Facebook Comments Box

Saturday, October 5, 2013

HAMIS TAMBWE AENDELEA KUWA KINARA WA UFUNGAJI HUKU RUVU IKIIPUNGUZA KASI SIMBA TAIFA


Hamis Tambwe akishangilia moja ya mabao yake.

LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara imeendelea leo, huku vinara Simba SC wakipunguzwa kasi kwa sare ya 1-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Ruvu ndiyo waliokuwa wakwanza kupata bao la kuongoza katika dakika ya nane tu ya mchezo kupitia kwa Saidi Dilunga 'Said Magoli' na Simba kusawazisha kwa penati katika dakika ya 51 ya mchezo baada ya Betram Mombeki kuangushwa ndani ya eneo la hatari ndipo Hamis Tambwe alipoukwamisha mpira wavuni na kufunga bao lake la nane katika ligi ya vodacom Tanzania Bara.
 
Hata hivyo, wachezaji wa Ruvu Shooting walimzonga refa Mohamed Theophil wakipinga penalti hiyo, kabla ya kulainika na kukubali ipigwe na Mrundi Tambwe akaenda kufunga bao lake la nane ndani ya mechi saba katika msimu wake wa kwanza Simba SC.
 
Matokeo hayo, yanaifanya Simba SC itimize pointi 15 baada ya mechi saba na kuendelea kushikilia usukani wa Ligi Kuu. 
 
Beki wa Coastal Union, Juma Nyosso akimdhibiti mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco 'Adebayor' katika mchezo wa leo, Uwanja wa Mkwakwani.   



Azam pia wakitoka sare ya bila kufungana na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ikiwa ni sare yao ya nne katika ligi hii, sare zingine ni zile za mechi kati ya Mtibwa & Kagera Sugar na ile ya Ashant.
 
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga mechi ilikuwa kali, ilitawaliwa na vurugu za mashabiki tangu hata kabla mchezo haujaanza. Kosa kosa zilikuwa za pande zote mbili, safu ya ushambuliaji ya Coastal ikiongozwa na Mganda, Yayo Lutimba na Pius Kisambale na Azam ikiongozwa na John Bocco, Mganda Brian Umony na Kipre Tchetche wa Ivory Coast.

Refa Andrew Shamba aligeuka kituko kipindi cha pili, baada ya kuwapa kona isiyostahili Azam na ilipopigwa wakafanikiwa kupata bao, lakini akakataa bao hilo.

Baada ya kutoa kona hiyo, beki wa Azam Erasto Nyoni alienda kupiga vizuri ikaunganishwa nyavuni na John Bocco kwa kichwa dakika ya 71, lakini Shamba akaamuru mpira uwekwe chini upigwe kuelekea lango la Azam- kana kwamba kuna faulo ilichezeka.

Mshika kibendera namba mbili, Hassan Zani alisababisha mchezo kusimama kwa dakika tatu ili apatiwe huduma ya kwanza, baada ya kupigwa chupa na mashabiki wa Coastal Union dakika ya 43.

Beki wa kulia wa Coastal Union, Hamad Hamisi alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 70 baada ya kumpiga kichwa Kipre Tchetche wa Azam FC. Tukio hilo lilifuatia  majibizano na kusukumana kwa wachezaji hao.

Mshambuliaji wa Azam, Kipre Tchetche alikutana na ‘mvua’ ya chupa dakika ya 73 akiambaa kuelekea langoni mwa Coastal Union, jambo ambalo lilimfanya refa asimamishe mchezo na kuomba Polisi waende kusimama mbele ya jukwaa la mashabiki wa Coastal.
 
Baada ya mchezo huo, mashabiki wa Coastal walitoka jukwaani na kuwafuata marefa, lakini Polisi walifanikiwa kuwadhibiti.

Kikosi cha Coastal Union kilikuwa; Shaaban Kado, Hamad Hamisi, Othman Tamim, Mbwana Hamisi ‘Kibacha’, Juma Nyosso, Jerry Santo, Uhuru Suleiman/Yussuf Chuma dk79, Crispin Odula, Pius Kisambale/Suleiman Kassi ‘Selembe’ dk64, Yayo Lutimba na Keneth Masumbuko.

Azam FC; Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Said Mourad, Aggrey Morris, Kipre Balou, Brian Umony/Seif Abdallah dk69, Salum Abubakar, John Bocco, Humphrey Mieno na Kipre Tchetche.
 
Na katika Uwanja wa Chamazi kulikuwa na mechi kati ya JKT RUVU na Kagera Sugar ambapo Kagera Sugar imefungwa mabao mawili kwa sinia na wenyeji wao.
 
Nayo timu iliyokuja kwa kasi katika ligi hii Mbeya City ilikuwa wageni wa JKT Oljoro ambapo wageni hao Mbeya City wameibuka na ushindi wa mabao mawili dhidi ya moja la wenyeji wao.


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU