Kanali Ali Mahfoudh ni Mmoja wa Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania, JWTZ waliotajika sana kwa Miaka hii 50 ya Jeshi letu hili,
viza Ushupavu, Ushujaa na Umahiri wake Vitani zikielezewa kwa Vijana
na kuwashajiisha wengi kutamani kuingia Jeshini kufuata njia yake
njema ya Utumishi wa Kutukuka, Kujituma, Weledi, Ushupavu na
Ushujaa.
Akifanya kazi njema ya Ukombozi tokea Mapinduzi ya Zanzibar
ambapo vipawa vyake na Umahiri wake Jeshini lionekana mwanzoni
tu, japo kwa kuwa naye alisomea Ukomandoo wa Kijeshi Nchini Cuba
alihusishwa zaidi na kundi la Makomredi wa Umma Party chini ya
Profesa Abdulrahman Mohammed Babu na Mzee Ali Sultan Issa.
Mara baada ya Mapinduzi na kuundwa Muungano wa Nchi za
Tanganyika na Zanzibar, Kanali Ali Mahfoudh na wengi wa Makomredi
wenziwe waliingizwa kwenye Serikali ya Muungano na kuondolewa
kabisa Zanzibar kwa kukhofiwa kwa Ujemedari wao, Usomi wao na
"Utata" wao.
Kanali Ali Mahfoudh alikuwa Mkurugenzi wa Operesheni wa Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ kuanzia Mwaka 1964
alipohamishiwa Bara mpaka Mwaka 1972. Mwanajeshi huyu ni mmoja
wa askari waliopata umaarufu sana katika JWTZ kwa utumishi wao,
Wengi wamesikia jina lake, lakini wachache wamepata kumuona kwa
sura na hao waliobahatika kumuona wakikiri kwamba "alikuwa na sura
nzuri" lakini alikuwa Shupavu hasa.
Kanali Mahfoudh alipata Umaarufu zaidi kati ya Mwaka 1964 - 1972
katika kuvisaidia Vyama vya Ukombozi vya Afrika kama FRELIMO,
ZANU, ZAPU na MPLA katika vita vyao vya Msituni vya Ukombozi wa
Nchi zao, na pia akitajwa kuwa ndiye aliyeongoza Kikosi cha JWTZ
katika RABSHA moja Maarufu dhidi ya Uchokozi wa Rais Kamuzu
Banda wa Malawi.
Wakati wa Mapambano ya Frelimo kudai Uhuru kutoka kwa Waremo
Kanali Mahfoudh alijichimbia Nachingwea akiwasapoti Majemedari wa
Msumbiji Albarto Sipande na Raymundu Pasinuwapa katika ukombozi
wa nchi hiyo kutoka Mikononi mwa Wakoloni hao waonevu.
Kati ya Mwaka 1972 mpaka mwaka 1978 aliwekwa kizuizini Jijini Dar
es salaam kwa Tuhuma za kuhusika na Mauaji ya Rais wa Kwanza wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Makamo wa Rais wa Kwanza wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheikh Abedi Amani Karume na
akahukumiwa Kifo katika Kesi ambayo iliendeshwa Zanzibar bila yeye
kuwepo.
Wengine waliotiwa Kizuizini pamoja naye ni Profesa Abdulrahman
Mohammed Babu, Tahir Ali Salim, Hashil Seif Hashil, Salim Saleh
Salim, Ali Yusuf Baalawi, Hemed Hilal Mohammed, Suleiman
Mohammed Abdullah, Amour Mohammed Durgheish, Ahmed
Mohammed Habib, Haji Omari Haji, Saleh Abdallah, Abdallah Juma
Khamis, Ali Salim Hafidh, Shaaban Salim Mbarak, Badru Said, Ali
Mohammed Ali na Abdulaziz Abdulkadir Ahmed, Makomredi wengine
kama Ali Sultan Issa, Sharifu Ahmad Badawy Qullatein na wenziwao
walishikiliwa Zanzibar.
Baada ya Mbinyo mkali wa Shirika la Haki za Binaadam la Amnesty
International na Mataifa ya Kigeni juu ya kushikiliwa kwao, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Julius Kambarage Nyerere
alitoa amri ya kuachiwa kwa Kanali Ali Mahfoudh na Makomredi
wenzie Tarehe 26, Mwezi Aprili Mwaka 1972.
Mara baada ya kutolewa Gerezani Kanali Ali Mahfoudh alichukuliwa na
Serikali ya Msumbiji kwa Ombi Maalum la Rais Samora Machel kwa
kuthamini mchango ambao Nguli huyu alitoa kwa Nchi hiyo, japo
ikidaiwa kuwa kulikuwa na Makubaliano Maalum ya Kuhakikisha
Kanali Ali Mahfoudh hakanyagi tena Ardhi ya Tanzania.
Nchini Msumbiji Kanali Mahfoudh alikuwa Mshauri Mkuu wa Mambo
ya Kijeshi wa Rais Samora Machel na kwa kiasi kikubwa ndiye
anayetajwa kuisaidia Msumbiji kimbinu kupambana na Waasi wa
Renamo waliokuwa wakipewa Msaada wa Mbinu za Kijeshi, Silaha na
Fedha kwa Dhahiri na Makaburu wa Afrika ya Kusini pamoja na
Mataifa mengi makubwa ya Magharibi. Kwa kutambua Ushujaa na
Ujuzi wa Mbinu mbalimbali za Vita wa Kanali Ali Mahfoudh, Makaburu
walijaribu Mara tatu kutaka kumuua lakini Mara zote walishindwa
katika Majaribio yao hayo.
Kanali Ali Mahfoudh aliendelea kuishi Msumbiji hata mara baada ya
kustaafu kazi yake ya Ushauri wa Mambo ya Kijeshi kwa Serikali ya
Msumbiji, Baadaye alijiingiza kwenye Biashara, mara nyingi alikuwa
Akipatikana katika Klabu ya Watanznia iliyokuwa katika Jengo la
Ubalozi wa Tanzania Nchini Msumbiji ambalo tulipewa zawadi na
Serikali ya Msumbiji kwa msaada wetu kwao. Hata alipofariki Dunia
Nchini humo bado Kanali Ali Mahfoudh hakurudishwa Tanzania na
alizikwa Katika Makaburi ya Mashujaa (Heroes Cemetary) Jijini
Maputo huko huko Msumbiji.
Aliyekuwa Mke wa Kanali Ali Mahfoudh, Mama Naila Majid Jiddawi
aliendelea kubaki Tanzania ambapo baadaye naye alikuja kuwa Mtu
Maarufu na Nguli mno katika Siasa za Tanzania hasa kwa Upande wa
Zanzibar, ambapo alipambana sana katika siasa kupitia Vyama vya
CUF na NCCR Mageuzi (aliwahi kuwa Mgombea Mwenza wa Urais wa
Chama hicho) lakini naye kama Mumewe alikutana na Rungu la
Serikali kwa kufanyiwa Hujuma za wazi katika Biashara zake kiasi cha
kufikia Mpaka kuchomewa Hoteli anayoimiliki.
Wakati Rais Amani Abedi Amani Karume akiwa Madarakani
alishutumiwa sana kwa kutoa Msamaha kwa Wafungwa ambao
walifungwa kwa kosa la kuchoma hoteli ya Mama Naila Majid Jidawwi,
ikionekana ni kama vile Serikali ilikuwa inatoa Msamaha kwa watu
ambao ilidhanika kwamba iliwatuma wachome Hoteli ya Mama huyu.
Mama Naila Majid Jiddawi bado yuko hai huko Zanzibar, akifarijika
kwa Mtoto wake mwema aliyefanikiwa kuzaa katika ndoa yake na
Kanali Ali Mahafoudh, Mtoto huyo anaitwa Mahfoudh au kwa jina
Maarufu "CHE" Mahfoudh kwa kuwa kama baba yake naye kafanana
sana na Mwanamapinduzi Enersto "Che" Guvara wa Amerika ya
Kusini.
Pichani ni Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akimvisha medali ya Ushujaa wa
Vita vya Ukombozi wa Nchi za Afrika Mwanajeshi Mkakamavu,
Komandoo aliyeogopwa na Maadui wa Tanzania na Afrika na
Mpiganaji Shupavu aliyejitolea kupigania Ukombozi, Kanali Ali
mahfoudh, Picha hii ilipigwa mwaka 1969.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog