Tutawatambuaje wenye mabilioni Uswisi?
WAKATI
Serikali na Bunge zikiwa kwenye mvutano kuhusu hatua za kufuatwa
kurejesha mabilioni ya fedha za Kitanzania yaliyofichwa kwenye benki za
nchini Uswisi, swali kubwa lililopo ni kwamba ni akina hasa ambao wana
fedha huko.
Mtoaji wa hoja binafsi kuhusu suala hilo, Mbunge wa
Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, amegoma kutaja majina ya vigogo
wanaotajwa kuhifadhi fedha akitaka uchunguzi ufanyike na majina
yafahamike wakati huo, huku serikali ikimtaka ataje majina ili ipate pa
kuanzia kwenye uchunguzi huo.
Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu,
Jaji Frederick Werema, inataka kuendesha uchunguzi kuhusu madai hayo ya
Zitto lakini kwanza inataka mbunge huyo ataje majina ya baadhi tu ya
vigogo ambao ana ushahidi wamehifadhi fedha Uswisi.
Pamoja na
hayo, swali moja ni lazima lipate majibu, leo au kesho. Swali lenyewe ni
hili; ni akina nani waliokwiba fedha za Watanzania na kwenda
kuzihifadhi ughaibuni?
Niseme mapema kwamba kuwa na akaunti nje
ya nchi si dhambi. Dhambi inakuja pale inapofahamika kwamba fedha hizo
zilipatikana isivyo halali.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Uswisi iliyotolewa Juni mwaka jana, Watanzania wamehifadhi kiasi cha dola za
Marekani
milioni 178 (zaidi ya Sh bilioni 300) katika benki mbalimbali nchini
humo. Ripoti hiyo haikutaja majina, wala kiwango walichonacho watu hao
na kutokana na taratibu za kibenki za taifa hilo la Ulaya, ni lazima
kuwepo na sababu nzito za wao kutoa taarifa zozote kuhusiana na wateja
hao.
Hata hivyo,
taarifa hiyo ya Benki Kuu ya Uswisi si ya kuaminika sana kwa vile taifa
hilo linafahamika kwa kutoa taarifa zisizoaminika kuhusu kiwango hasa
cha fedha kilichohifadhiwa na wateja wake.
Kwa
mfano, wakati Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilipodai
fedha zilizoibwa na aliyekuwa rais wa taifa hilo, Mobutu Sesesseko,
zilizokadiriwa kufikia dola bilioni tano, Waswisi walirejesha dola
milioni nane tu wakidai ndiyo kiasi kilichokuwapo!
Hata
hivyo, ripoti hiyo ya Benki Kuu ya Uswisi imesaidia tu kuthibitisha
kwamba wapo Watanzania waliohifadhi mamilioni ya dola katika akaunti
mbalimbali nchini humo.
Swali linakuja ni akina nani hao? Nimefanya utafiti kidogo na yafuatayo yanaweza kusaidia kupata majina ya wahusika.
1. Mazingira ya wizi
Kwa
mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Kupambana na Ufisadi
(Global Financial Integrity, GFI), katika mataifa mengi ya kiafrika,
fedha huibwa katika mazingira makubwa matatu- rushwa, ukwepaji kodi na
mauzo ya bei za kurusha ya bidhaa au huduma mbalimbali.
Kuna
maeneo mengine madogo kama vile ‘usafishaji’ wa fedha haramu, biashara
ya silaha, dawa za kulevya na mambo mengine lakini GFI inaamini kwamba
maeneo haya madogo yanafanya kazi zaidi katika mataifa ambayo yana
serikali zisizo imara.
Kwa
vile Tanzania ina serikali imara (walau), kulinganisha na nchi kama
vile Somalia, sababu hizo tatu za awali kwa mujibu wa GFI ndizo
zinazoweza kutoa picha kuhusu ni akina waliohifadhi fedha zao nchini
Uswisi kutoka nchini mwetu.
GFI
wametoa takwimu zinazoonyesha kuwa zaidi ya dola za Marekani milioni
148 (Sh bilioni 246) huibwa Afrika kila mwaka kutokana na rushwa. Dola
milioni 50 (Sh bilioni 80) kwa ukwepaji kodi na dola milioni 30 (Sh
bilioni 48) zinazotokana na misaada kutoka kwa wahisani. Je, wapi
tuanzie kuchunguza?
2. Idara ya Usalama wa Taifa (TISS)
Kwa
mujibu wa gazeti la The Guardian la Tanzania la Juni mwaka jana, katika
kipindi cha kati ya mwaka 2001 hadi 2008, Tanzania imepoteza zaidi ya
Tsh. trilioni 1.2 kutokana na mikataba mibovu, rushwa na ununuzi wenye
kutia shaka.
Haya
yote yamefanyika wakati Idara ya Usalama wa Taifa nchini ikiwa inatazama
na katika hali ya kawaida haiwezekani kwa idara hii kutofahamu chochote
kwenye kashfa kama za ununuzi wa rada ya mtumba, Meremeta, Deep Green,
EPA na Richmond.
Kimsingi,
serikali imeshindwa kutoa maelezo kuhusu mradi wa dhahabu wa Meremeta
ikidai suala hilo lina maslahi ya taifa na vigogo kadhaa wa Idara ya
Usalama wa Taifa wanatajwa kuhusika na mradi huo.
Mwanzoni
mwa miaka ya 2000, serikali ya Uswisi ilirejesha nchini Peru kiasi cha
dola milioni 180 (Sh bilioni 288) zilizodaiwa kuhifadhiwa humo na
aliyekuwa Mkuu wa Usalama wa Taifa wa nchi hiyo, Vladimiro Montesinos,
wakati wa utawala wa Rais Alberto Fujimori.
Kwa
vyovyote vile, watu wetu wa usalama watakuwa wanajua kitu kuhusu
ufisadi wote huu. Ipo imani kwamba makachero wa Tanzania ni miongoni mwa
walio bora katika Bara la Afrika. Ni lazima TISS imulikwe ili ieleze
iwapo ilikuwa na taarifa kuhusu ufisadi uliokuwa ukifanyika lakini
taarifa hizo hazikufanyiwa kazi na watawala au yenyewe nayo ina mkono
kwenye hilo.
Kwa
sababu tayari tuna ushahidi wa Montesinos. Kwa sababu tayari serikali
imekwishakutaja usalama wa taifa kwenye ufisadi wa Meremeta.
Kuna
uwezekano mkubwa kuwa katika hizo trilioni 1.2 zilizoibwa katika
kipindi cha miaka kumi iliyopita, nyingine zitakuwa zimeangukia Uswisi.
3. Mawaziri
KWA
mujibu wa taratibu zilizopo nchini, Waziri wa Fedha anaruhusiwa kutoa
misamaha ya kodi kwa kampuni au taasisi mbalimbali pale atakapoona
inafaa.
Tayari
mawaziri wawili wa zamani wa serikali ya awamu ya tatu, Basil Mramba na
Daniel Yona Ndhira, wamefikishwa mahakamani kwa kuisababishia serikali
hasara ya Sh. bilioni 11.2 kwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni ya Alex
Stewart.
Utafiti huu
hauna haja ya kuwatia hatiani akina Mramba lakini kwa sababu GFI
inasema sehemu ya fedha zinazoibwa hupatikana kwa misamaha ya kodi huu
ni mfano mmoja wapo wa namna mtu anavyoweza kutumia mamlaka yake
kujitajirisha.
Kama
serikali imeweza kufungua mashitaka kwa mawaziri wawili tu wa zamani wa
fedha ambao hasara waliyotia imefikia kiasi cha Sh. bilioni 11.2, je
imepoteza kiasi gani kwa mawaziri wengine katika awamu tofauti za
uongozi?
Kama kweli
serikali inataka kufahamu ni akina nani wana fedha Uswisi, sehemu nzuri
ya kuanzia ni hapa kwa mawaziri wa fedha na uchumi waliopita kwenye
awamu tofauti hapa nchini.
Wengi
wa vigogo wa nchi mbalimbali waliobainika kuhifadhi fedha Uswisi
wanatoka katika nchi zenye utajiri wa maliasili kama Tanzania.
Serikali
inaweza kuangalia zoezi zima la ugawaji wa vitalu kwa kampuni kubwa za
mafuta zinazotafuta uwepo wa nishati hiyo hapa nchini na misamaha
mbalimbali iliyowahi na inayoendelea kutolewa kwa makampuni ya madini
hapa nchini.
Kuna
taarifa kwamba baadhi ya makampuni makubwa ya kigeni hutumia rushwa ili
wapewe vitalu vya gesi katika maeneo ambako kuna uwezekano mkubwa wa
kupatikana gesi kuliko mengine. Wakipewa upendeleo huo, huweka fedha
kwenye akaunti za waliowasaidia zilizo nje ya nchi.
Uchunguzi
wa hili usiishie tu kwa mawaziri bali uende hadi kwa makatibu wakuu wao
na maofisa wa ngazi za juu waliokuwa na ushawishi katika utoaji wa
misamaha, vitalu na leseni mbalimbali za uchimbaji wa madini.
Humu ndimo wanapopatikana wengi wenye fedha chafu nchini Uswisi.
4. Jeshi la Polisi Tanzania
WAKATI
‘dili’ zinapofanyika na kubainika, watu wa kwanza kupewa taarifa ni
Jeshi la Polisi kwa ajili ya kukamata watuhumiwa. Hawa ndiyo wanaoandaa
mashitaka na hawa ndiyo wataamua kuwapo au kutokuwapo kwa kesi.
Aliyewahi
kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi la Afrika Kusini, Jackie Selebi, amefungwa
jela hivi karibuni, kutokana na uhusiano wake na mhalifu maarufu nchini
humo, Glen Agliotti. Mhalifu huyo alikuwa akimpa mkuu huyo zawadi
mbalimbali na pia kumwekea fedha katika akaunti zake.
Tanzania
kwa sasa ni miongoni mwa nchi zinazokamata sana dawa za kulevya ingawa
kuna tuhuma kwamba magwiji wa biashara hizo wana mahusiano mazuri na
baadhi ya vigogo wa Jeshi la Polisi.
Tukichunguza
vizuri mabosi wa Polisi, tunaweza kupata kitu kuhusu akina nani
wamehifadhi fedha zao Uswisi au popote duniani isivyo halali.
5. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
KATIKA
kashfa ya ununuzi wa rada, jina la aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Andrew Chenge, limeibuka mara nyingi na vyombo vya upelelezi
vya Uingereza vinamtaja kama miongoni mwa wahusika wakuu wa kashfa hiyo.
Mwanasheria
Mkuu wa serikali ndiye mshauri mkuu wa serikali kwenye mikataba minono
(mikubwa) baina ya nchi na nchi au nchi na mashirika makubwa ya
kimataifa.
Yeye ndiye
anayeweza kuamua iwapo serikali iingie kwenye dili au la. Kama Chenge
na baadhi ya wasaidizi wake walitajwa kwenye kashfa ya rada, ni wazi
kwamba ofisi hii inatakiwa kumulikwa wakati serikali ikitafuta
walioficha fedha Uswisi.
Kwa
bahati nzuri, tayari inafahamika kuwa Chenge ana akaunti katika nchi za
kigeni kama ilivyobainika wakati wa uchunguzi wa kashfa ya rada.
6. IKULU
Fujimori,
Mobutu, Sani Abacha, Francosi Duvallier, Omar Bongo na Theodor Nguema
wana mambo matatu yanayowafananisha; wote waliwahi kuwa marais katika
nchi zao, walifanya ufisadi wa kutisha na wote walificha mabilioni yao
Uswisi.
Japo hii
haimaanishi kuwa waliowahi kuwa marais wa Tanzania nao wana akaunti
katika taifa hilo, sio vibaya kujiridhisha kwa kufanya uchunguzi ili
kubaini kama wanaweza kuwa wameficha fedha Uswisi.
Kwa Tanzania, marais wenyewe wako wanne tu na hivyo kuchunguza si kazi ngumu.
Ikumbukwe
kwamba rais pekee wa Tanzania kufungua ofisi ya biashara akitumia
anuani ya Ikulu, Benjamin Mkapa, alipoumwa goti takribani miaka kumi
iliyopita, alikwenda kutibiwa nchini Uswisi !
Labda
tujiulize, angewezaje kuishi kule kwa miezi mitatu bila ya kuwa na
akaunti katika mojawapo ya benki za huko? Je, ilikuw (ina) kiasi gani
cha fedha?
Kwa mfano,
Mkapa si ndiye aliyekuwa rais wakati wa ubinafsishaji? Serikali yake si
ndiyo iliyopitisha misamaha mingi ya kodi kwa makampuni ya madini? Si
mkitaka mnachunguza tu?
Tukiwa
na nia ya kutaka kujua nani ana fedha Uswisi tutajua tu. Mimi nimetoa
mchango wangu wenye pa kuanzia tu. Wengine wanaweza kutoa michango yao
kwenye maeneo mengine.