KLABU ya soka ya Simba, ipo mbioni kuwatimua kikosini wachezaji wake watatu na jana kocha Patrick Liewig aliwatimua mazoezini wachezaji Haruna Moshi ‘Boban’ na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
Habari zaidi ambazo zimethibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, wachezaji hao watajadiliwa na kamati ya utendaji kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utovu wa nidhamu.
BOBAN, CHOMBO WATIMULIWA MAZOEZINI
Wachezaji Boban na Chombo jana walitimuliwa katika mazoezi ya timu hiyo kwa kile kilichoelezwa kwamba, hawaendani na mazoezi ya Kocha Liewig.
Baada ya kuwavumilia kwa muda mrefu, Liewig aliwaita wachezaji hao na kuwataka kutoka katika kundi la wenzao kisha akawalekeza kwenda kaskazini mwa Uwanja wa TCC.
Wachezaji hao walifanya hivyo hadi wenzao walipomaliza mazoezi na moja kwa moja ilionekana Liewig amefikisha suala lao kwa uongozi ili waweze kuchukuliwa hatua zaidi.
Hata hivyo, mara baada ya kuondoka baadaye, meneja wa Simba, Moses Basena, alimpigia simu Chombo na kumtaka leo audhurie mazoezi ya timu hiyo kama kawaida.
Hiyo ina maana kwamba, Chombo hana kosa kwa Liewig lakini Boban amekalia kuti kavu, kwani hajaitwa na moja kwa moja jina lake limepelekwa kwa uongozi kwa hatua zaidi.
MWINYI KAZIMOTO, NGASSA, BOBAN KIKAANGONI
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ameuambia mtandao huu kwamba wachezaji watatu wa timu hiyo, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto na Boban majina yao yametua kwa uongozi ili waweze kujadiliwa kutokana na kukithiri kwa utovu wa nidhamu kikosini.
Bila kufafanua aina ya utovu wa nidhamu walionao wachezaji hao, Kaburu anasema; “Kocha ametuletea majina ya wachezaji hao na kusema tukae nao kisha tujue kama wanataka kuendelea kuichezea Simba au vinginevyo.”
“Kocha wetu yupo makini katika suala zima la nidhamu na kama mchezaji hana nidhamu, tutatmwondoa kikosini.”
Mtandao unakuahidi kufuatilia zaidi matokeo ya kikao cha uongozi wa Simba juu ya kuwajadili wachezaji hao.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog