Facebook Comments Box

Sunday, February 17, 2013

CHUO CHA ST JOHN'S DODOMA CHAFUNGWA BAADA YA WANAFUNZI KUGOMA

Chuo Kikuu cha St John’s cha mkoani Dodoma kimefungwa baada ya wanafunzi kususia mitihani wakituhumu na kupinga unyanyasaji wanaofanyiwa na wahadhiri kwa kuwangusha kwenye mitihani na baadhi kuwabaka wanafunzi wa kike.

Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Gabriel Mwaluko, wanafunzi zaidi ya 290 wamesimamishwa masomo baada ya kukiuka sheria na kugomea mitihani, hivyo chuo kimefungwa kikisubiri taratibu za kinidhamu kuchukuliwa.

Awali uongozi wa serikali ya wanafunzi wa chuo ulieleza kuwa wanafunzi 290 wa St John’s na vyuo vikuu vishiriki vya Dar es Salaam walisimamishwa masomo huku uongozi wa chuo ukiwapa barua za kuwaondoa chuoni kuanzia wiki hii.

Habari hizo zilisema wanafunzi 196 wanaosoma Dodoma na wengine 94 wanaosoma katika vyuo vishiriki vya St. Mark's na Town Centre vya jijini walipewa barua za kuondolewa chuoni.

Rais wa serikali ya wanafunzi, Andrew Chiduo, akizungumza na NIPASHE Jumapili, alisema hatua ya kuwasimamisha inalenga kuwatisha ili kuendelea kuwalinda walimu wanaodaiwa kuwanyanyasa na kuwadhalilisha na kwamba wanasusia kufanya mitihani inayofanyika mwezi huu. Alisema wahadhiri wanalazimisha kufanya ngono na wanafunzi wa kike, kuwabaka na wale wanaokataa wanaangushwa kwenye mitihani.

Alisema katika tukio la hivi karibuni muhadhiri (jina tunalo) alituhumiwa kumbaka mwanafunzi baada ya kumhadaa kumpa mitihani mingine baada ya kushindwa ile aliyofanya mhula uliopita. Alisema wamelazimika kugomea mitihani baada ya mhadhiri mmoja (jina linahifadhiwa) kuwafelisha kwa makusudi wale wanaochukua kozi ya biashara wa mwaka wa kwanza huku akiwapa vitisho.

Akijibu tuhuma hizo Profesa Mwaluko alisema madai ya mwalimu kumbaka mwanafunzi yanachunguzwa kwa kuwahusisha polisi, kadhalika alisema mhadhiri anayetuhumiwa kuwafelisha wanafunzi madai yake yanafuatiliwa pia.


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU