KIKOSI
cha timu ya Young Africans kitashuka dimba la Uwanja wa Taifa siku ya
jumapili kupambana na Wajelajela, Timu ya Jeshi la Magereza,Tanzania
Prisons kutoka jijini Mbeya ikiwa ni mchezo wa pili wa mzunguko wa
kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu wa 2014/2015.
Akiongea
na tovuti rasmi ya klabu leo mara baada ya mazoezi, kocha mkuu wa Young
Africans Mbrazil Marcio Maximo amesema vijana wake wako fiti kuelekea
mchezo huo wa siku ya jumapili huku wakiwa wamejipanga kuhakikisha
wanaondoka na pointi tatu muhimu.
Maximo
amesema baada ya kupoteza mchezo wa awali dhidi ya wakata miwa wa Mtibwa
Sugar, kikosi chake kimekua kikiendelea na mazoezi kila siku katika
uwanja wa shule ya sekondari Loyola huku wakiyafanyia marekebisho makosa
yaliyojitokeza katika mchezo huo wa awali.
Kuhusu
timu ya Tanzania Prisons, Mbrazil Maximo amesema anatambua walishinda
mchezo wa awali dhidi ya Ruvu Shooting hivyo wana morali bado ya
kuendeleza ushindi siku ya jumapili, lakini pia kikosi chake kipo fiti
kusaka pointi tatu muhimu.
Aidha
Maximo amesema habari njema kwa wana Yanga ni kurejea dimbani kwa kiungo
Andrey Coutinho pamoja na mshambuliaji Jerson Tegete ambao wanatarajiwa
kuonekana kwenye mchezo huo na kuhakikisha wanaisaidia timu yao kupata
ushindi.
Wachezaji
watakaoukosa mchezo wa siku ya jumapili ni Oscar Joshua na Hussein Javu
ambao wote ni majeruhi, wakisumbuliwa na maumivu ya nyama za paja, na
jumatatu wanatarajiwa kuanza mazoezi mepesi baada ya kuwa kwenye
matibabu chini ya usimamizi wa daktari wa timu Dr Suphian Juma.
Marcio
Maximo amewaomba wapenzi, washabiki, wanachama na wadau wa soka kwa
ujumla kujitokeza kwa wingi siku ya jumapili katika mechi dhidi ya
Prisons kuja kuwapa sapoti vijana na kuwashangilia muda wote wa mchezo.
Chanzo:shaffihdauda
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog