Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda ameagiza kuundwa kwa kamati maalumu itakayohusisha pande mbili za waumini wa dini ya Kiislam na Kikristo, ili ishughulikie mgogoro mbichi unaohusu haki ya kuchinja wanyama.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana alipofika mkoani Mwanza na kufanya kikao -kilichodumu kwa saa tano- na wawakilishi wa madhehebu ya dini hizo mbili ikiwa ni hatua ya kutafuta njia ya kutatua mgogoro wa nani mwenye haki ya kuchinja wanyaka kati ya waumini wa dini hizo mbili.
Kwa wakati huu, Waziri Mkuu amesema shughuli hiyo iendelee kufanywa kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa desturi zilizokuwepo hadi hapo yatakapofikiwa na kutolewa maagizo mapya.
Waziri Mkuu ameagiza kamati hiyo ifanye shughuli zake na kuwasilisha ripoti yake Serikalini haraka iwezekanavyo kwa ajili ya hatua zaidi za kimaamuzi.
Hata hivyo, hadi Waziri Mkuu anaondoka katika kikao hicho, Waislam waliridhia kuundwa kwa Kamati hiyo wakati Wachungaji na Mapadre walikataa.
Waziri Mkuu alikumbushia kuwa suala hili ni la kiimani na ijapokuwa Serikali haina dini, wananchi wake wanazo imani kwa mujibu wa dini zao hivyo ni vyema Wachungaji, Mapadre na Masheikh wakawasihi waumini wao kuwa na subira hadi hapo utakapopatikana ufumbuzi mwingine.
Waziri Mkuu pia ameonya kuhusu redio mbili ambazo zimenyooshewa vidole na waumini wa pande zote mbili kuwa zinachochea uhasama wa kidini. Akazitaja kuwa ni redio Imani iliyopo Morogoro na redio Neema iliyopo mkoani Mwanza na kuzionya kuhusu mafundisho yake ambayo ikilazimu, Serikali itachukua hatua dhidi yake.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog