Baadhi
ya washiriki wa mkutano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania
(TCRA) na kampuni za mitandao ya simu Tanzania wakisikiliza maoni
mbalimbali, Dar es Salaam jana, kuhusu utozaji wa viwango sawa kwa
upigaji simu kwa mitandao yote nchini ifikapo Mwezi Machi mwaka huu.
(Picha: Charles Lucas/MAJIRA)
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kampuni za mitandao ya simu Tanzania wakisikiliza maoni mbalimbali, Dar es Salaam jana, kuhusu utozaji wa viwango sawa kwa upigaji simu kwa mitandao yote nchini ifikapo Mwezi Machi mwaka huu. (Picha: Charles Lucas/MAJIRA)
Mapendekezo ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kampuni za simu kushusha gharama hizo kwa dakika kuanzia Machi mosi mwaka huu ili kumpunguzia gharama ya kupiga simu kwa mteja wa kampuni moja ya simu ya mkononi kwenda kwa mteja wa kampuni nyingine yamekubaliwa kwa kiasi kikubwa.
Wakizungumza Dar es Salaam jana katika mkutano wa kukusanya maoni ya wadau na watumiaji wa simu za mkononi ulioandaliwa na TCRA, Kampuni za Airtel Tanzania, Tigo Tanzania na Vodacom Tanzania zilidai punguzo hilo litawapotezea mapato na kuvuruga nia yao ya kuendelea kuwekeza.
Mwakilishi wa Airtel Tanzania, Mwanasheria Clara Mramba, alisema wao wanakubali punguzo hilo lakini gharama zishuke kwa hatua kutoka mwaka mmoja hadi mwingine kwa kuanzia Sh 84 Machi hadi Sh 29.26 mwaka 2017. Alidai kuwa kushuka kwa kiwango hicho kikubwa cha Sh 34.92 Machi, kunaweza kuharibu uwekezaji wao:
Tunataka ianze kushuka kutoka shilingi 112 hadi shilingi 85 kwa mwaka huu, shilingi 63 kwa mwaka unaofuata, shilingi 47 kwa mwaka unaofuata, shilingi 34.5 kwa mwaka unaofuata na shilingi 26.96 kwa mwaka unaofuata.
Mkisema mshushe gharama hizo kutoka shilingi 112 hadi shilingi 35 ambazo ni sawa na asilimia 69 mtapunguza kasi ya uwekezaji wetu kwa sababu sekta ya mawasiliano inahitaji uwekezaji mkubwa.
Mwakilishi wa Vodacom Tanzania, Mwanasheria Walarick Ngitu, alisema kama gharama hizo zitashuka kwa kiasi hicho watashindwa kufunga minara ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini.
Alipendekeza punguzo lianze kwa asilimia 35 na mwakani asilimia 20 na kwenda taratibu hadi mwaka 2017 jambo litakalosaidia sekta hiyo ikue huku gharama ikipungua taratibu:
Watu wengi wa vijijini wanapigiwa zaidi simu kuliko wao kupiga, kwa hiyo mkishusha gharama hizo ni wazi minara ya mawasiliano haitafungwa vijijini kwa sababu kampuni itakuwa haipati faida na itawekeza zaidi mijini, tunaomba bei hizo zisishuke kwa uharaka wa namna hiyo.
Mwakilishi wa Tigo Tanzania, Revocatus Nkata, alisema endapo gharama hizo zitashuka zitawasumbua kulipa kodi ya Serikali kwa sababu mapato yao yatapungua. Alitaka punguzo lianzie Sh 80 na soko lisiingiliwe kwa kuwa tayari limekomaa ili liendelee na ushindani:
Uwekezaji wetu tunaotaka kuufanya lazima utapungua kama gharama hizi zitapungua, pia ni dhahiri tutapata tabu ya kulipa kodi serikalini.
Si hivyo tu, bali soko la mawasiliano sasa hivi limekomaa hivyo halihitaji kuingiliwa, bora liachwe na kampuni ziendelee kufanya biashara.
Kampuni za Sasatel, Sixtelecom, Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), BOL na Zantel na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia zimekubali gharama hizo kushuka.
Mwakilishi wa Sasatel, Godfrey Murisi, alisema punguzo hilo litawafaidisha wateja na watakuwa waaminifu kutokana na huduma wanazozipata.
Mwakilishi wa Sixtelecom, Said Abdala, alisema Tanzania ndio nchi pekee ambayo ina gharama kubwa katika muingiliano wa simu na ikishuka italeta ushindani katika soko.
Mwakilishi wa TTCL, Mrisho Shaaban, alisema mtumiaji wa simu hatakiwi kubebeshwa gharama zisizo za lazima na agizo hilo lilitakiwa kuanza mapema kabla ya Machi, mwaka huu.
Mwakilishi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Samson John, alisema gharama hizo zitakaposhuka zitampa mtumiaji unafuu wa kupiga simu na itaondoa ukiritimba katika soko:
Gharama zikishuka maana yake mtumiaji atafaidika na kampuni nyingine mpya zitapata nafasi ya kutoa huduma za mawasiliano sokoni, sisi tunataka sekta ya mawasiliano ikizidi kutanuka na ukiritimba wa baadhi ya kampuni uondoke.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Samson Mwela alisema wamekubaliana na mapendekezo hayo, kwa kuwa sekta hiyo inaendeshwa kwa ushindani ambao unalindwa, hivyo ni lazima mtumiaji apate haki zake.
Alisema kupungua kwa gharama hizo, kutawapunguzia watumiaji mzigo wa simu ikiwa ni pamoja na kudhibiti simu bandia zinazotumiwa na wengi na kuongeza unafuu wa matumizi ya simu mpaka vijijini.
Stanley Mwabulambo wa Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC), alibainisha kuwa waliunga mkono kwa kuwa mpango wa kibiashara wa kampuni hizo hutegemea gharama za muunganisho.
Alizitaka kampuni hizo kuwa bunifu katika ushindani huku akitaka punguzo hilo lionekane kwa mteja na TCRA ihakikishe punguzo hilo haliongezwi upande mwingine.
Mkuu wa Idara ya Ushawishi na Utetezi wa Ushindani kutoka Tume ya Ushindani (FCC), Shadrack Nkelebe alisema mapendekezo hayo yataongeza ushindani kwa kuruhusu wateja kuwa na chaguo na kampuni moja.
Waziri wa zamani wa Ujenzi na Uchukuzi, Nalaila Kiula aliunga mkono mapendekezo hayo na kuitaka TCRA kuzitazama zaidi kampuni za simu kwa manufaa ya wateja kutokana na huduma wanazotoza gharama kubwa.
Akifunga mkutano huo wa mwisho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TCRA, Jaji mstaafu, Buxton Chipeta, alisema maoni yaliyotolewa yatafanyiwa kazi:
Mawazo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi na tutakuja na jibu moja kabla agizo halijaanza kutekelezwa, nia yetu kubwa tunataka mtumiaji wa simu asiumizwe na mtoa huduma za mawasiliano naye asiumie.
Mkurugenzi wa Ofisi za Kanda wa TCRA, Victor Nkya alisema jana kwamba katika mapendekezo yao gharama hiyo inatakiwa kushuka kuanzia Machi kutoka Sh 112 ya sasa mpaka Sh 34.92. Mwakani inatarajiwa kuwa Sh 32.4; mwaka 2015 Sh 30.58; mwaka 2016 Sh 28.57 na mwaka 2017 Sh 26.96.
Kutokana na mapendekezo hayo ambayo yalitokana na utafiti uliobaini kuwa gharama hizo nchini ni kubwa, wadau na kampuni zilizohudhuria kongamano la wadau la kujadili bei hizo, walikubali.
TCRA ilitoa mapendekezo hayo baada ya kupata ripoti ya Kampuni Mwelekezi Mshauri kutoka Uingereza iliyofanya utafiti kwa kuangalia mapato na faida za kampuni za simu nchini.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog