UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi ya Sh.
milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam, Sheikh
Ponda Issa Ponda na wenzake 49 wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu Dar es Salaam imuone Ponda na wenzake wanakesi ya kujibu kwa
sababu umeweza kujenga kesi yao.
Kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya
upande wa Jamhuri unaowakilishwa na wakili Mwandamizi wa Serikali
Tumaini Kweka na Inspekta wa Polisi, Hamisi Said na upande wa utetezi
unaowakilishwa na Juma Nassor na Njama kuwasilisha majumuisho yao kwa
njia ya mdomo ya kuomba mahakama iwaone washitakiwa wanakesi ya kujibu
au la.
Kweka ambaye alitumia dakika kumi tu kuwasilisha
majumuisho alidai upande wa Jamhuri umeweza kujenga kesi yake kupitia
mashahidi wake 16 na vielelezo 13 walivyovileta mahakamani ambapo
waamini kisheria vitawafanya washitakiwa wapande kizimbani kujitetea.
Wakili
wa utetezi Nassor Juma akiwasilisha majumuisho yake, aliomba mahakama
iwaone washitakiwa hawana kesi ya kujibu na waachiliwe huru kwa sababu
upande wa Jamhuri umeshindwa kujenga kesi yao.
Nassor alidai
wanachokiona katika kesi hiyo ni kuwa kuna mgogoro wa ardhi ambao
ulitakiwa ukatatuliwa kwanza na Mahakama ya Ardhi kwa mujibu wa kifungu
cha 167 cha Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999, “Sisi upande wa utetezi
tunaiomba mahakama hii iwaachilie huru washitakiwa wote na iwaone hawana
kesi ya kujibu kwas ababu kesi hii imefunguliwa kwa jazba na polisi na
upande wa Jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi ambao utaweza kuishawishi
Mahakama iwaone washitakiwa wote wana kesi ya kujibu,” alidai wakili
Nassor.
Hakimu Nongwa aliarisha kesi hiyo hadi Machi 4 mwaka huu,
ambapo atakuja kutoa uamuzi wa ama kuwaona washitakiwa wana kesi ya
kujibu au la na kuamuru Ponda na Mkadamu warudishwe rumande kwa sababu
bado Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk Eliezer Feleshi hajaondoa hati
yake ya kuwafungia dhamana.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog