KOCHA wa zamani wa Simba, Milovan Cirkovic ametua nchini jana kufuatilia fedha zake za kuvunjwa mkataba kati yake na klabu hiyo, imefahamika.
Chanzo cha habari makini kutoka ndani ya Simba, kimeambia mtandao huu kwamba, Milovan alitua jana na amepanga katika hoteli moja katikati ya jiji la Dar es Salaam kufuatilia madai yake ambayo ni zaidi ya Sh. 100 milioni.
Fedha anazodai Milovan zinatokana na fidia ya kusitishwa kwa mkataba wake na klabu hiyo ambayo sasa inanolewa na Patrick Liewig raia wa Ufaransa.
Milovan raia wa Serbia alifanikiwa kuipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara klabu ya Simba, lakini msimu huu ameifundisha timu hiyo kwa mzunguko mmoja tu kabla ya kutupiwa virago na klabu hiyo alipoenda kwao kwa likizo.
Inaelezwa kwamba, Milovan amekuja nchini baada ya kupenyezewa habari kwamba, Simba imemuuza mshambuliaji wake Emmanuel Okwi na ipo mbioni kutia kibindoni kiasi cha zaidi ya Sh. 400 milioni.
Taarifa zinasema, Milovan amepanga malipo yake yatokane na mauzo hayo ya Okwi kwani anaamini akikosa fedha kupitia mauzo hayo, hatoweza kupata fedha katika muda mfupi kutoka Simba.
“Kocha amefika jana na yupo katika hoteli ya (anaitaja), yeye amefuatilia fedha zake na anadhani anaweza kulipwa kwani amepewa taarifa kwamba kuna fedha za mauzo ya Okwi,” kimesema chanzo chetu makini kutoka ndani ya Simba.
Mtandao huu ulijaribu kumtafuta Milovan kwa njia ya simu leo kuanzia asubuhi hadi mchana na hatukumpata lakini juhudi zinaendelea ili kuweza kuzungumza naye kufahamu zaidi kuhusu mlolongo wa malipo ya fidia yake.
Shaffidauda.com uliwasiliana na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye alisema hana taarifa za ujio wa Milovan licha kutoweka wazi malipo ya kocha huyo.
“Sifahamu lolote kama Milovan amekuja nchini, hata hayo malipo yake siwezi kuyazungumzia kwa sasa. Nikipata taarifa yoyote tutawasiliana,” amesema Kaburu.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog