Facebook Comments Box

Thursday, July 3, 2014

MTOTO AFUNGIWA KWENYE BANDA LA MBUZI KWA MIAKA 10

Mwenyekiti wa Umoja wa Watu wenye Ulemavu Kenya, David Sankok akionyesha hali halisi ya maisha ya mtoto huyo kabla ya kuokolewa. Picha na Ndaya Mgoyo Juni 21 ilikuwa ni siku ya kawaida kwa Mama Nancy mkazi wa Narok nchini Kenya, lakini ilifichua siri nzito ya mtoto aliyefichwa kwa miaka kumi katika banda la mbuzi.Akiwa katika shughuli zake za nyumbani, mara akatokea mtoto mdogo wa jirani yake aitwaye Jane. 
     
Binti huyo akaanza kucheza na wenzake kwa dakika kadhaa na mara akaacha michezo na kuanza kukimbia kuelekea nyumbani kwao.Wenzake wakamuuliza “mbona unakimbia wakati bado tunacheza”. Akajibu, “nakwenda kwenye banda la mifugo kumpa chakula Ben. Muda umekimbia na hakuna mtu nyumbani”.Kwa kauli hiyo, mwanamke huyo alitaka kujua iwapo Ben anaishi kwenye nyumba ya jirani yake kwani ni miaka 10 imepita tangu amtie machoni.“Ben yupo na anaishi kwenye banda la mifugo. Huwa anahudumiwa na mama, lakini kwa sasa mama hayupo na baba amekwenda kazini. Mimi nina jukumu la kumpa chakula,” alijibu Jane.

Mama huyo akapata shauku ya kumtembelea mtoto huyo kuona kinachoendelea kwa jirani zake, Lo! anachokiona haamini macho yake; Mtoto Ben amefungwa kwa kamba kwenye kigodoro chembamba akiwa hajiwezi kwa njaa. Hivyo ndivyo alivyoibuliwa mtoto Ben baada ya kukaa katika banda la mbuzi kwa muda wa miaka 10 bila majirani kufahamu. 

Ben, ambaye kwa sasa ana miaka   miaka 14 alizaliwa akiwa kiziwi, bubu   na ulemavu. Aibu ya kuzaa mtoto kama huyo ndiyo ilifanya wazazi wake wamfungie kwenye zizi la wanyama kwa muda wa miaka 10 na wakihakikisha  hakuna jirani wala ndugu wa karibu anayefahamu juu ya tukio hilo. Historia ya mtoto huyo Kwa mujibu wa baba mlezi Mr Jeremiah Mbusia,  ambaye ni askari katika Wizara ya Mali Asili, Narok Kenya, mtoto  huyo siyo wake wa
kuzaa bali alifika katika nyumba hiyo miaka 12 iliyopita akiwa na mama yake wakati huo mtoto huyo alikuwa na miaka minne.

 Alilelewa katika nyumba hiyo kwa miaka miwili na ndipo wazazi wake, yaani baba yake wa kambo na mama yake mzazi wakaamua kumuweka katika kibanda kidogo nje ya nyumba yao  na hutumiwa
kama zizi la mbuzi na kondoo. Maisha ndani ya  zizi Akiwa kwenye zizi mtoto huyo aliwekewa godoro ukutani na mkono wake mmoja ulifungwa kwa kamba ukutani. Ilikuwa ni vigumu kuvumilia harufu kali kutoka katika zizi hilo kwani kulikuwa na mchanganyiko wa kinyesi na mikojo ya binadamu na wanyama.

Wadogo zake Ben walisema kuwa wazazi wao huwa wanamsafisha mtoto huyo wakati wowote wanaotaka na kuwa anaweza kushinda na kinyesi au kulala nacho. “Ni mara chache kukuta akisafishwa   mara mbili kwa siku. Kwa kawaida husafishwa mara moja tu na wakati mwingine hasafishwi kabisa,” alisema mtoto huyo. 

Kwa nini ilikuwa rahisi kujulikana? Ugunduzi wa mtoto huyo ulitokana na ukweli kwamba mama yake aliamua kuondoka nyumbani na kuacha familia nzima kutokana na ugomvi na mume wake. Mama huyo alikuwa akifanya siri ya kulinda mtoto huyo asijulikane hapo nyumbani na alipoondoka watoto wenzake ndiyo walikuwa na jukumu la kumlisha mwezao. Kauli ya baba mlezi Kwa kujibu wa baba wa kambo, mama wa mtoto huyo alikuwa hamtaki mwanaye kwani aliamini kwamba kuishi naye ni kuongeza mikosi.

 Baada ya kuishi pamoja walijikuta wakiwa wamezaa watoto watatu na mama huyo aliona kuwa watoto hao ndio walikuwa muhimu katika maisha yake kuliko Ben, ambaye alimzaa na mwanaume mwingine kabla ya kuolewa katika ndoa rasmi. “Mama yake alikuwa hampendi na hata wazo la kumweka katika banda lilitoka kwake. Aliamini kuwa kukaa naye ndani kama watoto wa kawaida ilikuwa ni usumbufu na akitoa visingizio kwamba akikaa ndani anaweza kuvunja vitu na kuwa anaweza kushika vitu vya hatari kama vile moto,” alijitetea baba mlezi wa Ben. 

“Tulikosana na mama watoto kwa ugomvi wa kawaida tu katika familia, hiyo ilikuwa ni miezi minne iliyopita, ajabu ni kwamba amenikimbia na kuniachia familia akiwamo mtoto mlemavu.”

“Nashindwa kumlea vizuri kwa kuwa natakiwa kwenda katika mihangaiko yangu ndiyo maana wadogo zake walikuwa wakimhudumia wakati sipo.” Imefahamika kuwa mwanamke huyo amekimbilia kwao eneo la Rimuru, Kenya ambapo ni kwa wazazi wake na akiwaambia jamaa zake wa karibu kuwa hawezi kurudi katika nyumba ya mume wake kwani hawapatani. 

Kauli za majirani Majirani wanasema walikuwa wakifahamu kuwa nyumbani kwa jirani yao kuna mtoto mwenye ulemavu wa akili lakini hawakumwona kwa muda mrefu. 

“Tulikuwa tukifahamu kwamba kuna mtoto mlemavu wa akili lakini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita hatukumwona. Tulidhani wamemhamishia sehemu nyingine. Ilikuwani vigumu kusikia sauti
kwa kuwa mtoto mwenyewe ni bubu na kiziwi,” alisema jirani mmoja. Kumuokoa Ben Baada ya majirani kupata taarifa za kuwepo kwa mtoto huyo, walimuita mwandishi wa habari mmoja ili kushuhudia hali halisi.

Mwandishi huyo alitoa taarifa polisi na pia kwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu Kenya, Dk David Ole Sankok na kwa pamoja walivamia katika nyumba hiyo iliyopo Fanaka Estate, Narok na kumwokoa mtoto huyo katika mateso.

 Baada ya kumtoa kwenye kibanda hicho waligundua kuwa hali ya mtoto huyo haikuwa nzuri kwani alikuwa amepooza upande mmoja wa kushoto kutokana na kulala kwa muda mrefu, viungo vyake vilikuwa vimejikunja kutokana na kukosa lishe kwa siku nyingi na nywele zake zilibadilika rangi kutokana na kutokaa kwenye mwanga wa jua kwa muda mrefu. “Alikuwa akitoa harufu kali, ilikuwa ni vigumu hata kumsogelea, lakini kwa kuwa tulikuwa tumedhamiria kumwokoa ilibidi tufanye hivyo,” akasema Dk Ole Sankok. “Tulimkuta katika mateso makubwa sana, eneo alilokuwa amelala lilikuwa na kunguni, chawa na viroboto wengi,” anasema.

Anaongeza kuwa wadudu hao walipokuwa wakimsogelea kinywani
alikuwa akiwatafuna na kuwameza kwani alikuwa na njaa muda wote.“Nilipoona hali hiyo nilijaribu kuondoa viroboto waliokuwa karibu na mdomo wake, kwa kuwa alikuwa amewazoea sana na aliona ni kama kitoweo chake alitoa sauti ya ukali kuashiria kwamba nisiwatoe, nilipojaribu kuwatoa kwa nguvu alitaka kuniuma kwa meno,” alisema daktari huyo. 

Wazazi wa kijana huyo walikuwa hawaaniki godoro nje kwani
hawakua na jingine la kumtandikia pia walihofia majirani huenda wangehoji. Huduma ya kwanza Baada ya kugunduliwa, Ben alipelekwa katika Hospitali ya Mji wa Narok kwa ajili ya matibabu. Alipewa huduma za haraka ikiwa ni pamoja na huduma za kurudisha afya mwilini kwa vyakula vya protini na vitamini.

 Vilevile alikuwa akianikwa juani mara kwa mara kwa lengo la kumrudishai vitamini. Kwa kuwa mgongo wa mtoto huyo ulianza kutoa vidonda alipewa matibabu ya vidonda. “Mtoto huyo alikuwa amepungua mwili kwa kiasi kikubwa  ilikuwa unaweza kumbeba kama mtoto mdogo. Hata   rangi yake ya ngozi ilibadilika,” alisema Dk Sankok, ambaye pia anaendesha kliniki binafsi katika mji wa Narok. “Licha ya kuwa na umri wa miaka 14 alikuwa na kilo 15 pekee,” aliongeza.

Sankok aliwahakikishia watu waliomzunguka mtoto huyo kwamba
atamfikisha katika kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa akili na viungo na atampa mazoezi ya kutosha kuhakikisha anarudi
katika hali ya kawaida.

“Unajua kuna wazazi ambao wana kawaida ya kuwaficha watoto
wao kwa sababu wana matatizo ya viungo ama   ya akili. Hilo siyo
jambo zuri hata kidogo, watoto kama hao ni binadamu wa kawaida
na wanatakiwa kulelewa kwa misingi yote ya kibinadamu,” anasema.

Anasema kama mzazi anaona hawezi kumhudumia mtoto kama
huyo ni bora amfikishe katika vituo vya kulea watu wa aina hiyo
kuliko kumficha ndani na kumpa mateso makubwa.
Chanzo: Mwananchi


AZAM WASAJILI MSHAMBULIAJI WA HAITI

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Haiti, aliyecheza Kombe la Mabara mwaka jana nchini Brazil, Leonel Saint-Preux ametua Azam FC kwa ajili ya kujiunga nayo kwa msimu ujao.

Kocha Joseph Marius Omog raia wa Cameroon amesema amekuwa na mchezaji huyo kwa siku mbili na atahitaji muda zaidi kumuona kabla ya kuamua kumsajili au la. Mshambuliaji huyo aliyezaliwa Machi 12, mwaka 1985 in Cap-Haitien mara ya mwisho alichezea klabu ya FELDA United F.C. ya Ligi Kuu ya Malaysia.

Preux alianzia Zenith ya kwao,ambako alikuwa mfungaji mzuri katika Ligi ya nchini humo. Saint-Preux alisaini Minnesota Thunder ya Daraja la Kwanza Marekani Aprili 15, mwaka 2009, kabla ya kuhamia Hanoi ya Vietnam.

Machi 2010 alisiani mkataba wa awali na Aztex, lakini akatemwa baada ya kufeli vipimo vya afya. Kimataifa Saint-Preux, alianzia kuchezea timu za vijana za Haiti wa umri tofauti. Alikuwemo kwenye kikosi cha Haiti kilichofuzu michezo ya Olimpiki mwaka 2008 mjini Beijing, akifunga bao la kukumbukwa kutoka umbali wa mita 40 timu yake ikishinda 2-1 dhidi ya Canada.

Alianza kuchezea timu ya wakubwa ya Hati mwaka 2007. Alifunga
bao lake la kwanza timu ya taifa ya Haiti Novemba 19, mwaka 2008 katika sare ya 1-1 Surinam. Haiti ilifungwa 10-0 na Hispania kwenye michuano.
Hii ndio mechi ambayo Haiti ilitandikwa goli 10 kwa 0 mshambuliaji huyu wa azam anaonekana akikabwa na beki ya Hispania ambayo imeonesha udhaifu mkubwa kwenye kombe la dunia linalo endelea Brazil hivi sasa. Katika mechi hiyo mshambuliaji huyu mpya wa azam hakuweza kumsaidia timu yake kabisa.
CHANZO: BIN ZUEIRY


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU