Facebook Comments Box

Tuesday, October 21, 2014

MREMA AWAFUKUZA MADIWANI WAKE WAWILI KWA KUMUUNGA MKONO MBATIA


Augustin Lyatonga Mrema (MB) wa jimbo la Vunjo.
Joseph Mbatia (MB) ambae ametangaza kugombea jimbo la Vunjo.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, amekunjua  makucha yake yaliyowahi kurarua viongozi wenzake akiwa katika NCCR-Mageuzi na TLP, na sasa amewafukuza madiwani wawili wa chama chake waliounga mkono nia ya Mbunge wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ambaye ametangaza kugombea ubunge wa Vunjo.

Mrema amewavua uanachama wa TLP, Meja Mstaafu Jesse Makundi, aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya Mrema; na Yorolanda Lyimo, Diwani wa Kilema Kaskazini.

Jimbo hilo linawakilishwa na Mrema tangu 2010, na amesema mara kadhaa kwamba hataki kusikia mtu akitaka ubunge katika jimbo lake. Tayari amemlalamikia Mbatia kwa Rais na katika Bunge Maalumu la Katiba.

Kilichowaponza Makundi na Lyimo ni kushiriki harambee iliyoongozwa na Mbatia ya ujenzi wa maabara na mabweni katika shule za Sekondari za Pakula, Kiluani na Mwika, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika harambee hiyo, Makundi alisema anatambua uwezo wa Mbatia na kwamba, kwa sababu hiyo, anamuunga mkono katika azima yake ya kuwa mbunge mwakani.

Alisema kwa kuwa alipokea tochi ya kumulikia wana Vunjo kutoka kwa Mbatia, ameona ni busara kuirudisha kwa yule aliyemkabidhi tochi hiyo.

“Leo nimefikia uamuzi ambao naamini ndio hitaji la wana Vunjo, kwa kuwa Jimbo hili nililipokea kutoka kwa Mbatia na kwa kuwa yeye ndiye aliyenikabidhi hii Tochi, natamka hadharani kuwa Mbatia ndiye chaguo langu, yeye ndiye atakayemulika wana Vunjo,” alisema Makundi.

Yorolanda naye alidai kuwa uamuzi wa kumuunga mkono Mbatia ni wa Mungu.

“Tunamuomba Mungu amuinue aweze kuwa Mbunge wetu. Mimi ni Diwani wa TLP, nina Mbunge wangu, namuheshimu sana (Mrema), lakini namuomba Mungu amteue Mbatia chaguo letu Wana Vunjo. Nafahamu wapo watakaonukuu maneno yangu lakini kama mbaya acha iwe mbaya,” alisema.

Mrema amekerwa na kauli hizo, akawavua uanachama akidai wameonyesha utovu wa nidhamu na wamekiuka katiba ya chama chao kuunga mkono mtia nia wa ubunge wa chama kingine, katika jimbo lake ambalo naye ameshatangaza kuwania nafasi hiyo tena mwakani.

Alikuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Mwanjeni, Kata ya Mwika Kusini.

Hata hivyo, Makundi amesema uamuzi wa Mrema ni batili, kwani mwenyekiti wake huyo hana mamlaka hayo.

Mrema amekuwa analalamikia hatua ya Mbatia kutaka ubunge wa Vunjo, akisema kinachomtia kiburi ni ubunge wa kuteuliwa aliopewa na Rais Jakaya Kikwete.

Analaumu pia vyama vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA na CUF vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambavyo vimetangaza kuweka mgombea mmoja mmoja kila jimbo kwa ushirikiano.

Hata hivyo, UKAWA haijatangaza mgombea wa Vunjo. Licha ya Mbatia, yupo mtia nia mwingine kutoka CHADEMA, John Mrema, ambaye naye ameshatangaza kugombea ubunge huo, akisubiri uamuzi wa mwisho wa UKAWA.

Lakini Mrema amekuwa anamshambulia Mbatia kwa kuwa ndiye amekuwa anafanya mikutano ya mara kwa mara.

“Siko tayari kujibizana na mtu. Kuna kazi kubwa mbele yetu. Tuelekeze nguvu zetu kuwatumikia Wana Vunjo. Mkutano wa Septemba ndio unaomtesa. Nyinyi ni mashahidi. Tangu Septemba 6, sijafanya mkutano wowote. Kulalamika kwake ni sawa na kulalamikia kivuli. Kivuli chake kinamuhukumu. Mimi siko tayari kumjibu,” alisema Mbatia.


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU