Facebook Comments Box

Thursday, September 25, 2014

DEREVA TAX NA MWANDISHI WA HABARI WALISAIDIA NYERERE ASIPINDULIWE

SIRI ya mashujaa waliozima jaribio la kutaka kupindua Serikali ya Tanzania chini ya Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1982, imewekwa hadharani kwamba mashujaa hao walikuwa vijana wawili; mmoja dereva wa teksi na mwingine mwandishi wa habari wa gazeti la Serikali la Daily News.

Akitoboa siri hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani, aliyekuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Balozi Augustine Mahiga, alisema kama si vijana hao, huenda mapinduzi yangefanyika na yangefanikiwa, amani ya Tanzania leo isingekuwepo.

Akisimulia ilivyokuwa, Balozi Mahiga ambaye alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa akiwa kijana wa miaka 30, alisema kuna kijana wa miaka 23 aliyekuwa dereva wa teksi (bila kumtaja jina), ambaye alipata taarifa hizo ambazo Serikali haikuwa nazo.

Baada ya kupata taarifa hizo, Balozi Mahiga alisema kijana huyo alimweleza mwandishi wa
habari wa Daily News (bila kumtaja jina), ambaye naye alikuwa kijana mdogo wa miaka 27, ambaye alipeleka taarifa hizo kwake.

Kwa mujibu wa Balozi Mahiga, alipopata taarifa hizo, aliamua kufanya uchunguzi na kubaini kama kweli kulikuwa na mpango wa kutaka kupindua Serikali, ambao waliuzima kwa kukamata washukiwa ambao walipelekwa mahakamani na kufungwa.

Watu hao ambao alisema walisamehewa wakati wa uongozi wa Awamu ya Pili, sasa wapo huru lakini mpango wao kama ungefanikiwa, huenda amani iliyopo sasa isingekuwepo kwa kuwa kuipoteza ni rahisi kuliko kuirejesha.

“Rasilimali kubwa ya amani ni vijana kwa kuwa kama si wale vijana kutoa taarifa, mapinduzi yangetokea na amani iliyopo sasa isingetokea…amani ikipotea ni shida kuirejesha.

“Msiombe kutokee vita…mimi nimeona watu wanaoishi katika vita, hawana hata muda wa kula wala kulala, akifa mmoja mwingine anabeba silaha anaendelea,” alisema Balozi Mahiga.
Daily News ni moja ya magazeti yanayochapishwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali ya TSN, mengine yakiwa HABARILEO, HABARILEO Jumapili, Sunday News na SpotiLEO.

HabariLeo: Mwandishi TSN atajwa kuzima uasi


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU