Wewe Makengeza,
Wewe kwa kweli unakuwa kipofu. Katika kulilia mavi ya kale unashindwa kuona mazuri yaliyopo. Si binadamu tu wanaobadilika kulingana na wakati, hata nchi inapaswa kufanya hivyo, bila unafiki, bila kificho.
Hebu tuchukue mfano wa katiba yetu iliyopitwa na
wakati. Yaani bado inatangaza kwamba tunafuata siasa ya Ujamaa na
Kujitegemea. Nani anadanganyika na uongo huo? Labda vijana ambao
wanafikiri Azimio la Arusha linahusu ujenzi wa barabara mjini na kwamba
ujamaa maana yake ni kusaidiana kukwapua yanayokwapulika.
Ujamaa ni hujumaaa! Bila kusahau kwamba
kujitegemea ni kutafuta wafadhili na mafedhuli wengi iwezekanavyo kutoka
nje. Haisaidii!
Kwa hiyo, si vizuri kuendelea kuwa na maneno tata
ndani ya katiba. Lazima kuwa na dira ya kutuongoza na hata kututongoza
tukubali kujitoa na kujitosa katika maendeleo ya nchi yetu changa ya
macho.
Ndiyo. Hebu angalia uchaguzi unavyoendelea kwa
sasa kupata wajumbe wa mabaraza ya kata. Ni wajumbe tu wa mabaraza ya
kata wenye lengo la kutoa mawazo kuhusu katiba yetu iweje. Lakini
badala ya watu kujinadi kwamba wana mawazo haya au yale kuhusu katiba,
wanatwangana ngumi kwa misingi ya makundi ndani ya chama hiki au kile.
Waliofanikiwa kuchaguliwa kwenye ngazi ya mtaa
wanadaiwa rushwa ili wapite kwenye ngazi ya kata na kadhalika. Bila
kuhonga, hata nafasi ya kuchangia Katiba Mpya huwezi kupata.
Kwa hiyo, waliofikiria kwamba Katiba ni suala la
kuwatafuta watu wenye mawazo chanya ili kuwa na Katiba ambayo itatulinda
sisi wa kizazi hiki pamoja na vizazi vijavyo vyote wanajidanganya. Au
tuseme kwamba wanaogombea nafasi hizo za kuingia kwenye mabaraza ya
kata wameelewa kitu cha msingi sana kuliko wasomi wote wanaobwatia
nadharia. Mchakato wa katiba ndiyo dira ya Katiba.
Bila rushwa, nchi yetu haiwezi kuendelea. Naamini
kwamba wananchi wote wameelewa hivyo ndiyo maana wanaendelea kubariki
mtindo huu wa kupata wajumbe na mambo mengine yote ndani ya jamii yao.
Msingi huo ni wazi pia. Nikilinyamazia jambo fulani maana yake
nimelikubali.
Kwa hiyo napenda kutangaza kwamba katika misingi
ya taifa inayoorodheshwa ndani ya Katiba, itangazwe rasmi kwamba
‘Tanzania ni nchi ya rushwa na kujitafutia’. Kwa njia hiyo, tunakuwa
mfano bora wa uwazi na ukweli na pia tunaweza kuwashughulikia watu
wahafidhina kama wewe mnaotaka kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Hebu tutafakari kidogo. Juzi, nilipanda daladala
kwenda vijijini. Wakati tunaanza safari jamaa mmoja alikuwa anamcheka
mwimbaji maarufu eti analalamika kwamba wimbo wake hauchezwi na kituo
cha redio kwa kuwa hajatoa hela.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog