Facebook Comments Box

Wednesday, March 4, 2015

KAPTENI KOMBA AZIKWA KIJIJINI LITUHI HUKU RAIS JAKAYA KIKWETE AKIONGOZA MAZISHI HAYO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, aliungana na mamia ya waombolezaji kumzika Mbunge wa Jimbo la Nyasa na msanii mahiri wa muziki nchini, Mheshimiwa Kepteni John Damiano Komba, kwenye makaburi ya Kanisa Katoliki katika Kijiji cha Lituhi, Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma. 

Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Songea, akitokea Dar es Salaam, kiasi cha saa tano na robo asubuhi, Rais Kikwete alikwenda moja kwa moja Lituhi, karibu kiasi cha kilomita 140 kutoka mjini Songea, kwa ajili ya mazishi ya Mheshimiwa Komba ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM). 

Rais Kikwete alijiunga na waombolezaji akiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda kiasi cha saa tisa mchana kwa ajili ya mazishi hayo. 
 
Shughuli za mazishi za kidini ziliongozwa na Askofu John Ndimbo wa Jimbo Katoliki Mbinga.

Mwili wa Marehemu Komba uliteremshwa kaburini saa 9:30 mchana huku ukishuhudiwa na mjane wa marehemu Salome Komba na watoto wake 11. 

Rais Kikwete ameondoka Lituhi mara baada ya mazishi kurejea mjini Songea kumalizia ziara yake ya siku mbili ya kikazi mkoani Ruvuma.



Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU