Facebook Comments Box

Friday, December 19, 2014

SSERUNKUMA MAJANGA SIMBA: HUENDA ASICHEZE MECHI YOYOTE YA LIGI

Wakati Simba SC ikidai kumalizana na mshambuliaji Mganda Simon Sserunkuma na kupata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC), klabu yake ya Express imesema imechezewa rafu na itavunja uhamisho huo sanjari na kuipeleka
Simba mahakamani kwa kughushi nyaraka.

Baada ya kufanya vizuri katika mechi yao ya kwanza ya majaribio Tanzania wakiisaidia Simba kuifunga Yanga mabao 2-0 Jumamosi, Sserunkuma na beki wa kati Juuko Murshid (Mganda pia),walisaini mikataba ya kuitumikia
klabu hiyo ya Msimbazi. Sserunkuma alisaini mkataba wa miaka miwili wakati Murshid alisaini miaka mitatu.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Express SC Francis Ntalazzi amekaririwa na mtandao wa Kawowo Sports leo akilia kufanyiwa rafu na Simba katika kukamilisha usajili wa Sserunkuma uliofanyika Jumapili, siku moja baada ya mechi ya ‘ndondo’
ya ‘Nani Mtani Jembe 2′.

Akielezea faulo iliyofanywa na Simba kufanikiwa usajili wa Sserunkuma, Ntalazzi anahoji juu namna saini yake ilivyoghushiwa kwenye mkataba wa mchezaji huyo.

“Binafsi, sikusaini nyaraka yoyote kuthibitisha uhamisho wa mchezaji husika (Sserunkuma) hivyo saini ilighushiwa,” kiongozi huyo wa juu
amesema huku akiweka wazi kusudio la kuipeleka Simba mahakamani kwa udanganyifu na amejipanga kuhakikisha anavunja uhamisho wa mchezaji huyo.

Ingawa uongozi wa Simba haukuwa tayari kuweka wazi fungu ambao nyota huyo amepewa kabla ya kukubali kumwaga wimo, ilielezwa jana kuwa ilimpatia dola la Marekani 40,000 (Sh. milioni 67).

Baada ya kusaini dili hiyo, (Sserunkuma) alirejea kwao Uganda na katika hali ya kushtusha Jumanne alikuwa miongoni mwa nyota wa Express, timu hiyo ilipochapwa mabao 2-1 dhidi ya Kikosi cha Bul F.C katika mechi ya Ligi Kuu ya
Uganda msimu huu.

Kabla na baada ya mechi hiyo, Sserunkuma alionekana akigawa pesa kwa wachezaji wenzake na viongozi wa Express kama ishara ya kuagana.
Sserunkuma, ambaye aliwahi kukipiga na klabu za Kyegenra Happy Boys F.C, Victors, SC Villa, Vipers na Express alisema; “Nimefurahi kuhamia Simba na ninawashauri wachezaji wenzangu kujifua kwa bidii, kuwa na nidhamu, kila mmoja na muda wake maalum katika maisha.”

SIMBA WANASEMAJE
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, baada ya kutafutwa na mtandao huu kuzungumzia suala hilo, amesema Sserunkuma hana mkataba na klabu, bali wakala wake ndiye amekuwa akiingia mikataba na klabu zinazomsajili.

“Mkataba wa Sserunkuma na Express ulionesha kwamba hamzuii kujiunga na timu yoyote muda wowote. Sisi tumeingia mkataba na wakala wake kama ilivyokuwa kwa Express,” amesema
Hanspope. Ameongeza kuwa walipata ITC ya mchezaji huyo kutoka Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) siku mbili baada ya kumsainisha mkataba (Jumanne).

Kuhusu kucheza mechi ya Ligi Kuu ya Uganda akiwa na Kikosi cha Express ilhali amejiunga na Simba, Hanspope amedai hawana taarifa hizo huku akiahidi kufuatilia suala hilo.


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU