Facebook Comments Box

Tuesday, February 5, 2013

UTOTO WA WABUNGE WETU UNACHANGIA UMASIKINI WETU

Picture
Na. Emmanuel J. Shilatu
Mara baada ya kufanikiwa kuziondoa tawala mbovu, nyonyaji na za kidhalimu za Wakoloni hapa nchini, aliyekuwa akiongeza harakati hizo ambaye pia ni Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema ya kuwa “tumefanikiwa kuwaondoa wakoloni na hivyo tupo huru na Uhuru ni kazi”. Hapa Mwalimu Nyerere alikuwa na maana ya kuwa ili tuweze kupiga hatua kimaendeleo ni lazima tuutumie huu uhuru wetu vilivyo kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa yote ili kuleta maboresho katika Nyanja zote za kimaisha yaani uchumi, kijamii na kisiasa.
Na ndio maana yeye kama kiongozi alianza kuonyesha mfano wa dhahiri kwa kuanzisha mapambano kwa vitendo dhidi ya maadui zetu watatu ambao ni ujinga, maradhi, na umaskini. Sehemu ya mafanikio yake ni kwa kupitia kuanzisha maazimio, mashirika, kauli mbiu na sera mbalimbali. Hayo yoote (yaani tangu kusaka uhuru wa Tanganyika) aliweza kufanikiwa kutokana na kufanya mambo kwa matendo zaidi kuliko maongezi (porojo) zisizoisha.
Pia Mwalimu Nyerere alikuwa na falsafa (dhana) ya kimaendeleo ambapo aliamini kuwa maendeleo sahihi hayawezi yakapatikana nje ya uwepo wa mambo manne ambayo ni“Watu”, “ardhi”, “siasa safi”na “uongozi bora”
Ndio “Watu”ni kiungo kimojawapo cha hakikisho la maendeleo chanya yeyote yale ndani ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla. Kama tutakuwa na miundombinu bora ni watu wamechangia uwepo wake; kama tutakuwa na mazao ya kutosha kwa ajili ya chakula, kiada na biashara ni watu ndio wamechangia hayo; Endapo kuna amani na utulivu nchini basi ujue watu wamechangia hayo; ama taifa likiwa na wasomi wa kutosha ni watu mbalimbali ndio wamechangia hilo.
Licha ya kwamba Taifa letu Tanzania lina watu zaidi ya Milioni 45 lakini hao watu wamekuwa ndio kikwazo kikubwa katika uletaji wa maendeleo ya kweli na ya dhahiri. Tatizo lililopo ni uibukaji wa umaskini mkubwa wa utegemezi na utajiri mkubwa wa porojo ndani ya jamii na kila Mwana jamii ni mwathirika wa hili si Kijana wala Mzee awe ni Mwanamke au Mwanaume.
Utakuta vijana wengi kutwa wanashinda kwenye kucheza “pool table” na kukaa vijiweni tu; Wazee ama akina Baba nao kutwa wanacheza “bao” ama “draft” tu; na akina Mama nao kila kukicha wapo vibarazani wakisutana na kupashana umbea tu. Hayo ndio maisha ya kila siku ya baadhi ya wanajamii ya kutokupenda kufanya kazi kwa bidii.
Jamii inachojua ni utegemezi pekee. Kivipi? ... Kwa jinsi tuanavyoishi utadhani tunawangojea baadhi ya watu kutoka nje ili waje watuletee maendeleo yaani imefika kipindi kwa mtu hata kutandika kitanda chake mwenyewe anacholalia imekuwa ni kazi kuubwa kwake. Pia suala la maendeleo ya nchi yetu wenyewe tumewaachia viongozi pekee huku tukijiengua katika kapu la dhana ya neno“Serikali” wakati kiuhalisia na kikatiba pia ni kwamba Serikali inaundwa na viongozi pamoja na Wananchi.
Hii yote inatokana na jamii kuziasi mitazamo miongozo na falsafa za Mwalimu Nyerere (mathalani ile ya “Uhuru ni kazi”) hali inayosababisha kiwango cha idadi ya watu maskini kuzidi kukua nchini licha ya kujaariwa rasilimali na mali za asili kwa kuyachakachua maendeleo yetu wenyewe. Kisa? Porojo kutawala maisha yetu.
Hali hii tuliyonayo ya kutaka kuongea ongea ovyo huku parojo zikituendesha katika masuala ya kimsingi ya maisha yetu, tunataka tuwaambukize hata na viongozi wetu. Imefika kipindi kigezo ama kipimo cha uwezo wa Kiongozi unapimwa na utokeaji wa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari ama uongeaji, uropokaji na ubwatukaji wa mara kwa mara kwenye jumba letu tukufu la kutunga sheria na wala si utendaji wake kazi na uletaji wa maendeleo katika jamii yaani ni usanii, usanii mtupu. Hii ni hatari sana.
Hivi tunachotaka kutoka kwa Kiongozi ni mazungumzo pekee ama matendo yake ya kimaendeleo? Ama uwezo wa kiongozi bora upo kwenye mazungumzo tu ama utakelezaji wa kimaemdeleo? Hivi uhodari wa mbunge wangu unatoka na amezungumza mara ngapi Bungeni ama amenipunguziaje zigo langu la matatizo ya kimsingi? Bila shaka majibu ni hapana ila ajabu ya firauni ni kuwa kwa miaka ya hivi karibuni kumeibuka dhana mfu ya kupima uwezo wa Kiongozi si kwa uletaji wa maendeleo bali ugwiji wake wa kuzungumza Bungeni kwa kuchangia hoja kuulizwa maswali ya msingi na kadhalika.
Mtazamo huu unaonyesha kuwa kiongozi bora anapimwa kwa uwezo wake wa kuongea Bungeni na si utetaji wa maendeleo; Pili, wanawafundisha viongozi wetu tabia mbaya ya kuwa wawe ni wazungumzaji tu na si watendaji; Tatu, inavyoonyesha hawaijali thamani ya maisha ya Mtanzania bali ya Yule anayeiwasha vipaza sauti mara kwa mara pale mjengoni.
Katika kipindi fulani cha nyuma tafiti mojawapo nchini walitoa matokeo yao ya utafiti ambapo waliueleza Umma kuwa Mh. Edward Ngoyai Lowassa ndiye anayeongoza pale Bungeni kwa kutokuongea pale Bungeni tangu 2005. Jamani hivi ni kweli?
Lowassa wanayemzungumzia ni yule yule ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika serikali hii ya awamu ya nne kwa takribani miaka miwili. Kikatiba, Waziri Mkuu ndiye Kiongozi wa shughuli nzima za Serikali Bungeni. Hivi inawezekana vipi kwa kiongozi mkubwa kama huyo (Waziri Mkuu) kutokuongea lolote lile kwenye mikutano na vikao vya Bunge? Amu hoja au maswali mazito yahusuyo serikali yakiwashinda Mawaziri, M/Waziri au Mwanasheria Mkuu huwa yanatolewa ufafanuzi na nani?
Suala la kuongea mno Bungeni sio hoja ya kuwaletea neema ya kimaendeleo bali Wapiga kura wanahitaji matendo na wala sio maneno matupu . Wapo Wabunge ambao sio waongeaji lakini kwenye majimbo yao wameleta neema ya ajabu kupitia uongozi wao.
Mathalani Mh. Nimrod Mkono ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini katika kipindi cha ubunge wake amewaletea neema kubwa Wapiga kura wake. Amewajengea shule ya sekondari kubwa na ya kisasa na kuikabidhi kwa Serikali, amejenga maabara ya kisasa iliyojitosheleza kila kitu mihimu, amejenga nyumba za walimu. Pia amewanunulia gari la kubebea wagonjwa kwa wana wa jimbo la Musoma vijijini na kadhalika. Pamoja na kutokuongea kwake Bungeni lakini Wapiga kura wake hauwaelezi kitu kwani ni Mkono, Mkono tu. Hivyo kutokuongea Bungeni sio tatizo.
Pia mwangalie Mohamed Dewji “MO” (Mbunge wa Singida Mjini) ambaye yeye si muongeaji lakini nyakati zote ameonyesha nia ya dhati ya kuwapenda na kuwathamini wapiga kura wake. “MO” amejitolea kwalipia ada ya vyuoni wale wote wa jimbo lake waliobahatika kupata elimu ya juu (chuoni), kwa wale pia ambao wana vigezo amewaahidi kuwapa ajira za kudumu kupitia makampuni yake, hata hivyo pia amekamilisha miradi mingi ya maendeleo ambayo ilikuwa inasuasua.
Hao ni baadhi tu ya wale ambao sio waongeaji lakini ni watendaji haswaa ambao Wapiga kura wao wanajivunia nao. Lakini wapo wale ambao ni mafundi wa kuongea hadi kuwa wabwatukaji pale Bungeni lakini uongeaji wao huo haujawasaidia lolote lile Wapiga kura wao.
Licha ya ufundi wao wa kuongea lakini wameshindwa kuwatatulia kero za maji, umeme, hospitali, shule ama masoko kwa ajili ya bidhaa zao; wengine waliahidi kuwajengea majosho ya kuogesha ng’ombe wao, kuwajengea machinjio ya kisasa na hata wengine wameshindwa kuikamilisha mradi wa ujenzi wa kawaida cha kusindika Tangawizi tu. Wengine ndio wameua kabisa sekta ya kilimo katika majimbo yao hali ambayo inawafanya Wananchi waishi maisha magumu na yasiyoelezeka.
Nimelazimika kuyaeleza haya kutokana na mitazamo isiyo na tija kwa jamii inayozaa matukio ya uletaji ushabiki wa kisiasa kwenye chombo muhimu cha kutunga sharia za nchi ambapo Wabunge wanawatelekeza wapiga kura wao kwa kutokupigania maslahi yao na badala yake wanaendekeza ushabiki wa kichama ndani ya Bunge.
Ni aibu isiyoelezeka kumuona Mbunge anawasha kipaza sauti na kuanza kutoa maneno ya kebehi kwa kufuata utashi wa kisiasa. Huko ni kuwapotezea muda wapiga kura wao.
Dhana ya hiyo ya kushabikia waongeaji ndani ya Bunge imewafanya Wabunge wengi wasiwe watiifu mbele ya kiti cha Spika kwa kujiamulia kuwasha vipasa sauti na kila mmoja kuanza kuzungumza na hatimaye kuligeuza Bunge kuwa gulio na si tena mhimili wa dola.
Utoto wa Wabunge haustahili kuvumiliwa hata kidogo kwa kuwa wao ni Watu wazima na watu wamewaamini kiasi cha kuwapatia madaraka.
Endapo Mbunge atakuwa anatumia muda mwingi kwa ajili ya kuzomea zomea ndani ya Bunge ama kutoa lugha za kebehi na dharau ndani, atapata wapi wasaa wa kuwasemea matatizo ya Wapiga kura wao? Je, sisi Wananchi wa kawaida tunanufaikaje na matokeo hayo ya kitoto yanayofanywa na Wabunge wetu tuliowachagua?
Kimsingi, umaarufu wa Mbunge hauji kwa kuzunumza kwa jazba wala kutoa lugha za maudhi awapo Bungeni, umaarufu wa Mbunge utatokana na kutekeleza ahadi ahadi ya kukidhi matarajio kwa waliomchagua.
Ni vyema Wabunge wakatambua ya kwamba fursa na uhuru waliopewa na watu waliowaamini una mipaka na una mwisho wake, ni vyema wakautumia huo uhuru kabla wakati haujawapita kwani wakati ni ukuta, wakishindana nao wataumia.
Ndugu zangu, kuna haja kubwa ya kuwa makini sana wakati wa upigaji kura ili kuepukana na wabunge wasijali maslahi ya Wananchi bali maslahi yao na ya chama chao, kuwaepuka viongozi watovu wa nidhamu dhidi ya kanuni na utaratibu husika. Bila ya hivyo, tutazidi kuwa maskini!


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU