Facebook Comments Box

Saturday, January 26, 2013

MAANDAMANO YA GESI MTWARA NI MWAMKO WA WANANCHI

Tatizo linalojitokeza Mtwara isichanganywe na laana za rasilimali zinazoikumba bara la Afrika. Huu ni mwamko mpya ambapo wananchi wanatambua haki zao za msingi na kuamua kuyapigania, hasa rasilimali zao kwa lengo la kujikwamua kutoka kwenye umasikini unaowakabili. Serikali iliyo madarakani isiingize pamba masikioni na kuligeuza swala la kupingwa na wananchi kuwa la kisiasa. Ni vyema serikali ikajitathmini kwa umakini mkubwa na pia ikaheshimu maoni ya wananchi ili ijiokoe Desturi ya kutengeneza mikataba mikubwa kwa usiri na viongozi wa umma wasio na maadili, imewaletea wananchi wa Tanzania matatizo makubwa ya kiuchumi. Tatizo la Mtwara ni zao la udanganyifu kwenye mikataba yetu. Ni tatizo linalotoa nafasi ya kipekee kwa serikali yetu kujitathmini na kupitia upya sera zake za kiuchumu na uwekezaji, ambazo zimekuwa kandamizi, danganyifu na isiyo na tija kwa raia wa Tanzania. Kuna baadhi yetu ambao wanaweza kuyafananisha migogoro nchini Kongo na Nigeria na maandamano ya Mtwara. Kwa hakika Migogoro ya Kongo na Nigeria ni tofauti na huu wa Mtwara. Wa-kongo na Wanaigeria ni makundi ya kipiganaji ambayo yapo kwenye mapambano na serikali zao. Wanapigania uongozi na utawala wa nchi. Ni watu wenye silaha nzito zinazolenga kuzing’oa serikali zao, tofauti na wana mtwara wanaopigania haki na maendeleo ya kiuchumi. Wana Mtwara wanapinga ufisadi na dhuluma inayoendelezwa na serikali kupitia maandamano ya amani Wana Mtwara ni raia wa kawaida wasiokuwa na silaha yoyote isipokuwa nafsi zao. Wakufunzi wa historia watakubaliana nami kwamba, katika historia ya dunia, hakuna jeshi ambayo imeweza kuishinda nguvu ya umma, hasa pale wananchi wanapoamua kupigania haki zao kutumia njia ya amani. Mfano wa ufisadi unaopingwa na watu wa kusini mwa Tanzania ni ule wa gharama ya ujenzi wa bomba la gesi. Kwani vyombo vya habari vimenukuliwa vikisema kwamba, tathmini ya ujenzi kutoka mtwara hadi Dar-es-salaam, ilikuwa ni dola za kimarekani 600millioni, lakini cha ajabu, mwisho wa siku gharama hiyo imeongezeka na kufikia dola za kimarekani 1.2billioni. Wananchi hawawezi kunyamazia ufisadi kama huu. Na kwa mwenendo huu, nguvu yao inazidi kuongezeka na hakuna chochote ambacho serikali inaweza kukifanya kujinasua. Ni bora serikali ikakiri makosa na kuwashugulikia mafisadi waliojiusisha na huu hujuma dhidi ya watanzania. Kwani mwisho wa siku, hiyo hasara atakayebebeshwa ni mtanzania ambaye amechoswha na dhuluma pamoja na umasikini. Siyo fisadi aliyeficha fedha Uswisi Ugunduzi wa mafuta nchini Kanada umewaletea neema ya kiuchumi wananchi wa jimbo la Alberta, na uchumi wa Kanada kwa ujumla. Malipo ya dola 120 za kimarekani kwa lisaa limoja kwa wahitimu wa sekondari, ni ya kawaida. Wakazi wa Alberta wanafurahia rasilimali zao. Makampuni ya mafuta yanashiriki kikamilifu kusaidia miradi ya kijamii. Lakini katika hali ya kusikitisha kule Tarime (Nyamongo) wakazi wa maeneo yale wamekuwa masikini zaidi ya walivyokuwa kabla ya wawekezaji kuchukua ardhi yao. Vyanzo vyao vya maji vimechafuliwa na havifai tena, mifugo na hata baadhi ya wakazi wanakufa na mangonjwa yasiyojulikana Umasikini, ukiwa, na ukosefu wa ajira unatawala Tarime, kwani hata wachimbaji wadogo wadogo hawana ardhi tena ya kuchimba, huku wageni wakipewa ajira ndogo ndogo kama za kuendesha malori ya mchanga ambazo zingefanywa na wazawa wa Tarime. Inasikitisha kuwaona Wakenya, Wa Afrika Kusini, Wa Kanada na Wa Australia wakiendesha hayo malori huku wakazi wa Nyamongo wakionekana kama adui kwenye ardhi yao. Na hayo ndio baadhi ya matatizo ambayo serikali yetu imeyafumbia macho, hasa serikali inapoamua kuwatumia polisi kuwaua raia wanaodai haki yao ya kupata riziki. Wana Mtwara wanaandamana kudai maendeleo ya kiuchumi. Watu wa kusini wameiona gesi asilia kuwa ndio njia pekee ya kujikwamua kutoka kwenye umasikini. Wameshuhudia ndugu zao kule Tarime wanavyonyanyaswa na serikali na hata kuuwawa na polisi. Hawataki tena ahadi. Wanachokita ni utekelezaji utakao boresha maisha yao. Serikali isifanye kosa ya kupuuzia haya madia . Wasithubutu kuyaletea siasa au kajaribu kutumia nguvu ili kuwaziba midomo wanaharakati wanapinga gesi kupelekwa Dar-es-salaam, badala yake, serikali iwe makini katika kutafuta chanzo cha matatizo na suluhisho la kudumu Serikali makini itajiuliza maswali ya msingi kama vile ni kwa nini wananchi hawataki gesi isafirishwe kwenda Dar-es-salaam. Katika kujitathmini, bila shaka itapata majibu mbalimbali . Itagundua kwamba tupo katika nyakati tofauti. Wakati wa kizazi cha Intaneti, hasa vijana wenye muamko na hamasa wasiotaka kuwatwika wengine lawama ya matatizo yanayowakabili. Serikali itagundua kizazi cha kipekee kisicholaumu wengine kwa ufukara wao. Kizazi kisichoogopa mabomu ya machozi, maji ya kuwasha au risasi za moto. Kizazi kisichoshabikia uomba-omba. Serikali itagundua kizazi kinachotaka kujikwamua kutoka kwenye umasikini kutumia rasilimali na vipaji vyao. Ni kizazi kipya kinachotaka ajira, elimu bora, huduma bora za afya na miundombinu inayoridhisha. Ninamaanisha kizazi kinachoelewa wazi kwamba, WACHINA hawana upendo nao, ila WACHINA wanapenda rasilimali zao. Watu wa kusini wamegundua kwamba hadithi za Abunuwasi haziishi, na uhakika wa kuishi maisha ya neema ni lazima yaanzie kwao wenyewe kwa kuamka kutka usingizini. Na kwa hakika, wanakusini wameamka. Na kama serikali haitashugulikia madai yao, basi mwisho wa hiyo serikali siyo swala la mjadala. Wanakusini wamegundua kwamba, ni lazima “waamke” na kujitegemea badala ya kusikiliza ahadi ambazo wamekuwa wakiyasikia kwa miaka 50 iliyopita. Waheshimiwa Mwakyembe, Kagasheki, Magufuli na Muhongo wanajulikna kuwa wachapakazi wasiowaonea aibu majambazi ya kiuchumi -Mafisadi-. Lakini hawa viongozi wakiendelea kufanya kazi katika mazingira ya kuzungukwa na majambazi ndani ya serikali, na wanasiasa wasiokuwa na nidhamu katika kusimamia rasilimali za umma. Basi watabaki kuwa mateka wa mafisadi ingawa wengi wa hao mafisadi, serikali inawahamu. Kizazi cha simu za mikononi na ujumbe mfupi, na mitandao ya kijamii wameamka kutoka usingizini, na kasi yao ni ya kutisha. Hakuna wa kuwazuia. Hawataki propaganda za kisiasa na misaada ya KICHINA ambayo mara nyingi ndio chimbuko la ufisadi tunayoiona nchini kwetu, kama hiyo ya Mtwara. Wametambua wanayoyataka na kwa muda wanaoutaka wao. Maandamano ya Mtwara ni moto utakaosambaa kwa kasi. Ni moto wa UAMSHO. Unawaamsha wananchi waliolala kujua haki zao za kimsingi. Serikali ijitathmini na kuyashugulikia kero za wananchi mapema. Mafisadi wasipewe nafasi kuiyumbisha nchi Mungu Ibariki Tanzania

John Mashaka
mashaka.john@yahoo.com

Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU