Facebook Comments Box

Thursday, October 25, 2012

POLISI WADAIWA KUTOROSHA MTUHUMIWA

MKAZI mmoja wa Kijiji cha Kogaja kata ya Goribe wilayani Rorya mkoani Mara Bw. Hamisi Omenda (33) amedaiwa kumuua kikatili mke wake Bi. Levina Hamisi (27) kwa kumkatakata kwa panga na kisha kutoroka, huku Polisi wakidaiwa kushiriki katika utoro huo kwa kuandaa mazingira ya kutoroka. Polisi wa kituo cha Kogaja wanadaiwa kuhusika na utoro huo kwa kile kilichodaiwa kuwa hawakumkamata mtuhumiwa licha kufika kituoni hapo kuchukua PF3 baada ya kufanya kitendo hicho. Hata hivyo, taarifa kutoka Kituo cha Polisi Kogaja zimedai kuwa Mtuhumiwa alitoa maelezo kuwa mkewe alikatwakatwa mapanga na watu wasiofahamika hivyo aliomba PF3 kwa ajili ya kumpeleka marehemu katika Hospitali ya Tarime mjini Tarime. Utetezi huo unadaiwa kuwa ni njama ya Polisi kwa kuwa wanayo mahusiano wa kibiashara na mtuhumiwa huyo. Akizungumza na waandishi wa habari, Mtendaji wa Kijiji cha Kogaja, Bw. Lukas Ambonya alikiri Bw. Omenda kuhusika katika tukio hilo na kwamba wakiwa njiani kwenda hospitalini mke wake alifariki na yeye kutokomea kusikojulikana hivyo hakuwepo hata wakati wa maziko. Kitendo hicho kiliwakasirisha ndugu wa marehemu ambapo juzi wakati wa maziko walitishia kuvamia kituo cha Polisi na kutaka kuchoma baadhi ya nyumba za ndugu wa mtuhumiwa kijijini hapo. Alisema chanzo cha mauaji hayo ni marehemu kutofautiana na Mumewe siku ya Jumamosi asubuhi, tarehe 20 Oktoba, 2012, (tofauti ambayo haijawekwa bayana), na marehemu baada ya kuhisi hali ya hatari alikimbia kutoka nyumbani hapo. Hata hivyo mume wake Bw. Omenda aliwatuma baadhi ya vijana kwa pikipiki waolifanikiwa kumkamata na kumrudidha nyumbani ambapo majira ya saa 4 asubuhi siku hiyo alimfungia ndani na kuanza kumkatakata kwa panga. “Sisi tunasema haya kwa sababu tunaishi kijijini hapa na Bwana huyu ana mahusiano makubwa na polisi hawa , ndio maana hawakutaka kumtia ndani badala yake walisaidia kuandaa njama za kutoroka kwake ..yeye alipeleka mke wake hospitalini akiwa marehemu” alisema mkazi mmoja ambaye hakutaka kutaja jina. Marehemu hajaacha watoto. Polisi inawashikilia baadhi ya ndugu wa mtuhumiwa kwa mahojiano zaidi.

Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU