mwanasheria
Mkuu wa Kenya, kushiriki katika kesi hiyo kama rafiki wa mahakama na
siyo mdaiwa kama ilivyokuwa awali. Wakili wa Cord, George Oraro
alikubali uamuzi huo licha ya kuupinga awali.