Facebook Comments Box

Thursday, September 26, 2013

BABU WA LOLIONDO - SAMUNGE AITABIRIA MAKUBWA TANZANIA


Mchungaji Ambilikile Mwasapile "Babu wa Loliondo"
 
 Mchungaji Ambilikile Mwaisapile wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) amesema Mungu ameendelea kujifunua kwake na kumuonyesha kuwa Tanzania itakuwa kioo cha Afrika na baadaye kioo cha dunia.

Ametoa kauli hiyo siku ya (Jumanne, Septemba 24, 2013) mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati msafara wa Waziri Mkuu uliposimama nyumbani kwake ili kumsalimia akiwa njiani kurejea mjini Arusha.

Mchungaji Mstaafu Mwaisapile maarufu kama 'Babu wa Samunge' alisema kuna mambo mengi ambayo yameandikwa kwenye Biblia lakini hayakutokea Israeli na sasa yatafanyika hapa Samunge. “Mungu ametupenda sana, yanakuja mambo makubwa na wala hayako mbali. Kama mimi ni mzee na nitayaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako mbali kutokea,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema katika mafunuo aliyopewa na Mungu ameonyeshwa kwamba watu wengi zaidi watafurika kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa hapo awali. Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa misaada iliyotoa wakati wa ‘kugawa kikombe’ ikiwemo mahema, maji na ulinzi.

Akitoa ombi maalum kwa niaba ya vijana mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Elias Kalumbwa alisema wanaomba kuchimbiwa bwawa ili waweze kujiajiri kupitia kilimo cha mbogamboga na matunda.

Bw. Kalumbwa ambaye amesomea masuala ya wanyamapori alisema eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wa msimu unaopita kijijini hapo. “Eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wetu, vijana tunaweza kujiajiri endapo tutapata bwawa ili tufanye kilimo cha umwagiliaji maji,” alisema huku akishangiliwa.

Naye Bibi Martha Sereri (70) alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanaomba jimbo la Ngorongoro ligawanywe kwa sababu ni kubwa sana kiasi kwamba inamuwia vigumu mbunge wao kufika maeneo yote. Aliomba pia wapatiwe walimu wa sayansi na hisabati kwa ajili ya shule 10 za sekondari zilizopo kwenye tarafa yao.



Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU