NDEGE kubwa za abiria za kimataifa zinatarajiwa kuanza kutua
Uwanja wa Ndege wa Kigoma kuanzia Desemba 15 mwaka huu baada ya uboreshaji wake
kufikia hatua nzuri.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na blog hii mjini
Kigoma, Meneja wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama wa Anga (TCAA), Godlove Hongore
amesema hadi kufikia katikati ya mwezi ujao meta 1,450 za kuruka na kutua ndege
zitakuwa zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami kati ya meta 1,800
zinazotarajia kujengwa.
Alisema mkataba wa ujenzi wa mkandarasi wa uwanja huo
unaisha Juni mwakani lakini ujenzi umeelezwa na msimamizi wa Kampuni ya
Synohydro ya China
kwamba unaweza kukamilika mapema zaidi ya muda uliopangwa.
Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mkoani Kigoma, Elipid
Tesha alisema mazungumzo yanaendelea vizuri ili kampuni hiyo ya Synohydro ya China
iendelee na sehemu ya pili ya mradi huo katika mwaka ujao wa fedha
utakaohusisha ujenzi wa njia ya kurukia ndege kufikia meta 3,000 na jengo la utawala
na abiria uwanjani hapo.
Alisema tayari fedha za fidia kwa ajili ya eneo la makaburi
ambalo litatumika kwa upanuzi huo, ipo na mazungumzo yanaendelea ni kuwezesha
mkandarasi huyo kuendelea na sehemu hiyo ya pili ya mradi huo.
Meneja huyo wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Mkoa, alisema
kukamilika kwa Awamu ya Pili ya ujenzi wa awanja huo kutaufanya Uwanja wa Ndege
wa Kigoma kuwa na hadhi ya kimataifa na kuruhusu ndege kubwa zaidi ya tani 70
kutua.
Alibainisha kuwa uwanja huo ukikamilika, utakuwa kitovu cha
ndege nyingi kutoka nchi za ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika ya Kati kwenda
Kusini na Kaskazini mwa Bara la Afrika na nje ya bara hilo.