Facebook Comments Box

Tuesday, August 19, 2014

MIAKA 18 BILA KOMRED A M BABU (1924 - 1996): TAFAKURI JUU YA ATHARI ZA 'UTAJIRISHO WA UTAWALA'

Arrival Cabral, Abdulrahman Babu na Eduardo Mondlane

"Kwa dhahiri Ken Saro-Wiwa alipaswa kuuawa, hiyo ni kwa sababu alishirikiri kutenda kile kinachojulikana katika dunia ya tatu kama 'Dhambi ya Kiuchumi' - Kutishia muunganiko wa Kimaslahi kati ya 'Makampuni ya Kimataifa' na Viongozi Walarushwa wa Nchi za Dunia ya Tatu. Wajumbe wa Genge la Watawala wa Kijeshi wa Nigeria walikuwa Manyang'au kwa kuwa walihakikisha sehemu kubwa ya mapato ya Mafuta ya Taifa hilo yanaelekezwa kwenye kukuza Utajiri wao binafsi, na yeyote ambaye alionekana kupinga mpango huu maalum wa 'Utajirisho wa Watawala' alipaswa kushughulikiwa kwa njia yoyote iwayo, halali ama haramu.

Sehemu kubwa ya Mafuta yaliyopelekea mauaji haya ya kila aliyeonekana ni kikwazo cha 'Utajirisho wa Viongozi' yalitokea katika eneo la Ken Saro-Wiwa la Ogoniland. Kampuni ya Mafuta ya 'Shell Oil' ilikuwa inamiliki asilimia 30 ya Shirika la Mafuta la Nigeria, Mafuta ni chanzo kikuu cha 'Rushwa ya Kutisha' inayozunguka maisha ya Nigeria.

Saro-Wiwa hakuwahi kujaribu kukusanya nguvu ya wafuasi katika ngazi ya Kitaifa. Alizituamanisha harakati zake za kudai maslahi ya kiuchumi yatokanayo na Rasilimali kwa watu wake wa Ogoni tu, eneo ambalo lilikuwa na changamoto tofauti na sehemu nyengine za Nigeria. Nigeria bado haijaweza kuzalisha Kiongozi Mahiri mwenye maono na Karisma ya kuwaunganisha pamoja Mamilioni ya Wanaijeria wote ili wauondoe Utawala wa Rushwa na Kinyang'au. Kwahiyo basi Mafungamano ya 'Utajirisho wa Watawala' kati ya Serikali na Makampuni ya Kimataifa yataendelea kufaidi sehemu kubwa ya Rasilimali za Taifa hilo.

Kuthibitisha hilo (La kuendelea kwa mafungamano ya 'Utajirisho wa Watawala'), siku mbili tu baada ya Kunyongwa kwa Ken Saro-Wiwa pamoja na Wanaharakati wenzake nane wa Ogoni (Saturday Dobee, Nordu Eawo, Daniel Gbooko, Paul Levera, Felix Nuate, Baribor Bera, Barinem Kiobel na John Kpuine), Kampuni ya Mafuta ya Shell Oil ilisaini Mkataba wa Dola Bilioni 2.5 (Zaidi ya Trilioni 4 za Tanzania) kwaajili ya Gesi ya Taifa hilo".

Komredi Abdulrahman Mohamed Lain Babu (1924 - 1996), katika Makala yake 'WHY KEN SARO-WIWA HAD TO HANG?' iliyochapwa na Pacific News Service, San Francisco, Marekani - 1996.

Zaidi ya Miaka 18 iliyopita Makomredi wawili muhimu kwa Mapambano ya 'Ukombozi' wa pili wa Bara la Afrika waliiaga dunia, vifo vyao vikiwa na mafunzo makubwa mno kwa kizazi cha sasa cha Tanzania na Afrika kwa Ujumla, hasa kwa mazingira tuliyonayo ya Unyonywaji wa Rasilimali za nchi za Kiafrika unaofanywa kwa ushirikiano kati ya Watawala Mafisadi wanaoziongoza nchi zetu na Makampuni ya Kibepari ya Kimataifa yanayoletwa kwa wimbo wa 'Uwekezaji' usiowanufaisha wananchi wanyonge.

Makomredi hao ni Ndugu Kenule "Ken" Beeson Saro-Wiwa - Mwandishi, Mtayarishaji wa Vipindi vya Televisheni na Mwanaharakati wa Mazingira, na Rais wa Vuguvugu la Uhai wa watu wa Ogoni, MOSOP, aliyeuawa Novemba 10, 1995 kwa kunyongwa na Serikali Katili ya Kijeshi ya Dikteta Sani Abacha baada ya kuendesha Kampeni za kutokutumia nguvu kupinga Uharibifu wa Mazingira uliokuwa ukifanywa na Makampuni makubwa ya Mafuta yaliyokuwa yakichimba mafuta katika eneo la Ogoni, Niger Delta, Nigeria.

Mwengine ni Komredi Abdulrahman Mohammed Lain Babu, Kiongozi Mzalendo mwenye kufuata Itikadi ya Ukomunisti wa mrengo wa Kimarxi na mmoja wa waasisi wa Taifa hili. Babu alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kizalendo cha Kizanzibari cha ZNP, Mwanahabari wa Shirika la Utangazaji la China, Mhariri wa Jarida la Kimapinduzi la ZANEWS, Muasisi na Rais wa Chama cha Mrengo wa Kushoto cha Umma Party kilichorikiana na Chama cha ASP kuunda Serikali ya kwanza ya Mapinduzi ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Babu pia alikuwa Waziri wa Mambo ya nje wa SMZ chini ya Rais Karume na Waziri wa Kwanza wa Mipango na Uchumi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Nyerere.

Tarehe 5 mwezi kama huu mwaka 1996 Komredi Babu aliiga dunia jijini London mara baada ya kuumwa kwa muda mfupi, Alizikwa nyumbani kwao Ukutani katika Viunga vya Mji Mkongwe, Unguja Agosti 9, 1996 - Leo ikiwa ni miaka 18 na siku kadhaa tangu Mzalendo huyu atutoke.

Pichani ni Komredi Abdulrahaman Mohammed Babu akiwa pamoja na Komredi Amilcar Cabral (Kushoto), Mhandisi-Kilimo, Mwandishi na Mpigania Uhuru wa Nchi za Guinea-Bissau na Cape Verde na Katibu Mkuu wa Chama cha PAIGC na Komredi Eduardo Mondlane (Kulia), Rais wa Chama cha Ukombozi cha Msumbiji, FRELIMO. Picha husika ilipigwa Oktoba 1965, Jijini Dar es salaam wakati wa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Vyama vya Kupigania Uhuru wa nchi za Afrika zinazotawaliwa na Ureno - CONCP, Mkutano ambao Babu alikuwa Mgeni Rasmi.

Picha ni kwa hisani ya Hifadha ya Watanzania Mashuhuri .

Babu ni
Mchumi Mjamaiya
Komredi Mmarxiya
Mwafrika Mmajumiya
Mzalendo Mtanzaniya
Mwanamapinduzi Mzenjibiya
Ulale Pema Mahliya
Vijanao Twakuombeya


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU