Mtoto aliyefariki |
Mtoto Matrida Michael mwenye umri wa miaka 9, mkazi wa
Mtoni kwa Azizi Ally, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, amefariki
dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Oktoba 23, mwaka huu kufuatia
majeraha ya moto aliyoyapata.
Marehemu Matrida na watoto wenzake wawili, Tatu Mapunda
(9) na Flora Mapunda (7), waliungua moto Oktoba 16, mwaka huu saa tano usiku
wakiwa wamelala baada ya chumba chao kulipuliwa kwa petroli na mtu anayedaiwa
kwa ni Brighton Mnamwa.
Inadaiwa kwamba chanzo cha Mnamwa kuamua kulipua watoto
hao ni ugomvi baina yake na mkewe Janeth Lwena, waliyekuwa katika mzozo wa
kumgombea mtoto wao wa miaka mitatu aitwaye Tulizo.
Watoto ambao wako hoi |
Mama mdogo wa marehemu Mary Ivo ambaye alikuwepo msibani
hapo, alisema kwamba dada yake yupo Muhimbili anawauguza majeruhi wawili
waliobakia na kwamba wakati wa ugomvi wao, mke alimzidia nguvu mumewe.
Aidha aliendelea kueleza kwamba baada ya mke kumzidi
nguvu, mume alizusha ugomvi mkubwa huku akitishia kumuua kwa panga, hata hivyo
mke alimdhibiti.
‘Baadaye mume huyo inadaiwa kwa aliondoka hapo nyumbani
na haikujulikana alikoenda, ndipo mke alienda chumba cha jirani na kumuomba
Matrida abakie na watoto pale chumbani akatoe taarifa polisi lakini mtoto
aliyekua akigombewa alienda naye kituoni,’ alisema mama mdogo.
Habari zinasema kwamba yule mume alienda kituo cha mafuta
kununua petroli ili aweze kuwatekezeza wote, lakini hakujua kama mkewe pamoja
na mtoto aliyekua akigombewa hawakuwepo.
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba baada ya mume huyo kurudi,
alimimina mafuta hayo katika chumba hicho kisha kukilipua wakati watoto hao
watatu wakiwa katika usingizi na wananchi walipojitokeza walikuta chumba
kikiteketea huku sauti ya watoto ikisikika wakiomba msaada.
Wananchi waliokuwepo kwenye eneo la tukio walisema kwamba
walipatwa na uchungu hivyo walijitosa kuuzima moto ule na kuwaokoa watoto hao
watatu huku wakiwa wameungua vibaya, waliwakimbiza Hospitali ya Temeke na
kutokana na hali yao kuwa mbaya walipelekwa Muhimbili ambapo Matrida alifariki
dunia.
Naye Michael Melkiori Kess, baba wa marehemu alisema
kwamba amesikitishwa na kitendo hicho na amedai ni cha kinyama hivyo ameiomba
dola kumsaka mtu huyo hatari kwani huko aliko kwa sasa bado anaweza kusababisha
majanga megine.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mtoni Sabasaba, Mwita
Mang’ana alisema kwa kitendo hicho ni cha kinyama kwani amesababisha kujeruhi
watoto wasiokua na hatia na amewataka wananchi kushirikiana na jeshi la polisi
kuhakikisha kuwa mtuhumiwa anapatikana .
Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba msako wa kumtafuta
mtuhumiwa unaendelea sambamba na uchunguzi wa tukio.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog