TAARIFA YA UCHUGUZI JUU YA KUTEKWA NA KUUMIZWA KWA ABSALOM KIBANDA 
IMEWASILISHWA NYUMBANI HOTEL - TANGA MEI 30, 2013UTANGULIZI:
Usiku
 wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013, Mhariri Mtendaji wa New 
Habari (2006) Ltd, ambaye pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania 
(TEF), Absalom Kibanda alivamiwa na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango
 la kuingilia nyumbani kwake Mbezi Juu, Dar es Salaam.
Tukio hilo
 liliishtua na kutikisa taifa kwa kiwango kikubwa si tu katika tasnia ya
 habari nchini, bali pia jamii kwa ujumla hasa baada ya aina ya utekaji,
 utesaji na usiri uliotumika katika kufanikisha uhalifu huu kufanana kwa
 karibu na tukio lilomkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madkatari Tanzania, 
Dk. Stephen Ulimboka lililotokea karibu miezi tisa kabla ya tukio la 
Kibanda yaani, usiku wa Juni 26, 2012.Ukiacha matukio hayo, miezi sita 
kabla ya Kibanda kutekwa na kuteswa Mwandishi Daudi Mwangosi, aliuawa 
akiwa mikononi mwa vyombo vya dola Septemba 2, 2012 huko Nyololo, Iringa
 akiwa kazini.Tukio la Kibanda limekuwa na sura ya mwendelezo wa mauaji 
au utesaji wa wanahabari, hasa ikitiliwa maanani kuwa Mwandishi Issa 
Ngumba (45) wa Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia kazi zake katika Wilaya
 ya Kakonko, Kigoma, Januari mwaka huu, alipigwa risasi na kuuawa katika
 mazingira ya kutatanisha. Kama hiyo haitoshi, tukio la kutekwa na 
kudhuriwa kwa Kibanda limetokea mwezi mmoja tu baada ya Mwandishi wa 
Gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu kupigwa risasi na polisi akiwa 
nyumbani kwake Dar es Salaam kwa maelezo kuwa kimakosa polisi walidhani 
Matutu ni jambazi.
Mazingira ya kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda 
yalitia wasiwasi kuwa upo uwezekano, na dalili zilionyesha kwamba 
waliofanya kitendo hicho cha kinyama hawakuwa wezi wala majambazi 
kutokana na ukweli kwamba licha ya kuwa na fedha zipatazo shilingi 
milioni tatu taslimu ndani ya gari, laptop, simu tatu za gharama (
ipad, iphone na Blackberry), watekaji hawa hawakuchukua chochote baada ya kukamilisha uhalifu wao.
Kibanda
 aliumizwa kwa kiwango kikubwa. Alitobolewa jicho la kushoto, akaumizwa 
vibaya kichwani kiasi cha kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya mifupa ya 
kichwa. Aling’olewa meno mawili na kucha mbili, tena bila gazi. Watekaji
 hawa, katika unyama wa ajabu kabisa, walimkata pingiri ya kidole cha 
pete chini ya kucha na kuondokana nayo.Hali hiyo iliibua maswali mengi, 
watu wengi wakajiuliza na kutafuta sababu za kutekwa na kuumizwa kwa 
Kibanda kiasi hiki. Kutokana na kuwapo kwa maelezo mengi 
yanayotofautiana kuhusu tukio hilo, ikabidi Jukwaa la Wahariri Tanzania 
lifanye uamuzi.Katika kikao cha Machi 8, 2013 Jukwaa la Wahariri 
Tanzania liliunda TIMU ya watu watano na kuipa hadidu rejea za kufanya 
uchunguzi wa kihabari juu ya shambulio hilo kubaini limetokana na 
nini.Timu hiyo iliundwa kufuatia uamuzi wa Jukwaa la Wahariri kufanya 
uchunguzi huo na baada ya kukubalika kwa ombi la ruzuku ya kufanya 
uchunguzi huo wa kihabari kutoka Mfuko wa Vyombo Vya Habari Tanzania 
(TMF). Ruzuku ya TMF ililenga kiujumla kutumia tukio la Kibanda kuwa 
chanzo cha kutengeneza mazingira salama zaidi kwa waandishi na wahariri 
na kwamba kiwango cha matukio ya kuteswa, kupigwa na kuuawa kwa 
waandishi yanapungua kila mwaka. Timu hii imefanya kazi usiku na mchana 
kwa kwa zaidi ya mwezi. Timu imezungumza na wadau 26. Kati ya hawa yumo 
Kibanda mwenyewe, mke wake, ndugu zake, wasaidizi wake, waajiri wake wa 
zamani na wa sasa, viongozi wa kisiasa na vyombo vya dola kutafuta 
ukweli wa jambo hili. Pia tumesoma matamko na habari zilizochapishwa 
kwenye mitandao ya kijamii na magazeti ya kati ya Machi 5, 2012 na 
Aprili 5, 2012 kwa nia ya kufanya ulinganishi wa taarifa tulizozipata 
kutokana na uchunguzi na habari zilizochapishwa baada ya kutekwa 
kwake.Vyombo vya dola akiwamo Waziri mwenye dhamana walikataa kuhojiwa 
wakisema kuna tume ya serikali inayofanya kazi hiyo na kwamba kuhojiwa 
kungeonyesha kutokuwa na imani na tume hiyo.Leo tunawasilisha muhtasari 
wa ripoti hii. Ripoti kubwa pamoja na viambatanisho vyake, itachapishwa 
na kuwekwa katika kitabu kimoja. Utaratibu mwingine wa kuchapisha habari
 ambazo hazijachapishwa kuhusiana na tukio hili (untold stories) pia 
utaandaliwa kwa ushirikiano na Jukwaa la Wahariri kwa nia ya kuieleza 
jamii maajabu juu ya kadhia hii.Tulipewa Hadidu Rejea ziafuatazo:
HADIDU
 REJEA:1. Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la 
kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama 
kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya 
mashambulizi dhidi yake.2. Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa 
kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 
2013.3. Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari 
(2006), Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake 
kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.4. 
Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za 
kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.5. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi 
kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile 
kitakachobainika
YALIYOJIRI KATIKA UCHUNGUZI:1.0. Kuchunguza 
mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya 
kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote 
vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake.Timu ya 
uchunguzi ilitumia muda mwingi katika eneo hili, kubaini iwapo 
kulikuwapo viashiria, sababu au matukio ya wazi yenye mwelekeo wa 
kujitokeza kwa shambulio hili. Tuliangalia pia iwapo wapo watu au 
makundi yaliyokwishapata kuonyesha ishara kwa matendo au kwa kauli juu 
ya uwapo wa nia hii. Uchunguzi umebaini kuwa kuliwapo viashiria vingi, 
isipokuwa Kibanda au watu wake wa karibu hawakupata kufikiri kuwa huenda
 vingeweza kuleta madhara makubwa kiasi hiki kama ifuatayo:-
1.1.
 Wiki tatu kabla ya Kibanda kuvamiwa, kutekwa na kuumizwa, gari la 
polisi aina ya gofu Na PT 180 liliwafuatilia kwa muda mrefu Absalom 
Kibanda na Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe 
likiwa limeegeshwa nje ya ofisi zao Sinza Kijiweni na baadaye 
likawafuatilia hadi Sinza Makaburini, ambapo walisimamisha magari yao na
 kuzungumza na polisi hao waliosema walikuwa wanatilia shaka magari yao.
 Baada ya kuzungumza kwa muda polisi waliondoka.
1.2. Usiku wa 
Februari 25, mwaka huu majira ya saa 09:00 usiku, Kibanda walivamiwa na 
watu walioingia kwenye uzio wa nyumba yao wakavunja kioo cha gari 
analotumia, lakini kioo kilipovunjwa ‘alarm’ ilipiga kelele, Kibanda 
akatoka nje na watu hao wakakimbia.
1.3. Kutokana na uvamizi huo,
 Kibanda na wapangaji wengine katika nyumba zilizopo kwenye uzio mmoja, 
waliona hatari ya kuvamiwa hivyo wakaanza mazungumzo na kampuni ya 
Ulinzi ya Kiwango, iliyowataka kufunga kamera za usalama na kuweka 
walinzi watano. Hadi Kibanda anatekwa, walikuwa hawajahitimisha 
mazungumzo na kampuni hii ya Kiwango.
1.4. Kuna askari anayefanya
 kazi Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) miezi minane kabla alipata kumpa
 Kibanda taarifa za kinteligensia, kuwa kulikuwapo mpango wa kumteka na 
kumuumiza. Taarifa kama hizo pia alipewa na wasamaria wanaofanya kazi 
katika Jeshi la Polisi. Kwa maneno yake Kibanda alisema:“Kuna rafiki 
yangu askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kama miezi minane au 
tisa hivi aliwahi kuniambia ‘unaandika sana usidhani kama watu 
wanakupenda. Chukua tahadhari hasa unapofika getini nyumbani kwako’. 
Tangu wakati huo nimekuwa nikichukua tahadhari sana.“Wiki mbili kabla ya
 tukio, niliwahi kuhisi kitu kama hicho [cha kuvamiwa] nikiwa getini. 
Nilipiga honi wakachelewa kuja kunifungulia, niliogopa sana. Hata 
nilipoingia ndani nilikuwa nimekosa raha kabisa.“Pia kuna rafiki zangu 
polisi waliwahi kuniambia kwamba ninatafutwa na kwamba watu 
wananifuatilia na ikibidi wanitengenezee ajali au kunifanyia kama 
Ulimboka au Kubenea.”
1.5. Ndani ya miezi mitatu mbele ya mlango 
wa ofisi yake Kibanda (Free Media Limited) ilikuwa mara kwa mara muda wa
 asubuhi anapofika ofisini anakuta damu. Haikufahamika kama damu hiyo 
ilikuwa ni ya binadamu, kuku, ng’ombe, kunguru au mbuzi, bali waliipuuza
 wakidhani ni masuala ya ushirikina. Mhariri Mtendaji wa sasa, Ansbert 
Ngurumo, amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo.1.6. Mfanyakazi mwandamizi 
wa Kampuni ya New Habari anakofanya kazi sasa Kibanda ndani ya wiki 
mbili kabla ya kutekwa na kuumizwa kwake alipata kumwabia Kibanda maneno
 mazito mara tatu, na hapa tunamnukuhu Kibanda:“Aliniambia Danny 
Mwakiteleko [aliyekuwa Naibu Mhariri Mtendaji wa New Habari] hakufa kwa 
ajali, bali alikufa kutokana na blood clotting (kuganda kwa damu). Hivyo
 ikitokea mtu ukapata ajali au ukapigwa na kuumizwa sana sehemu za 
kichwa hivi au tumbo, ni lazima madaktari wadhibiti sana blood 
clotting.“Na kweli, nilivyoletwa hapa Milpark hospitalini, madaktari 
walikuwa wananidunga sindano sita kila siku kwenye kitovu kuzuia blood 
clotting. .... (jina linahifadhiwa) aliniambia maneno haya mara tatu, 
katika mazingira yasiliyotarajiwa na kwa msisitizo ambao sikujua maana 
yake. Nasema .... (jina linahifadhiwa) naye achunguzwe kwa kina. 
Inawezekana kuna jambo analijua.”Ofisa huyu, alipishana dakika chache na
 Kibanda muda wa kutoka ofisini baada ya kipindi cha kwanza cha mechi 
kati ya Real Madrid na Manchester united kumaliza nusu ya kwanza (half 
time). Dakika ishirini baadaye Kibanda alishambuliwa.
2.0. 
Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika mwenendo 
wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013.2.1. Familia ya Kibanda na
 Kibanda Mwenyewe hawakuwa na wasiwasi wowote siku hiyo kwani hawakuwa 
na hisia wala wazo kuwa ungetokea uvamizi huo.
2.2. Kibanda 
alipopiga honi, mlinzi alisogea langoni kumfungulia. Ghafla akasikia 
kishindo kikubwa. Akasikia kelele za Kibanda akiomba msaada. Kijana huyu
 Baraka Ibrahim mwenye umri wa miaka 27, aliogopa. Aliogopa kwa mana 
hakuwa na silaha yoyote mkononi. Hakuwa na panga, kisu, rungu, wala 
filimbi. Kwa maneno yake anasema:“Nilivyoona ningefungua geti hata mimi 
ningekufa, nilikimbia kuwaamsha majirani. Sikuwa hata na namba ya simu 
ya mtu yeyote kati ya mabosi wangu ninaowalinda. Nilikuwa mimi tu, imani
 yangu na Mungu wangu.... kutokana na maisha naifanya hivyo hivyo tu. 
Vinginevyo milele nisingefanya kazi hii ya ulinzi.”Mlinzi huyo 
alikimbilia kwa majirani katika nyumba aliyoamini yumo mwanaume, lakini 
akaanza kumwamsha House Girl, ili house girl amwamshe baba mwenyenyumba.
 Kitendo cha kuamshana na kuwapa taarifa kilichukua dakika tano hadi 
saba, na ndani ya muda huo, Mlinzi anasema watekaji wa Kibanda 
walifanyafanya unyama na uasi huo na kuondoka ndani ya muda mfupi kiasi 
hicho. “Watu hawa wana mafunzo maalumu,” anahitimisha.
2.3. Mke 
wake alikwenda kazini asubuhi na kurejea nyumbani jioni, lakini tofauti 
na utaratibu wake wa kawaida ambapo huwa anaangalia televisheni sebuleni
 hadi Kibanda anaporejea nyumbani, siku hiyo alikwenda kuangalia 
televisheni akiwa chumbani na usingizi ukampitia. Anasema hakusikia honi
 wala tukio la Kibanda kutekwa. “Hii inanitesa sana moyoni. Najiuliza 
kwa nini siku hiyo tu sikukaa sebuleni? Kwa nini siku hiyo tu nimelala 
mapema kabla Baba Joshua hajarudi (machozi yanamlengalenga). Najiuliza 
sipati jibu.”2.4. Mmoja kati ya wasaidizi wawili wa nyumbani kwa 
Kibanda, alisikia kelele za Kibanda akiomba msaada. Alimwamsha mwenzake 
na kumwambia. “Nasikia Baba Joshua anapiga kelele kama amevamiwa hivi.” 
Mwenzake alimwambia “Unaota maana kuna kelele za mpira.” Siku hiyo 
kulikuwa na mechi kati ya Real Madrid na Manchester United.Ni kweli 
zilikuwapo pia kelele za wanaoshangilia mpira siku hiyo, hivyo Kibanda 
alipoomba msaada, hata waliosikia walidhani watu wanashangilia mpira. 
Binti aliwaamsha Angela na mwenzake, wakaenda sebuleni, wakakaa na 
kuchungulia dirishani, wakaona mwanga wa gari getini, lakini baada ya 
kutosikia kelele yoyote wakarejea kulala wakidhani siye. Lakini binti 
mmoja alibaki sebuleni. Baada ya muda jirani mmoja akampigia simu Angela
 kumweleza kuwa mumewe ameshambuliwa.2.5. Kibanda kwa upande wake, 
anasema alipofika getini, alipiga honi, ghafla akaona watu wawili 
wamesimama pembeni mwa gari lake na mtu wa tatu akiwa kwa mbali. Kisha 
akasikia kishindo kikubwa, akidhani wanataka kuiba gari, aliatokea 
mlango wa abiria na kuanza kukimbia huku akiita. “Mama Joshua 
nisaidieeeeee.”Katika kukimbia, aliteleza akaanguka. Huku watesaji wake 
wakisema mara tatu “Afande piga risasi.” Kibanda alijaribu kupambana, 
akashika rungu, akawahoji amewakosea nini hadi wampige kiasi hicho, 
lakini hawakumjibu lolote. Waliendelea kumpiga, hadi akapoteza fahamu. 
Hakujua jicho limetobolewa saa ngapi, meno yameng’olewaje na wala 
pingiri ya kidole chake imekatawaje. Ifuatayo ni sauti ya Kibanda 
mwenyewe. Inasikitisha ila tuwe wavumilivu na tuisikilize.
3.0. 
Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na
 nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free 
Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.
3.1. 
Mazingira ya kazi ndani ya New Habari (2006) Limited na Freemedia 
Limited, yanaacha maswali kadhaa yenye kustahili majibu. Kama 
ilivyoelezwa kwenye Hadidu Rejea Na: 1, ndani ya kampuni ya New Habari 
imekuwapo misuguano isiyo na afya kwa kazi ya Kibanda kama mwandishi na 
tasnia ya habari kwa ujumla.
3.2.Mazingira ya kazi ndani ya 
Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ni utata. Uhusiano katika chumba cha 
habari si mzuri. Ndani ya kampuni hawaaminiani na imefikia hatua 
wanatuhumiana kuwa huenda baadhi ya viongozi ndani ya New Habari 
wamehusika kumteka na kumuumiza Kibanda. Haya yameandikwa ndani ya 
mitandao ya kijamii, ikidai kwamba kiongozi mmoja ndani ya kampuni hiyo 
alihusika na utekaji wa Kibanda. Mkurugenzi wa Uhariri, Prince Bagenda 
anasema waliohusika kusambaza taarifa chafu dhidi ya kiongozi huyo wa 
New Habari wanatoka ndani ya kampuni hiyo.
3.3. Timu ya uchunguzi
 ilibaini kuwapo mgawanyiko mkubwa ndani ya New Habari (2006) Ltd kwa 
kuwapo kundi la ‘Habari Wazawa’ na ‘Habari wa Kuja’. Malalamiko mengi 
yanajikita katika msingi kuwa ajira hazitangazwi na watu wanaajiriwa 
bila kuzingatia sifa za kitaaluma.
3.4. Kibanda hakuhama Free 
Media kwa amani. Uchunguzi unaonyesha kuwa miezi kadhaa kabla ya 
kuondoka kwake alianza kupoteza mamlaka. Mwenyekiti wa Kampuni ya Free 
Media Ltd, Freeman Mbowe alianza kumsikiliza zaidi msaidizi wake ambaye 
alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji, Ansbert Ngurumo kuliko yeye Kibanda. Kwa
 maneno yake, anasema:“Nilihofu kuwa Mbowe anaweza kutugombanisha. 
Nikaona ni bora niondoke nisije nikagombana na Mbowe au Ngurumo.”Anasema
 alianza kupoteza mamlaka yake na kutoaminika kwa mwajiri wake baada ya 
kuandika makala kuhusu Abdulrahman Kinana ambayo kabla ya kuiandika 
hakuwa na wazo la kuondoka. Yaliyofuata baada ya makala hiyo, 
yalimshukuma aondoke.
4.0. Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.
4.1.
 Uchunguzi ulifuatilia masuala mbalimbali ikiwamo miendendo ya watu 
waliotajwa kwa njia moja au nyingine kuhusinaa na tukio hili. Hata 
hivyo, karibu watu wote waliohojiwa, akiwamo Kibanda mwenyewe 
aliyeumizwa walimtaja kwa kutilia shaka mwenendo wa kijana Joseph 
Ludovick. Hofu yao, iliongezwa nguvu na maandishi aliyoyachapisha 
Ludovick kwenye mitandano ya kijamii siku ya Machi 6, 2013.
4.2. 
Usiku aliotekwa na kuumizwa Kibanda, Ludovick katika naye alidai kuwa 
ametekwa katika eneo la Shekilango na kupelekwa hadi Kigogo. Baada ya 
kutekwa aliibiwa kila kitu, ikiwamo begi, laptop, simu mbili, fedha 
taslimu Sh 35,000, akavuliwa nguo na kubaki na chupi tu. Pia alieleza 
kuwa alitoa taarifa hizo kituo cha polisi Mabibo.
4.3. Maelezo ya
 Ludovick yalitiliwa shaka na watu wengi hasa baada ya kuleeza kuwa 
watekaji walitumia muda wa saa mbili kumtoa Shekilango hadi Mabibo, 
umbali ambao kwa kiwaida mwendo wake hauwezi kuzidi dakika 10. 4.4. 
Daniel Chongolo aliiambia timu kuwa alfajiri ya Machi 6, siku anayodai 
kutekwa Ludovick yeye alimuona eneo la Mabibo wakati anatoka Muhimbili. 
Chongolo alikwenda kituo cha polisi Mabibo na kupewa taarifa kuwa 
Ludovick alitoa taarifa polisi kuwa alikuwa ametekwa ila akarudishiwa 
mali zake zote. “Alipouliza amefuata nini polisi, akawambia kama raia 
mwema amefika kuandikisha kumbukumbu kwa nia ya kuonyesha kiwango cha 
uhalifu kinavyoongezeka nchini,” anasema Chongolo. Timu ya uchunguzi 
ilikataliwa kupitia leja ya polisi kama itakavyoelezwa hapa chini.
4.5.
 Pia taarifa za uchunguzi wa timu hii zinathibitisha kuwapo kwa utata 
juu ya madai ya kuibwa kwa simu za Joseph Ludovick, kwani simu yake ya 
tigo (inayodaiwa kuibwa) ilitumika saa 01:21 asubuhi siku ya Machi 6, 
2013. Muda huu ofisi za Serikali na Kampuni ya Tigo zilikuwa 
hazijafunguliwa
5.0. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika.
5.1.
 Uchunguzi umebaini kuwa maisha ya wanahabari yapo hatarini. Hatari hii 
inatokana na makundi mengi yenye masilahi kuwaona wanahabari 
wanaosimamia ukweli kuwa maadui wa masilahi yao haramu. Kuna hatari 
kubwa inayowakabili waandishi wakati nchi inapoelekea kwenye uchaguzi wa
 mwaka 2015.
5.2. Uchunguzi umebaini kuwa usiri umepungua katika 
vyombo vya habari. Tofauti na zamani ambapo habari nyeti ziliandikwa kwa
 kuhifadhi majina ya waandishi wakitumia jina la MWANDISHI WETU. Simu 
hizi hata habari za kutisha waandishi wanaweka majina yao na hata 
wasipoweka, ndani ya vyumba vya habari vingi waandishi wapo tayari 
kutaja nani ameandika habari fulani.
5.3. Usaliti miongoni mwa 
waandishi wenyewe ndani ya vyumba vya habari unazidi kuongezeka na 
usipodhibitiwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi. Mwenyekiti wa MOAT, Dk. 
Reginald Mengi anasema: “Hili ni jambo muhimu sana. Tuache usaliti 
vinginevyo wengi wataumia.”
5.4. Pia alishauri waandishi wa 
habari kurejea katika msingi wa taaluma, ambayo inawataka wao kuwa ndio 
wenye kuendesha vyombo vya habari badala ya kutegemea matakwa ya 
wamiliki au makundi yenye masilahi binafsi.
6.0. KILICHOBAINIKA:
6.1.
 Uchambuzi uliofanywa ni timu hii umebaini kuwa hoja nne zinazungumzwa 
kuhusiana na kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda. Hoja hizi ni:-(i) Kazi 
yake ya uandishi wa habari(ii) Uhusiano wa kisiasa na vyama au wanasiasa
 mbalimbali(iii)Uhusiano wa kijamii ikiwamo mapenzi(iv) Vitendo vya 
rushwa.
6.2. Timu imejiridhisha kutokana na majibu ya wengi kuwa 
dhana ya mapenzi na rushwa, havina nafasi yoyote katika tukio hili. Wote
 waliohojiwa walieleza pasi na shaka kwamba suala hili la kushambuliwa 
na kuumizwa kwa kiwango kikubwa kwa Kibanda, halina uhusiano wowote na 
rushwa au mapenzi.
6.3. Kutokana na yaliyotajwa hapo juu kazi 
yake na siasa vikiunganishwa vimechangia kwa kiasi kikubwa kuvamiwa kwa 
Kibanda. Timu imebaini kuwa kuna kutupiana mpira kati ya vyombo vya dola
 na vyama vya siasa. Mchezo huu mchafu unaweza ukawa mwanzo wa kuumizwa 
kwa Kibanda na waandishin wengine.
6.4. Baadhi ya waliohojiwa 
walidai kuwa utekaji huu umefanywa na vyombo vya dola ukiwa sehemu ya 
mpango mkakati wa vyombo hivi kukihusisha Chama cha Demokrasia na 
Maendeleo (CHADEMA) na vitendo vya ugaidi.6.5. Wanayataja matukio ya 
Uchaguzi Mdogo wa Igunga, maandamano ya Morogoro na Mkanda anaodaiwa 
kurekodiwa Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare kuwa 
vililenga kukifanya CHADEMA kichukiwe na Watanzania kwa kukitaja kama 
chama cha kigaidi ambacho kinateka watu na kinawaumiza.
6.6. 
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anadai kwamba mpango kama huo 
vyombo vya dola viliutumia kwa NCCR Mageuzi vikakisambaratisha, Chama 
cha Wananchi (CUF) kilisingiziwa udini kikapoteza mwelekeo na sasa 
vyombo hivyo vililenga kukifanya CHADEMA kionekane cha kigaidi mbele ya 
macho ya jamii ndiyo maana imerekodiwa mikanda kwa nia ya kuitumia 
kujenga hoja hiyo.
6.7. Wakati Mbowe akisema hayo, baadhi ya watu
 waliohojiwa wanadai kuwa CHADEMA kimepewa mafunzo na ushauri kutoka nje
 ya nchi kuwa kikitumia baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wasiokuwa
 waaminifu kuteka, kuumiza na hata kuua baadhi ya watu maarufu nchini 
wakiwamo waandishi na wanasiasa, basi wananchi wataamini kuwa Chama Cha 
Mapinduzi na Serikali yake kimeshindwa uongozi na sasa kimeanza kazi ya 
kuua wanaowapinga.
6.8. Kwa njia hiyo, inaelezwa kuwa hesabu za 
Chadema ni kuwa wananchi wataichukia CCM na Serikali yake na kukipa 
nafasi ya kuingia madarakani. Hapa kauli ya Chadema kuwa NCHI 
HAITATAWALIKA itakuwa imetimia.
6.9. Dhana nyingine iliyojitokeza
 ni kuwa wapo wafanyabiashara ambao wana vita binafsi, hivyo wanaamua 
kuumiza watu wasiowaunga mkono katika mipango yao na hilo ndilo 
limemkumba Kibanda, baada ya kuwa ameepusha mauaji ya mwandishi mmoja na
 aliyekuwa ameandaa mpango wa kuua mwandishi huyo hakuridhika hivyo 
akaamua amshughulikie Kibanda.
7.0. MAPENDEKEZO:Baada ya Timu kupata taarifa hizi na nyingine nyingi, inapendekeza yafuatayo:-
7.1. Taarifa hii ichukuliwe kama chanzo cha uchunguzi zaidi wa vyombo husika.7.2.
Yanahitajika
 marekebisho makubwa na ya haraka katika mifumo ya uendeshaji wa vyumba 
vya habari kwa nia ya kurejesha misingi ya uandishi wa habari 
inayokubalika.
7.3. Usalama wa wanahabari unapaswa kupewa 
kipaumbele na wamiliki, wanahabari wenyewe na jamii kwa ujumla. Hapa 
Timu inapendekeza yawepo mafunzo ya kuwawezesha wanahabari kutambua 
viashiria vya hatari na kuchukua hatua mara moja.
7.4. Kwa 
kiwango alichoumizwa Kibanda iwapo mwajiri wake asingejitolea kugharamia
 matibabu, hatujui hatima yake ingekuwaje leo hii. Tunapendekeza taasisi
 na mifuko mbalimbali inayojihusisha na masuala ya wanahabari kama 
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) , Baraza la Habari Tanzania (MCT), 
Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) na Umoja wa Klabu za Waandishi
 wa Habari Tanzania (UTPC) kuanzisha mfuko wa pamoja utakaotumika 
kugharamia matibabu ya waandishi watakaoumia wakiwa kazini.
7.5. 
Tukio la kutekwa kwa Kibanda limeonyesha mwanga kuwa wahariri 
tumegawanyika mno. Habari zilizochapishwa katika magazeti mbalimbali na 
mitandao ya kijamii zimeonyesha haja ya kuwafanya wahariri kuwa kitu 
kimoja kwa kuondoa tofauti zao zisizo na masilahi kwa tasnia ya habari.
7.6.
 Kuna viashiria vingi kuwa kuelekea mwaka 2015 matukio ya waandishi 
kuumizwa au kutekwa yanaweza kuongezeka kutokana na wanasiasa na vyama 
kuwania madaraka huku wakitumia baadhi ya watumishi katika vyombo vya 
dola. Kwa mantiki hiyo, vyombo vya habari na waandishi wa habari 
wachukue tahadhari kuanzia sasa.
7.7. Taasisi za habari zifanye 
juhudi za makusudi kukutana na vyama viwili vya siasa vya CCM na CHADEMA
 haraka iwezekanavyo, kuzungumzia viashiria hivi vya hatari 
vinavyoelekea kuvuruga amani ya Tanzania.
8.0. HITIMISHO:Ni 
dhahiri kuwa kupigwa na kuteswa kwa Kibanda kumejiegemeza katika siasa 
na kazi yake, hali inayofanya makundi muhimu kuchukua wajibu wa msingi. 
Kwa upande wa Serikali ni muhimu kufuatilia viashiria katika taarifa hii
 kwa nia ya kupata ukweli zaidi na kuchukua hatua stahiki za kisheria 
dhidi ya wahusika.Na kwa upande wa vyombo vya habari na taasisi za 
kihabari zinapaswa kutambua viashiria vinavyohatarisha usalama wa 
waandishi wa habari na wahariri na kutengeneza mazingira yatayokuwa 
salama zaidi kwa waandishi kufanya kazi zao.
9.0. SHUKRANI:
9.1.
 Tunapenda kulishukuru Jukwaa la Wahariri Tanzania, kwa kufanya uamuzi 
sahihi wa kuwezesha kufanyika kwa uchunguzi huu ulioanza kuonyesha 
mwanga wa nini kilitokea.
9.2. Tunapenda kulishukuru Baraza la 
Habari Tanzania (MCT) kwa kushiriki kikamilifu na kuiwezesha timu hii 
kwa Rasilimali Watu na Mali kufanikisha kazi hii.
9.3. Tunapenda 
kuwashukuru Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa uwezeshaji wa 
ruzuku, uliofanikisha kufanya uchunguzi wa kihabari uliohusisha kwenda 
nchini Afrika Kusini kufanya mahojiano na Kibanda. Uwezeshaji huo pia 
unahusisha kutengeneza mwongozo kwa waandishi wenye lengo la kuwaepusha 
na hatari za kiusalama.
9.4. Tunawashukuru Kibanda, mkewe 
Angela, wanafamilia, ndugu na jamaa wa Kibanda na wanahabari wote 
waliohojiwa kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Timu hii.
9.5. 
Tunawashukuru wahariri wote kila mtu kwa nafasi yake, kutokana na 
ushauri wa mara kwa mara mliotupatia katika kufanikisha uchunguzi huu.
10.0.
 WAJUMBE WA TIMU:Timu hii iliundwa na wajumbe watano ambalo ni:1. 
Deodatus Balile – Mwenyekiti2. Pili Mtambalike – Mjumbe3. Jane Mihanji –
 Mjumbe4. Tumaini Mwailenge – Mjumbe5. Rashid Kejo – Katibu
Mwisho.