Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts amekuwa akimtumia Bahanuzi kama mchezaji wa akiba tangu aliporejea uwanjani.
Bahanuzi aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro alikuwa anasumbuliwa na maamivu ya nyama za paja aliyoyapata akiwa na timu ya Taifa Stars mwaka jana.
Katika mechi mbili za ligi ambazo nyota huyo ametokea benchi zikiwa zimebaki dakika 15 kabla ya mchezo kumalizika amefanikiwa kutoa pasi ya bao kila mechi.
Mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Bahanuzi ndiye aliyetoa pasi kwa Hamis Kiiza kufunga bao la kusawazisha. Timu zote mbili zilifungana bao 1-1.
Pia, mchezo wa African Lyon uliochezwa Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Bahanuzi akitokea benchi alitoa pasi kwa Nizar Khalfan aliyefunga bao la tatu wakati Yanga ikishinda 4-0.
Mara zote anapoingia mshambuliaji huyo mwenye nguvu za miguu na uwezo wakufyatua mashuti makali, amekuwa akiichangamsha safu ya ushambuliaji ya Yanga tofauti alivyokuwa benchi.
"Kwa sasa nafikiri nimerejea kwenye fomu. Nafikiri kocha tu ndiye anashindwa kuniamini." alisema Bahanuzi mwenye bao moja kwenye ligi alilofunga kwa penalti dhidi ya Simba Oktoba 3, mwaka jana.
"Nilikuwa nasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja. Kwa sasa nafikiri hali yangu imeimarika kama awali." alisisitiza.
Kwa upande wake Ernie Brandts alisema; "Siwezi kumchezesha dakika 90. Nadhani Bahanuzi ametoka kwenye majeruhi. Kwa hiyo nimekuwa nikimpa dakika 15 za mwisho kutizama maendeleo yake.
"Nafikiri ameimarika kwa mechi mechi ambazo nimemuona akicheza."
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog