Facebook Comments Box

Thursday, February 28, 2013

KESI YA MAUAJI YA MWANGOSI ASKARI WAWAZUIA WANAHABARI


SAKATA la mtuhumiwa wa mauwaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten mkoani Iringa marehemu Daudi Mwangosi askari wa FFU mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simoni (23), limeendelea kuchukua sura mpya baada ya wanahabari kunusurika kupigwa na askari polisi ambao walikuwa wakiwazuia kusogea katika chumba cha mahakama kusikiliza kesi hiyo. Askari polisi hao wakiwa zaidi ya 10 walitumia nguvu za ziada katika kuwadhibiti wanahabari wa vyombo mbalimbali waliofika kusikiliza na kuripoti mwenendo wa kesi hiyo namba 1 ya mwaka 2012 ya mauwaji ya mwanahabari mwenzao, Mwangosi aliyeuwawa Septemba 2 mwaka 2012 katika kijiji cha Nyololo wilaya ya Mufindi wakati wa polisi walipokuwa wakitumia nguvu kuwatawanya wafuasi wa chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) aliokuwa katika shughuli za ufunguzi wa matawi ya chama hicho. Hata hivyo moja kati ya mbinu waliyopata kuitumia leo wakati mtuhumiwa huyo akifikishwa mahakamani hapo ni kuwafukuza waandishi wa habari eneo hilo la mahakama na kumtoa mtuhumiwa huyo kwa kificho cha hali ya juu kwa kumweka katikati ya watuhumiwa wa makosa mingine zaidi ya 8 huku mtuhumiwa akijificha sura yake kukwepa kamera za waandishi na baadhi ya askari wakimkinga ili kukwepa kupigwa picha. Tukio hilo lilitokea muda wa saa 6.10 mchana wakati mtuhumiwa huyo askari alipokuwa akitolewa na watuhumiwa wengine kutoka chumba cha mahabusu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Iringa na kumpeleka katika chumba cha Mahakama ya wazi kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa tena. Hivyo katika hali ya kushangaza ni pale askari hao kuwataka wanahabari hao kusongea umbali wa meta 700 kutoka eneo la Mahakama hiyo wakati mtuhumiwa huyo akiingizwa katika chumba cha Mahakama ya wazi mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa wa Iringa, Gladys Barthy ili kesi hiyo iweze kutajwa kwa zaidi ya mara ya tano sasa bila upelelezi kukamilika. Uamuzi wa askari hao uliwashangaza hata baadhi ya wananchi waliofika kusikiliza kesi na kuwawekea dhamana ndugu zao na kulazimika kuungana na wanahabari kupinga uamuzi huo na kusababisha askari kuwafukuza pia wananchi hao na kuwataka waungane na wanahabari kuondoka eneo hilo la chumba cha mahakama. Hakimu mkazi mkoa wa mkoa wa Iringa mheshimiwa Barthy alisema kuwa kitendo kilichofanywa na polisi hao kuwazuia wanahabari si maagizo ya Mahakama na kuwa wanahabari hao walikuwa huru kuingia kusikiliza kesi hiyo na kuhabarisha umma kwani hakukiwa na siri wala hakuna maagizo ya mahakama ya kuwataka polisi kuwafukuza wanahabari mahakamani hapo. “Kwanza nawapa pore sana kwa misukosuko mlioipata ....ila mimi nilikuwa ndani ya mahakamani sikujua kinachoendelea huko nje ya mahakama ila nawahakikishieni kuwa kesi hii ilikuwa ikisikilizwa katika mahakama ya wazi na mlikuwa huru kusikiliza,” alisema hakimu huyo akiakimhoji mmoja kati ya viongozi wa polisi kuhusu polisi hao kunyanyasa wanahabari na kuwataka kutorudia kufanya hivyo tena. Mwendesha mashitaka wa serikali Blandina Manyanda aliiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo na kuwa upelelezi bado haujakamilika na mahakama hiyo kupanga tarehe 14 machi ambapo kesi hiyo itafikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

SOURCE: WAVUTI



Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU