Facebook Comments Box

Sunday, January 5, 2014

YANGA YAWAHENYESHA WAZUNGU


Kocha Msaidizi wa timu ya Yanga Boniface Mkwasa akitoa maelekezo kwenye mazoezi ya timu ya Yanga hivi karibuni  

YANGA imeuanza mwaka 2014 kwa kasi ya aina yake ambapo makocha wazungu wenye hadhi zao wanahenya usiku na mchana wakisubiri simu za viongozi tayari kuitwa kazini kuanza kibarua kipya.
Lakini Abdallah Binkleb ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili wa Wachezaji, ameithibitishia Mwanaspoti kwamba kabla ya Jumatano ijayo lazima watakuwa wamemchagua mzungu mmoja wa maana.
Binkleb alisema: “Wapo wengi sana kila siku wanatuma maombi lakini sisi tunataka kocha mmoja tu wa maana ambaye ni fundi na anayeweza kutufanyia kitu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na analijua soka la Afrika.
“Tumemchukua Mkwasa (Boniface, anayekuwa Kocha Msaidizi) ni kocha wa maana pamoja na Juma Pondamali (Kocha wa Makipa) wanaijua Yanga vilivyo, tuna uhakika kwamba tukishakutana tukipitia orodha ya mwisho na kuchagua wa kutua nchini, tusifanye makosa.”
Hata hivyo kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Yanga hakuwa na idadi kamili ya makocha walioomba kazi hiyo inayoachwa wazi na Ernest Brandts ambaye amepewa notisi.
Bin Kleb alisema hawezi kusema idadi kwa sasa kwa vile wamekuwa wakipokea barua pepe za maombi hayo kila baada ya muda mfupi.
MKWASA AANZA KWA MIKWARA
Boniface Mkwasa ameiangalia timu hiyo na kutamka kuwa wachezaji wake hawana uwezo wa kucheza dakika 90, hivyo ataanza mazoezi ya aina nne kuwandaa kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mkwasa ametoa kauli hiyo mara baada ya mazoezi ya siku ya kwanza kumalizika jana Ijumaa baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuifundisha timu hiyo akirithi mikoba ya Fred Minziro aliyekuwa msaidizi wa Brandts.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkwasa alisema kuwa timu hiyo inahitaji mabadiliko ya haraka katika kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kutokana upungufu aliouona ambao ni;
Moja; Pumzi. Hilo ndilo la kwanza linalohitajika ambalo ameliona kwa wachezaji kushindwa kumudu kucheza dakika 90 jambo ambalo ni baya kwa timu inayojiandaa na michuano ya kimataifa.
Katika kuhakikisha analifanyia kazi hilo, tayari ameuomba uongozi kutafuta uwanja mkubwa kushinda ule wanaoutumia hivi sasa wa Bora uliopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam. Wanahamishia mazoezi yao Uwanja wa Tanganyika Packers ambao una eneo kubwa kwa lengo la kuwaongezea pumzi wachezaji hao.

Pili; Kasi. Ameona timu hiyo inacheza soka la taratibu ambalo yeye halitaki, anataka kuona timu inacheza kwa kasi ili kuwachosha wapinzani wao ndani ya uwanja.
Tatu; Pasi. Nalo ni tatizo kwani anasema wachezaji wanapiga pasi hovyo. Anasema ili timu icheze soka safi, lazima wapige pasi zitakazowafikia wenzao ndani ya uwanja na siyo kuwapelekea adui na kuanza kupata tabu ya kukaba.
Nne; Kumiliki mipira. Hilo nalo ni tatizo ingawa amesema ni karibu kwa timu zote zinazoshiriki ligi, hivyo amepanga kulimaliza tatizo hilo kwa Yanga.
“Ninajua ni ngumu kumaliza matatizo hayo katika muda huu mfupi wakati timu inajiandaa na ligi, lakini ninaamini nitalipunguza, jambo kubwa nahitaji ushirikiano kutoka kwa wachezaji, ninaomba viongozi kuhakikisha wanasimamia nidhamu ya wachezaji, pale wanaomba ruhusa na kupewa basi warudi kwa wakati,” alisema.
MAZOEZI MARA MBILI
Mkwasa amebadilisha muda wa mazoezi ambapo kuanzia keshokutwa Jumatatu yatakuwa yakifanyika jioni tu na kadiri siku zinavyokwenda mazoezi ya timu hiyo yatakuwa yakifanyika mara mbili kwa siku yaani asubuhi na jioni.
Mkwasa alikaa kikao kirefu na wachezaji juzi Alhamisi jioni klabuni na aliiambia Mwanaspoti kuwa kikao hicho kilikuwa kwa ajili ya kuwafahamu wachezaji kabla ya kuanza kazi rasmi jana Ijumaa.
“Lengo langu lilikuwa kufahamiana na kupanga mikakati, mimi si mgeni Yanga, naamini ushirikiano kutoka kwa wachezaji na viongozi utasaidia timu kupata mafanikio kwenye Ligi Kuu na michuano ya kimataifa,” alisema Mkwasa.
Habari za ndani zinasema Yanga itasafiri kwenda nchi mojawapo kati Hispania, Uturuki au Ureno na inadaiwa timu inatakiwa kuondoka kati ya Januari 9 na 10.
Viongozi wanafuatilia maandalizi ya safari hiyo ili ifanyike katika muda huo.  

CHANZO: MWANASPOTI


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU