Mashabiki wa timu ya Yanga wakiishangilia timu yao siku za hivi karibuni katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam |
Wanachama na matajiri wa Yanga wameingia mstari wa mbele kuhakikisha timu hiyo inashinda mechi zote tano zilizosalia na kufuta jeuri ya Azam ambao kasi yao imeanza kutishia amani ya mtaa wa Jangwani walio kileleni.
Azam inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 46 na Yanga ikishikilia usukani na pointi zake 49 jambo ambalo limezua mshtuko.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba uongozi wa Yanga utatoa Sh.70,000 kwa kila mchezaji kwa kila mechi wanayoshinda. Kwa mechi tano zilizosalia wakishinda timu nzima italamba Sh.10 milioni kwa wachezaji 29.
Lakini matajiri chini ya hamasa ya Abdallah Binkleb na Seif Ahmed Seif Magari wameingiza mkono wao ambapo wameahidi Sh.5 milioni kwa kila mechi Yanga watakayoshinda ingawa kuna wengine wameahidi kuongeza kuanzia mechi ijayo.
Habari za ndani zinasema kuanzia mechi ijayo watakuwa wakipewa dau la Sh.10 milioni na wataanza kununua idadi ya mabao yanayofungwa ili kuwajengea wachezaji morali ya kupachika mabao mengi lengo likiwa ni kurudisha kipigo cha mabao 5-0 watakapokutana na Simba Mei 18.
Simba ndio mabingwa watetezi ambao wakishinda mechi zao tano zilizobaki ikiwemo dhidi ya Azam kesho Jumapili na Yanga Mei 18 itatimiza pointi 50 ambazo Yanga ikishinda leo Jumamosi inazipita hivyo kubakiwa na kazi moja tu ya kuidhibiti Azam.
Yanga ina pointi 49 ikishinda mechi tatu ambazo ni dhidi ya Oljoro, Mgambo na JKT Ruvu pamoja na sare dhidi ya Coastal Union itafikisha pointi 59 ambazo Azam haiwezi kuzifikia kwani ikishinda mechi zake zote itakomea pointi 58.
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts ambaye atawakosa nyota wake tegemeo kama Mbuyu Twite mwenye kadi tatu za njano, Jerry Tegete na Stephano Mwasyika ambao hawako fiti kwa asilimia 100 tayari ameshawaambia mabeki, viungo na washambuliaji kuwa ni jukumu lao kufunga mabao katika mechi hiyo na nyingine.
Na katika kuhakikisha anafanikiwa, Brandts aliwahamishia mafichoni nyota wake katika Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola kutoka Bora, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Yanga inakutana na Oljoro ambayo haipo katika hofu kubwa ya kushuka daraja ikiwa nafasi ya nane na pointi 28 na katika kujiwekea mazingira mazuri ilifika mapema tangu wiki iliyopita na kujificha Ruvu, Pwani.
Brandts alisema: Lengo ni pointi tatu tu. Kutokana na hilo nimewasuka wachezaji wangu wote katika kuhakikisha kila mmoja anafunga na kuzuia.
SOURSE: MWANASPOTI
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog