Hatimaye Tumechagua Mabadiliko,
Salamu kwa wanafamilia wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF).
Salamu kwa wapenda michezo wa ndani na nje ya nchi yetu
Tanzania.
Naanza kwa kumshukuru Mungu kwa hekima, busara, akili, vipaji
na uwezo aliotujaalia kutuwezesha kutenda yote haya kwa amani na utulivu.
Shukrani za dhati zimwendee Bw. Leodegar Tenga, rais wa TFF
2005 - 2013 anayekabidhi madaraka kwa rais mpya wa TFF. Yeye na timu yake kwa
hakika wanastahili pongezi kwa mengi mazuri waliyofanya.
Shukrani kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi 2013 kwa
kunikubali, mimi Jamal E. Malinzi niwe Rais wa TFF kwa kipindi kijacho cha
miaka minne.
Kweli dunia imekuwa kijiji, kwani kipindi cha masaa 72 baada
ya kuzindua ilani yangu ya uchaguzi, nimepokea salamu, maoni na mapendekezo
toka ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Burundi, Ivory Coast, Denmark
na NewZealand.
Kupitia www.jamalmalinzi.com, twitter
@jamalmalinzi, Jamii Forum, Facebook na mitandao mingine, naomba tuendelee
kuwasiliana, kutoa maoni, kukosoa na kuchangia mijadala yenye tija na ufanisi
ili Tanzania yote ipate neema ya mpira wa miguu.
Safari ni ndefu na wasafiri ni wengi kwenye vyombo vichache
vya usafiri. Kwa wale ambao tayari wana ramani ya safari yetu, sote bila kujali
tofauti zetu hasa wakati wa kuwania uongozi, tutoe mchango wake ili Tanzania isonge mbele katika ulimwengu
wa soka.
Naam, kuna msemo wa Kiswahili unaosema 'kukata tamaa ukingali
unaishi ni dhambi'. Naomba msemo huu na utuongoze kila tunapojikwaa tunanyuke na
kuendelea na safari hadi tufike tulipopakusudia.
Historia imeshaanza kuandikwa, mwaka 2013 ni Tumechagua
Malinzi, Tumechagua Mabadiliko na sasa tunasonga mbele.
Jamal E. Malinzi
Oktoba 27, 2013
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog