Facebook Comments Box

Sunday, February 24, 2013

MNYIKA: MH. SHUKURU KAWAMBWA AMEBAKIZA SIKU KUMI TU


KAULI ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kwamba hawezi kujiuzulu, imeamsha hasira ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kimesisitiza kwamba maandamano ya kumng’oa yako pale pale na sasa amebakiza siku kumi tu.

Kauli hiyo ilitolewa  na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika wakati alipotakiwa kueleza msimamo wa chama chao, hasa baada ya kauli ya Waziri Kawambwa  kwamba hawezi kujiuzulu.

Akizungumza na mdau wa Kitongoni Blog, Mnyika ambaye ni Mbunge wa Ubungo, alisema kauli aliyoitoa Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe kwamba anampa siku 14 Waziri Kawambwa ajiuzulu, vinginevyo atang’olewa kwa maandamano bado ipo pale pale.

Alisema majibu ya Waziri Kawambwa yameonesha dharau kwa Watanzania, hasa walalahoi ambao ndio watoto wao wengi wamepata ziro katika mitihani yao ya kidato cha nne.

“CHADEMA tunaendelea kusisitiza kwamba Waziri Kawambwa ang’oke, awajibike, ameshindwa kazi na hili tunamaanisha,” alisisitiza Mnyika.

Alisema CHADEMA inaangalia namna ya kuitisha maandamano hayo kwa kuwashirikisha vijana waliofeli kwani wanaamini wamehujumiwa.

Mnyika aliwataka Watanzania na wengine wenye uchungu na udhaifu wa elimu ya Tanzania, hasa wazazi wajitokeze kwani fedha walizowekeza kwa watoto wao kwa ajili ya elimu, zimeteketea bure.


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU