Facebook Comments Box

Sunday, October 27, 2013

PICHA YA LEO: WACHEZAJI WA YANGA NA SIMBA WASALI PAMOJA

Picha chini ni timu B ya Yanga na simba walisali pamoja baada ya pambano lao kuisha kwa suluhu ya goli moja kwa moja.
Huu ndio mchezo wa kiungwana hongereni vijana mmeonesha njia



VIONGOZI CHADEMA WAZIPIGA KAVUKAVU

 
Mwasisi wa Chadema Edwin Mtei (mwenye kofia) akizungumza kwenye mkutano wa siku tatu wa Baraza la Kanda ya Kaskazini ya chama hicho jijini Arusha juzi

Mkutano wa Baraza la Uongozi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini juzi uligeuka ukumbi wa ngumi, baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kushushiwa kipigo.
 
Mwigamba alishushiwa kipigo hicho na baadhi ya viongozi wenzake wa chama kwa madai ya usaliti na tayari amesimamishwa uongozi kwa muda usiojulikana.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas jana alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na viongozi hao wa Chadema kufikishana polisi.
 
Alikutwa na zahama hiyo mbele ya viongozi wakuu wa Chadema Taifa, Mwenyekiti, Freeman Mbowe na mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei katika Hoteli ya Coridal Spring.
 
Viongozi hao wamekuwa wakifanya ziara za aina hiyo nchi nzima, kuimarisha chama na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na uchaguzi mkuu ujao wa Rais na wabunge mwaka 2015.
 
Habari kutoka ndani ya mkutano huo zinaeleza kuwa hatua hiyo ilifuatia tuhuma kwamba Mwigamba alituma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forums, unaodaiwa kukichafua chama hicho.
 
Tukio hilo la aina yake lilitokea wakati viongozi wote wa juu wa chama hicho, wakiongozwa na Mbowe walipokuwa wakijadili mustakabali wa chama hicho, mkutano ambao ulihudhuriwa na wabunge karibu wote wa Chadema wa kanda hiyo.
 
Hata hivyo, wakati mijadala ikiendelea baadhi ya viongozi wa chama hicho, akiwamo Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema walimtuhumu Mwigamba kutuma ujumbe kwenye mtandao huo, uliokuwa ukizungumzia ufisadi ndani ya chama hicho, wakidai alitaka Mwenyekiti Mbowe kukubali kuchunguzwa.
 
Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana, Mwigamba alisema kuwa baada ya Lema kutoa tuhuma hizo aliungwa mkono na viongozi wengine na vijana waliokuwa wameimarisha ulinzi, kumvamia na kuanza kumpiga pamoja na kumnyang'anya kwa nguvu kompyuta mpakato (Laptop), aliyokuwa nayo, kisha kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi, mjini Arusha.
 
"Wamenipiga sana na kuniweka ndani, ila nashukuru Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha (OCCID), alikuja na kunitoa saa 5:00 asubuhi," alisema Mwigamba.
 
Alisema kuwa leo katika mkutano wake na waandishi wa habari ataeleza yote yaliyotokea na hatua atakazochukua, kwa kuwa yeye ni kiongozi wa juu wa chama.
 
Hata hivyo, alieleza kwamba bado anashauriana na wanasheria wake kuona kama anaweza kuwachukulia hatua waliompinga.
 
Kauli ya polisi
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema polisi wameona hakuna kosa la kisheria lililotokea hasa kutokana na malalamiko yaliyofikishwa kwao dhidi ya Mwigamba ya kukichafua chama kwenye mitandao.
 
"Hili suala la mitandao ni kubwa na lina taratibu zake sasa kusema tu umechafuliwa na iwe kesi nadhani uchunguzi unahitajika kwao, sisi tumeona haya ni mambo yao wanaweza kuyamaliza wao ndiyo sababu tulimwachia, Mwigamba," alisema Sabas.
 
Kosa analodaiwa kufanya Mwigamba
 
Akizungumzia sakata hilo jana, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema kwamba Mwigamba alibainika kutuma ujumbe kwenye mtandao wa Jamii Forums uliokichafua chama hicho, akieleza haikuwa mara yake ya kwanza kwa kiongozi huyo kufanya hivyo na kwamba walikuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu.
 
"Kilichotokea ni hicho, vijana wa Red Brigade ndio waliomtoa ukumbini, baada ya kumbaini kukichafua chama, kwani laptop yake baada ya kuchunguzwa na wataalamu wetu walijiridhisha ni yeye ndiye aliyetuma ujumbe huo," alisema Lema.
 
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alitaja tuhuma zinazomkabili Mwigamba kuwa ni pamoja na kusema uongo, kupotosha taarifa za chama na kuchonganisha viongozi kupitia mtandao wa kijamii ya Jamii Forums.
 
Katika andiko lake kwenye mtandao, Mwigamba anadaiwa kuwatuhumu viongozi wa juu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa kuwa wamechakachua katiba ya chama hicho kuhusu ukomo wa nafasi za uongozi ili kujinufaisha binafsi.
 
Golugwa alisema kuwa baada ya kubanwa kwenye kikao, Mwigamba alikiri kuandika na kurusha taarifa hizo kwenye mitandao, lakini alipotakiwa kukabidhi kompyuta yake ili ichunguzwe na wataalamu wa mawasiliano wa chama hicho aligoma, hali iliyozua tafrani kati yake na walinzi wa chama hicho (Red Brigade), waliolazimika kutumia nguvu kumdhibiti.
 
Purukushani zilivyotokea
 
Habari zaidi zinaeleza kuwa katika harakati za kutaka kumnyang'anya Mwigamba kompyuta yake, mwenyekiti huyo wa Chadema mkoani Arusha alianza kushambuliwa na baadhi ya viongozi wa Chadema, kabla ya kufanikiwa kumdhibiti.
 
Zinaeleza kuwa katika tukio hilo kulitokea pia kurushiana maneno na matusi ya nguoni kati yake na viongozi wengine wa chama hicho akiwamo Lema.
 
Baadaye Lema aliliambia gazeti hili kwamba katika purukushani hizo Mwigamba alimrushia ngumi ambayo hata hivyo aliikwepa.
 
Alisema kuwa wanakusudia kumfungulia kesi Mwigamba ya kukichafua chama chao katika mitandao ya kijamii.
 
Hata hivyo, alisema kikao chao kiliendelea jana bila ya vurugu zozote na kuweka mikakati ya kushinda majimbo yote ya Kanda ya Kaskazini mwaka 2015 na kuchukua nchi katika uchaguzi huo ujao.
 
Adhabu kwa Mwigamba
 
Katika hatua nyingine Chadema, kimemsimamisha uongozi Mwigamba kwa tuhuma za kukisaliti, kukihujumu chama hicho na viongozi wake.
 
Akitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha jana, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Israel Natse alibainisha kuwa uamuzi wa kumsimamisha Mwigamba katika nyadhifa zote za uongozi ndani ya chama ulifikiwa na kikao cha Baraza la Uongozi wa Kanda ya Kaskazini kilichokutana juzi.
 
Alisema kuwa Mwigamba amesimamishwa kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na kuonya kuwa iwapo tuhuma zitathibitishwa, hatua nyingine za kinidhamu zitafuata kulingana na kanuni na katiba ya Chadema.
 
"Kwa sasa Mwigamba anatuhumiwa kuvunja sura ya kumi, kifungu cha 10.1 kifungu kidogo cha 8, 9 na 10 ya katiba ya Chadema inayozungumzia maadili ya uongozi," alisema Natse.
 
Akifafanua zaidi alisema kuwa sura na vifungu hivyo vinakataza kiongozi wa chama hicho kutoa tuhuma dhidi ya viongozi wenzake bila kufuata vikao halali vya kikanuni na kikatiba.


YANAYO ENDELEA KWENYE MSIBA WA BABA YAKE WEMA SEPETU

Mama mzazi wa Wema akiwa na simanzi baada ya kuondokewa na mumewe mzee Sepetu.
Kajala Masanja (kushoto), Wema Sepetu (katikati) na Zamaradi Mketema (kulia) wakiwa katika hali ya majonzi nyumbani kwao Wema Sepetu, Sinza - Mori jijini Dar.





Wema Sepetu akibubujikwa na machozi baada ya kuondokewa na baba yake mzazi.
STAA wa sinema za Kibongo na Miss Tanzania 2006 Wema Isaac Sepetu, bado yuko kwenye wakati mgumu baada ya leo asubuhi kupatwa na msiba mkubwa wa kuondokewa na baba yake mzazi Balozi Isaac Abraham Sepetu aliyefariki asubuhi ya leo.
 
 Kwa sasa kuna watu wengi wamefika kumjulia hali maeneo ya Sinza, Mori jijini Dar, rafiki yake wa karibu Kajala Masanja na Zamaradi Mketema wapo bega kwa bega kuwa naye karibu na vilio vimetawala kila kona ya familia ya marehemu Balozi Sepetu.
Bado haijafahamika mazishi yanafanyika lini maana wanasubuliwa watoto wa Marehemu Tunnu Sepetu na Sunna Sepetu ambao wanaishi nchini Marekani, lakini kuna tetesi kuwa huenda mazishi hayo yakafanyika siku ya Ijumaa. 
 
Mama mzazi wa Wema bado yuko kwenye hali ya huzuni baada ya kufiwa na mume wake ambaye amedumu nae kwa miaka mingi kabla ya kupatwa na mauti asubuhi ya leo katika hospitali ya TMJ jijini Dar. Mpaka mauti yanamfika, marehemu alikuwa akisumbuliwa na kisukari pamoja na kiharusi.


UCHAGUZI TFF: WAANDISHI WA HABARI WAFUKUZWA UKUMBINI

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA),Juma Pinto akizungumza na Waandishi wa Habari jioni hii nje ya Ukumbi wa Mikutano wa Water Front,kunakofanyika Uchaguzi wa Rais na viongozi mbali mbali wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) ambapo hadi sasa hakuna Mwandishi yeyote alieruhusiwa kuingia kwenye Ukumbi huo kwa madai kwamba Waandishi hawausiki na Uchaguzi huo,kwani waandishi jukumu lao ni kusubiria kupewa matokeo tu ya uchaguzi huo,kauli iliyotolea na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi,Ndg. Hamidu Mbwezeleni.Jambo hilo liezua tafrani kidogo kwenye Eneo hilo hasa pale Watu wa Usalama (Polisi) walipowataka Waandishi kuondoka kwenye Eneo hilo la Uchaguzi.Mwenyekiti wa TASWA,Juma Pinto amewataka Waandishi wa Habari kuachana na Uchaguzi huo na kutoripoti chochote,kwani kilichoonyeshwa ni dharau kubwa kwa waandishi wa Habari na watanzania wote nchini wanaopenda Michezo


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU