Facebook Comments Box

Tuesday, October 21, 2014

DIAMOND KUSIMAMA KIZIMBANI??


 Naseeb Abdulmaliki (Diamond Platnum) akiwa na sare za Jeshi
Hapa akiwa jukwaani

Msanii nyota wa muziki wa Bongo Flava nchini, Naseeb Abdulmaliki (Diamond Platnum) huenda akaingia matatani baada ya kupanda jukwaani kutumbuiza katika Tamasha la Fiesta 2014 akiwa amevaa sare ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kinyume cha sheria.

Tangu msanii huyo afanye hivyo, mjadala umeibuka kwa wengi wao kujiuliza nini maana yake na kama alifanya hivyo kwa kibali maalumu au la, hasa ikizingatiwa ni hivi karibuni Jeshi hilo lilitoa onyo kwa wasanii na wengineo kutotumia mavazi hayo.

Mbali ya Diamond, hata vijana wake nao walishambulia jukwaa wakiwa katika mavazi hayo, akiwemo msanii aliyemshirikisha katika moja ya nyimbo zake, Ney wa Mitego.

Wakati shoo hiyo ikiendelea, baadhi ya mashabiki walianza kumzomea kila alipoimba kabla ya video kubwa ambazo zilikuwa mbele ya jukwaa hilo kuanza kuonyesha picha za mnato na video za mwanamuziki huyo akiwa amevaa mavazi hayo huku akiwa kama askari ‘anayekoki’ risasi katika bastola na baadaye katika bunduki ya kivita.

Kitendo hicho, kilionekana kuwakera zaidi maelfu ya wapenzi na mashabiki wa muziki waliokuwa katika viwanja vya Leaders, huku kila mmoja akiwa na tafsiri yake.

Kwa upande wake Diamond, alitoa taarifa ndefu katika ukurasa wake wa Facebook na Instagram, akiishia kuelezea ni kwa nini alizomewa katika shoo hiyo.

Tanzania Daima ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura juu ya kitendo cha msanii huyo, alisema alikuwa hajui chochote na kuahidi kulifanyia kazi kama atapelekewa taarifa na wasaidizi wake.

Alipotafutwa Kaimu Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Msanja, simu yake iliita bila kupokelewa na alipotafutwa msaidizi wake, alikiri kupata taarifa na kujionea kupitia shoo hiyo, huku akisisitiza bosi wake anaweza kulizungumzia hilo.

Tukio hilo limefanyika ikiwa ni siku chache tu tangu kijana mmoja aliyekuwa amevalia mavazi ya kijeshi maeneo ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam, kuvuliwa na kupewa adhabu ya kuogelea katika dimbwi la maji machafu yaliyotuama.

Chanzo: Tanzania Daima


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU