Facebook Comments Box

Thursday, May 9, 2013

NIMEAMUA NISEME: HOTUBA YA KAMBONA YA 1966 NI SULUHISHO KWA CCM YA SASA (SEHEMU YA KWANZA)

Na Abukhayrat Hassan ka`bange
Habari za mishughuliko na mihangaiko ndugu zangu watanzania. Nikiwa katika mihangaiko ya kutafuta nini cha kusoma ili kushibisha akili zangu nikafanikiwa kupekuwa na kukutana na kitabu ambacho kimeandikwa ikiwa ni hutuba ya Marehemu Oscar Kambona akilihutubia bunge la Julai 14 mwaka 1966 ikielezea uongozi na misingi ya Tanu.Kitabu hiki kimepewa jina la UONGOZI BORA. Nikajiuliza kwanza kwanini kimeitwa jina hilo. Kikawa kimenivuta kukisoma. Niliyoyasoma nikajiuliza Je, wana ccm wa sasa kitabu hiki hawakijui? Au hiki kitabu wao hawana? Inakuwa vipi kama mimi kapuku tu nisiye husika na siasa kwa namna hiyo ya hao wanao jiita wanasiasa ninacho katika marundo yangu hapa ambayo mimi mwenyewe nayaita kwa jina zuri SHAJALA. Mfumo wa hotuba ulikuwa hivi:
KAMWE TUSISAHAU TANU:
Hapa Marehemu Kambona alikuwa akiwakumbusha wabunge kuwa wasiisahau TANU kwakuwa ndio iliyo wasababisha wakawa hapo bungeni na ndio chama kinacholeta misingi ya amani na umoja kwatika nchi. Na ileweke kuwa wao kama wanatanu watiifu ndio sababu iliyowafanya wawe hapo.Mtu mmoja mmoja binafsi sio jambo kubwa lakini wote kwa pamoja chini ya uongozi wa TANU ni jambo kubwa zaidi.
Kwenye CCM ya sasa tunaona hamna uwote kumeingia umimi,usisi,ukanda na mbaya zaidi udini kila mtu anataka lake hili ni moja linalo bomoa chama.

TUSIWEKE UBINAFSI MBELE:
Marehemu Kambona alilisema hili na kulikemea akaeleza kuwa ikiwa wanachama wa TANU wataleta ubinafsi chama kitadhoofika na hatimae kufa aliwanasihi wanachama wasiingiliwe na moyo huo wa ubinafsi.Viongozi hawawezi kutekeleza kazi zao bila ushirikiano wa wananchi. Na hawezi kushirikiana bila kujua utaratibu wa uongozi wa chama
Hili silisemei nani asiyejua ubinafsi ulivyotawala chamani leo?
TANU NI CHAMA CHA WATU:
Marehemu Kambona alielezea dhahiri bila kuficha kuwa TANU ni chama cha watu na watu hao wanaanzia katika ngazi za kijiji. Kwahiyo kama chama kinataka kuimarika inatakiwa chama kiimarike kuanzia vijijini ambako ndiko wanakokaa watu wengi. Hapa alikemea vilevile ubabe na utemi wa viongozi wa vijijini.
Kwa sasa vijiji tunavitenga kabisa hebu angalia bajeti tu ya maji vijijini ambako ndiko kunakadiriwa kuwa na watu zaidi ya asilimia themanini wanapewa kidogo kuliko asilimia ishirini ya mijini. Chama kinajenga hapa au kinabomoa?

VIONGOZI TUSHIRIKIANE-TUSIKOMOANE:
Marehemu Kambona alielezea kwa makusudi kabisa kuwa sehemu yenye maendelea ni ili ambayo viongozi wake wameshikamana wao kwa wao na wanachi. Wakianza migogoro wataunda makundi ambayo mwisho wake ni mbaya kwa chama. Alitoa suluhisho la kiongozi mwenye matatizo alisema apelekwe kwenye Halmashauri ya chama akajadiliwe na arekebishwe. Kumkomoa kiongozi mwenzio ni kubomoa nchi na kukiharibu chama
Tukiangalie chama chetu leo makundi yamekuwa mengi. Kukomoana kumezidi, Kiongozi mwenzio akikosea sehemu maalumu kwako kumsemea ni kwenye mitandao ya kijamii au magazeti

TUWAPENDE WANYONGE:
Hapa marehemu alijiaminisha kuwa viongozi wote wa TANU lao ni moja kuhakikisha hali ya mnyonge inainuliwa.Na akiasa viongozi washikamane katika kada mbalimbali kulifanikisha hilo. Alionya pia viongozi wanaotumia kadi za TANU kama hirizi zipo kwa ajili ya kutishia watu. Ukija anakuonesha kadi ya chama halafu anairudisha mfukoni wakati matendo yake ni kinyume na chama.
Tukiangalia chama sasa Je, viongozi wote wana dhamira ya kuinua hali za wanyonge? Vipi hawa wanaotumia vyeo vya vyama na kadi za chama kama hirizi. Kuna ofisi unakuta mtu kaweka picha kapiga na rais ukutani ili kuwatisha watu.

Itaendelea.......

Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU