Afisa Habari wa TFF Baraka Kizuguto
Kamati ya
Uendeshaji na Usimamizi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)
imethibitisha ushindi wa pointi 3 na mabao matatu kwa timu za Majimaji na
Toto Africans baada ya mechi zao za Ligi Daraja la Kwanza (FDL)
kuvurugika kutokana na sababu mbalimbali.
Toto
Africans imepewa ushindi huo kwa mujibu wa Kanuni ya 41(3) ya FDL baada
ya vurugu za washabiki wa Geita Gold kusababisha mechi hiyo iliyochezwa
Februari 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita kuvunjika
dakika ya 12.
Pia
Kamati hiyo iliyokutana Dar es Salaam jana (Februari 12 mwaka huu)
imezuia mechi za FDL kuchezwa kwenye uwanja huo ambao hauna uzio wa
kutenganisha wachezaji na washabiki kwa sababu za kiusalama.
Naye
mchezaji Venance Joseph wa Geita Gold ambaye alimpiga kichwa refa
akipinga adhabu ya penati iliyotolewa dhidi ya timu yake kwenye mechi
hiyo amesimamishwa wakati akisubiri kosa lake kusikilizwa na Kamati ya
Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Malalamiko
ya Friends Rangers kwenye mechi dhidi ya Majimaji yametupwa na kupigwa
faini ya sh. 500,000 kwa kusababisha mchezo huo uliochezwa Januari 29
mwaka huu Uwanja wa Majimaji mjini Songea kuvunjika dakika ya 39. Adhabu
hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 28(4) ya FDL.
Friends
Rangers imepoteza mechi hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 28(1) ya FDL,
Majimaji kama ilivyo Toto Africans imepewa ushindi wa pointi tatu na
mabao matatu.
Naye
Kocha wa Friends Rangers, Herry Chibakasa (Mzozo) suala lake limepelekwa
kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF ili aweze kuchukuliwa hatua za
kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni ya 39(8) ya FDL kwa kuhamamisha vurugu
kwenye mechi dhidi ya Majimaji.
Mwamuzi
John Mafuru wa Mbeya aliyechezesha mechi ya Majimaji na Friends Rangers
amefungiwa miezi 12 (kumi na mbili) kwa kutozingatia sheria kiasi cha
kuvuruga mchezo. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 37(1) ya FDL.
Pia
Kamishna wa mechi hiyo Kim Rajab wa Dodoma amefungiwa miezi 12 (kumi na
mbili) kwa mujibu wa Kanuni ya 38(1) ya FDL kwa kutoa taarifa zisizo
sahihi.
Lipuli ya
Iringa imepewa ushindi wa mabao matatu na pointi tatu baada ya timu ya
KMC (Tessema) kumchezesha mchezaji Morris Paulo Katumbo aliyekuwa na
kadi tatu za njano kinyume na Kanuni ya 41(12) ya FDL. Katumbo ambaye
alipata kadi hizo kwenye mechi namba 85, 100 na 112 alicheza mchezo huo
uliomalizika kwa timu ya KMC kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)