Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete leo, aliungana na mamia ya
waombolezaji kumzika Mbunge wa Jimbo la Nyasa na msanii mahiri wa muziki
nchini, Mheshimiwa Kepteni John Damiano Komba, kwenye makaburi ya
Kanisa Katoliki katika Kijiji cha Lituhi, Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa
Ruvuma.
Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa
Ndege wa Songea, akitokea Dar es Salaam, kiasi cha saa tano na robo
asubuhi, Rais Kikwete alikwenda moja kwa moja Lituhi, karibu kiasi cha
kilomita 140 kutoka mjini Songea, kwa ajili ya mazishi ya Mheshimiwa
Komba ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya
Chama cha Mapinduzi (CCM).
Rais Kikwete alijiunga
na waombolezaji akiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda kiasi cha saa tisa mchana kwa
ajili ya mazishi hayo.
Shughuli za mazishi za kidini ziliongozwa na Askofu John Ndimbo wa
Jimbo Katoliki Mbinga.
Mwili wa
Marehemu Komba uliteremshwa kaburini saa 9:30 mchana huku ukishuhudiwa
na mjane wa marehemu Salome Komba na watoto wake 11.
Rais
Kikwete ameondoka Lituhi mara baada ya mazishi kurejea mjini Songea
kumalizia ziara yake ya siku mbili ya kikazi mkoani Ruvuma.