LIGI KUU TANZANIA BARA 2012/2013
Michuano
ya Ligi Kuu kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kwa msimu wa 2012/2013
itaanza Septemba 15 mwaka huu kwa timu zote 14 kujitupa kwenye viwanja
tofauti.
Mechi za ufunguzi zitakuwa kati ya Simba vs African Lyon (Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam), Polisi Morogoro vs Mtibwa Sugar (Jamhuri,
Morogoro), Tanzania Prisons vs Yanga (Sokoine, Mbeya), Mgambo JKT vs
Coastal Union (Mkwakwani, Tanga), JKT Ruvu vs Ruvu Shooting (Azam
Complex, Dar es Salaam), Kagera Sugar vs Azam (Kaitaba, Bukoba) na Toto
Africans vs Oljoro JKT (Kirumba, Mwanza).
Mzunguko wa kwanza
(first round) utamalizika Novemba 11 mwaka huu ambapo kwenye mzunguko
huo mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba itachezwa Oktoba 3 mwaka huu
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ligi hiyo itamalizika Mei
18 mwakani kwa mechi kati ya Toto Africans vs Ruvu Shooting (Kirumba),
Mgambo JKT vs African Lyon (Mkwakwani), JKT Ruvu vs Mtibwa Sugar (Azam
Complex), Tanzania Prisons vs Kagera Sugar (Sokoine), Simba vs Yanga
(Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Azam (Sheikh Amri Abeid Kaluta) na
Polisi Morogoro vs Coastal Union (Jamhuri).
Endapo Simba na Azam
hazitafanikiwa kuvuka hatua mojawapo ya michuano ya Ligi ya Mabingwa
Afrika na Kombe la Shirikisho, ratiba hiyo itafanyiwa marekebisho.
WACHEZAJI 17 WAPINGWA KWENYE USAJILI
Klabu
mbalimbali zimewasilisha pingamizi Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kupinga usajili wa wachezaji 17 walioombewa usajili
katika timu za Ligi Kuu.
Toto Africans ya Mwanza imewawekea
pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton aliyeombewa usajili Kagera Sugar,
na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina
mikataba na wachezaji hao.
Pia Flamingo ya Arusha inapinga
usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na
Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado
hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles
Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.
Super
Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake
wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert
Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union)
kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho
hazikufuatwa.
Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal
Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo
unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass
Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga
kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile
bado hajafikisha umri wa miaka 23.
Azam inapinga usajili wa
Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye
unaomalizika Juni 11 mwakani. Nayo Simba inapinga Kelvin Yondani
kusajiliwa Yanga kwa maelezo kuwa ina mkataba naye uliosainiwa Desemba
23 mwaka jana.
Vilevile Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo
usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga kwa
maelezo alisaini mkataba na klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele yao,
viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na APR ambapo
alilipwa dola 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na
nauli yake ya kujiunga na klabu hiyo.
Nayo Yanga inapinga Simba
kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino
Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania
walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga
Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea
Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba
ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa
kwa maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja
wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa
Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel
Akuffor.
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF
chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana Jumapili
(Septemba 2 mwaka huu) kupitia pingamizi hizo pamoja na usajili wa
wachezaji kwa ujumla kwa 2012/2013.