Facebook Comments Box

Saturday, August 17, 2013

YANGA KUWEKA REKODI LEO IKIIFUNGA AZAM NA KUIPOTEZEA MBALI SIMBA


YANGA SC itaweka rekodi ya kuwa timu iliyotwaa mara nyingi zaidi Ngao ya Jamii, iwapo itaifunga Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam- hivyo kuwapiku wapinzani wao wa jadi, Simba SC. Hadi sasa, vigogo hao wa soka nchini, kila mmoja ametwaa Ngao mara mbili, wakati timu nyingine zaidi ya hizo iliyowahi kutwaa ubao huo ni Mtibwa Sugar ya Morogoro. Yanga SC ndio washindi wa kwanza wa Ngao mwaka 2001 walipoifunga mabao 2-1 Simba SC, enzi hizo Ligi Kuu inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager. 
Baada ya hapo, haikuchezwa tena mechi ya Ngao hadi mwaka 2009 wakati Mtibwa Sugar ilipoilaza 1-0 Yanga SC.
Mwaka 2010 Yanga walirejesha Ngao kwenye himaya yao, baada ya kuwachapa tena wapinzani wa jadi, Simba kwa penalti 3-1 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90.
Simba SC walitwaa mara mbili mfululizo Ngao na kufikia rekodi ya watani, kwanza 2011 walipoifunga 2-0 Yanga na mwaka jana walipotoka nyuma kwa 2-0 na kuilaza Azam 3-2.
Katika mchezo wa leo, Kocha Mholanzi, Ernie Brandts atamkosa mshambuliaji wake Mrisho Khalfan Ngassa ambaye amefungiwa mechi sita na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kamati hiyo baada ya kupitia usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom jana, ilimuidhinisha Ngassa kuchezea Yanga baada ya kukamilisha usajili wake.
Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imebaini kuwa Ngassa alisaini mkataba mwingine Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) ambapo anatakiwa kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30) pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh. milioni 15) ya fedha hizo kwa Simba.
Kamati pia imemfungia mechi sita za mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii), na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.


Kwa sababu hiyo, Simon Msuva anaweza kurejea uwanjani leo katika nafasi ya Ngassa, huku wachezaji wapya wanaotarajiwa kucheza leo Yanga sana ni Hussein Javu.
Kocha Muingereza wa Azam, Stewart John Hall atatakiwa kutorudia makosa mawili makuu aliyoyafanya msimu uliopita hata yakachangia kumkosesha ubingwa.
Alifungwa na Yanga SC 1-0 katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu kwa sababu siku hiyo alimjaribu kiungo Kipre Michael Balou katika beki ya kulia, badala ya kupanga beki halisi.
Akafungwa na Simba SC katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu pia msimu uliopita kwa kosa la kujaribu mfumo ambao wachezaji hawakuwa wamuelewa vyema na hizo ndizo pointi sita zilizowapa Yanga ubingwa.
Burudani inatarajiwa kuwa nzuri katika mchezo leo, kutokana na ukweli kwamba pande zote zina mafundi na wataonyeshana kazi uwanjani.
Upande wa Azam, langoni anaweza kusimama Aishi Manula badala ya Mwadini Ally, kulia Erasto Nyoni, kushoto Waziri Salum na katikati Aggrey Morris na Joackins Atudo. Himid Mao anaweza kuanza katika kiungo cha chini badala ya Balou na juu yake bila shaka atacheza Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Kulia anaweza kucheza Kipre Tchetche, kushoto Khamis Mcha ‘Vialli’ na John Bocco ‘Adebayor’ akaanza katika ushambuliaji na Ibrahim Mwaipopo.
Gaudence Mwaikimba ni mchezaji anayetarajiwa sana kutokea benchi leo kipindi cha pili kuja kujaribu kuisulubu timu yake ya zamani, Yanga SC.
Yanga SC hapana shaka Ally Mustafa ‘Barthez’ ataendelea kusimama langoni, Juma Abdul atacheza kulia badala ya Mbuyu Twite, kushoto David Luhende badala ya Oscar Joshua, katikati kama kawaida Kevin Yondan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’- Athumani Iddi ‘Chuji’ ataanza badala ya majeruhi Frank Domayo na juu yake anaweza kucheza Haruna Niyonzima.
Kwa kuwa washambuliai ni wengi kwa sasa Yanga, kiungo kulia na kushoto wanaweza kuenea wao tu. Kulia anaweza kucheza Simon Msuva na kushoto Hamisi Kiiza, wakati washambuliaji wanaweza kuanza Didier Kavumbangu na Jerry Tegete, Javu akianzia benchi. 

MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
Mwaka Mshindi            Matokeo     
2001: Yanga SC 2-1 Simba
2009: Mtibwa Sugar 1-0 Yanga SC
2010: Yanga SC 0-0 Simba (3-1penalti)
2011: Simba SC   2-0 Yanga
2012: Simba SC 3-2 Azam FC

CHANZO: BIN ZUBEIRY 

Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU