Facebook Comments Box

Tuesday, December 17, 2013

MWENYEKITI WA CCM MKOA WA MWANZA AUAWA KWA KIPIGO TOKA KWA WANANCHI

 


ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Chama Mapinduzi (CCM) mkoani hapa na Diwani wa kata ya Kisesa wilayani Magu kwa sasa, Clement Mabina (pichani), ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kipigo, kufuatia ugomvi wa shamba.

Kwa mujibu wa habari hizo, Mabina ambaye alikuwa Diwani wa Kata ya Kisesa (CCM) aliuawa kwa kushambuliwa kwa mawe na mapang, baada ya kutokea kutoelewana na wananchi wa eneo hilo la mlima ambapo alikwenda kupanda miti kwa madai kuwa lilikuwa shamba lake.

Mkuu wa polisi wa wilaya ya Magu (OCD) aliyejitambulisha kwa jina moja la Mkapa, alikiri kutokea kwa mauaji hayo na kudai kwamba awali ilisikika milio ya bunduki kwenye eneo la Kanyama kabla ya kumtuma Mkuu wa Upelelezi wa wilaya hiyo (OC CID) kwenda katika eneo la tukio, hivyo taarifa kamili itatolewa na polisi mkoani Mwanza.


Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Desdery Kiswaga wakati akielekea kwenye eneo la tukio hilo leo mchana(Jumapili), aliliambia Uhuru kuwa alipokea taarifa za kifo cha Mabina kwa masikitiko makubwa baada ya kusikia kauawa na wananchi wenye hasira kali wakati wakigombea shamba la mlima huo.

Taarifa zaidi kutoka katika eneo la Kanyama zimedai kuwa Mwenyekiti huyo wa CCM awamu iliyopita,leo(Jumapili) asubuhi alipofika kwenye eneo la mlima huo analolimiliki ambalo linadaiwa kuwa na mgogoro baina yake na baadhi ya wananchi wa Kanyama, wananchi walifika na kumhoji kwa nini anapanda miti.

Hali hiyo ilizua mabishano makali na kutoelewana na wananchi hao ambao baadhi walikuwa na mapanga na kuzidi kuongezeka huku wakimzingira.

Kutokana na hali hiyo, Mabina alifyatua risasi hewani kuwatawanya lakini wananchi hao walianza kumshambulia kwa mawe na ndipo alipojihami kwa kufyatua risasi nyingine ambazo kwa bahati mbaya, moja wapo ya risasi ilimpiga mtoto mmoja aliyekuwa kwenye tukio hilo na kusabaisha kifo chake.

Wananchi hao walizidi kumshambulia kwa mawe na kumjeruhi kichwani kabla ya kumuangusha chini na kumkata kwa mapanga na kusababisha kifo chake papo hapo.

Hadi tukienda mitamboni jana(Jumapili) mchana, habari kutoka ndani ya jeshi la polisi mkoani Mwanza zilisema kwamba, Kamanda mpya wa mkoa huo Varentin Mlowola, alikuwa katika eneo la tukio akiongoza timu ya askari kuwasaka wananchi hao waliojichukulia sheria mkononi.

Marehemu Mabina hadi anakumbwa na mauti hayo, alikuwa Diwani wa Kata ya Kisesa. Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Magu na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Mwanza kwa kipindi cha miak mitano, kabla ya kushindwa na Dkt Anthon Diallo katika uchaguzi mkuu wa Chama mwaka jana.
CHANZO:CCM BLOG


KIBONZO: KIPANYA AKIZUNGUMZIA MAHUSIANO



SIMBA NA YANGA ZAPEWA JEZI KWA MPAMBANO WAO WA JUMAMOSI WA NANI MTANI JEMBE

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager imekabidhi jezi kwa timu za Simba na Yanga kwa ajili ya mechi ya Nani Mtani Jembe itakayochezwa Jumamosi kuanzia saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kampeni ya Nani Mtani Jembe  iliyozinduliwa Oktoba 6 mwaka huu itamalizika Jumamosi kwa klabu za Simba na Yanga kuchuana vikali pamoja na kuwania Sh milioni 100 zilizotengwa na Kilimanjaro Premium Lager ambao ni wadhamini wakuu wa timu hizo.


George Kavishe akiwakabidhi Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itangare na Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto jezi maalum zitakazotumika kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe Jumamosi tarehe 21 Desemba. 


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meneja wa Kilimanjaro Premium Lager George Kavishe alisema wanakabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh milioni 6.8 kwa ajili ya kuzipa mwonekano mpya timu hizo katika mechi hiyo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Simba Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ aliwashukuru wadhamini hao Bia ya Kilimanjaro kwa vifaa hivyo huku akitamba timu yake kuibuka na ushindi.

Naye Ofisa Habari wa Yanga Baraka Kizuguto aliwashukuru wadhamini hao kwa kuwafanyia mambo mazuri na kuahidi kuendeleza mambo mazuri kwao na wataibuka na ushindi katika mechi hiyo.


RAISI KIKWETE AWATAKA WANANCHI KUWEKEZA KATIKA KILIMO ILI KUKUZA UCHUMI WA NCHI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Jakaya Mrisho Kikwete amesema endapo jamii itafanikiwa kuwekeza katika kilimo basi uchumi wa Tanzania utakuwa na kufanikiwa kupiga hatua katika maendeleo ya nchini.


Rais Kikwete ametoa msisitizo huo jijini Dar Es Salaam wakati wa mkutano wa saba wa baraza la Taifa la Biashara TNBC uliokutanisha taasisi binafsi na za umma kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizo za pandembili.


Kilimo ni moja ya sekta ambayo imekuwa ikisisitizwa siku hadi siku, ingawa utekelezaji wake umekuwa ukisuasua katika baadhi ya jamii za kitanzania.
 
Miongoni mwa masuala yaliyozungumzwa katika mkutano huo uliotawaliwa na viongozi kutoka taasisi binafsi na umma ni pamoja na mpango wa Matokeo Makubwa sasa ambao unaonekana kufanikiwa zaidi kutokana na ushirikiano utakaokuwepo baina ya sekta hizo.

Mkutano huo pia umejadili changamoto mbalimbali ikiwemo suala la ajira kwa vijana na namna gani sekta binafsi inaweza kuimarishwa ili iweze kuzalisha ajira.
 
Viongozi mbalimbali wa serikali na taasisi binafsi akiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mawaziri wa serikali wemehudhuria mkutano huo uliolenga kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi binafsi na za umma.

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa bodi ya Tanzania National Business Council muda mfupi kabla ya ufunguzi wa Mkutano wa TNBC uliofanyika katika hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaa.


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU