Facebook Comments Box

Sunday, January 27, 2013

MADIWANI KIGAMBONI: HAIWEZEKANI KUTUONDOA TEMEKE BILA UTARATIBU WA KISHERIA

  Tangazo la Serikali kulichukua eneo lote la Kigamboni na kuliondoa chini ya mamlaka ya Manispaa ya Temeke, limezua tafrani baada ya madiwani kutaka kuitisha kikao maalum cha kupinga hatua hiyo na tayari wameanza kukusanya saini za madiwani wanaofikia akidi ili kiitishwe kikao walichokiita kuinusuru Temeke. Tayari nusu ya kura imepatikana.

Hivi karibuni Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alitangaza kulitwaa eneo la Kigamboni na kuongeza ukubwa wa eneo kwa kuchukua kata nyingine kwa ajili ya uanzishwaji wa jiji la kisasa la Kigamboni. Pia, alitangaza kuanzishwa kwa chombo cha Wakala wa Kuendeleza Mji wa Kigamboni (KDA) ambapo hatua hiyo inaiondoa kutoka Manispaa ya Temeke kiutawala.

Madiwani hasa kutoka Kigamboni wamesema kitendo cha Serikali kuwaondoa kibabe bila kuwashirikisha kimezidisha hofu kwa wananchi wa eneo hilo ambao tangu mradi huo uanze kuandaliwa, wamerudishwa nyuma kimaendeleo.
Tumeshtushwa sana na kauli ya waziri Profesa Tibaijuka, ni hatua ya kibabe iliyochukuliwa bila kutushirikisha sisi madiwani, haiwezekani kutuondoa manispaa ya Temeke bila kufuata utaratibu wa kisheria.
Alisema inashangaza pia kuwa Serikali imeongeza kata nyingine nne --Kisarawe 11, Kimbiji, Somangila na Pembamnazi -- na kuziingiza kwenye mradi bila kutoa taarifa kwa wananchi ili waweze kujadili na kutoa maoni yao. Kata zilizokuwa awali ni Kigamboni, Tungi, Kibada, Mjimwema na Vijibweni.
Tutalazimika kukutana haraka kuona jinsi gani tutaijibu serikali kwa maamuzi yake haya ya ukandamizaji, sisi ni wawakilishi wa wananchi kwa nini wanafanya mambo yao kwa usiri mkubwa na kisha kutupa taarifa kama vile huku hakuna mamlaka inayokubalika.
via gazeti la NIPASHE.



Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU