Ili kukabiliana na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM dhidi ya wagombea, Wanachama na viongozi wa CHADEMA, Kamati Kuu imeagiza kwamba kitengo cha ulinzi cha Chama “Red Brigade”kiimarishwe zaidi kwa kuhakikisha kuwa vijana wote wa Red Brigade Nchi nzima wanapewa mafunzo maalum ya UKAKAMAVU yatakayoandaliwa katika Makambi maalum katika mikoa yote.
TAARIFA
KWA UMMA KUHUSU MAAMUZI YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA KILICHOFANYIKA
TAREHE 06-07/07/2013 KATIKA HOTEL YA BLUE PEARL, DAR ES SALAAM.
Kamati
kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo ilikutana katika Kikao cha
dharura kuanzia tarehe 06-07/07/2013 katika Hotel ya Blue Pearl Dar es
salaam kujadili pamoja na mambo mengine Rasimu ya Katiba mpya na hali ya
Siasa nchini.
Kamati kuu imejadili na kuyatolea maamuzi mambo mbalimbali kama ifuatavyo:
1:0. Hali ya Siasa Nchini.
Kamati kuu imepokea taarifa ya hali ya siasa nchini na kuzingatia mambo yafuatayo:
a) Shambulio la Bomu Arusha.
Kamati Kuu imesikitishwa na kulaani kwa nguvu zote tukio la Bomu Arusha
lililosababisha watu wanne kuuwawa na zaidi ya watu 70 wengine
kujeruhiwa vibaya.
Kamati Kuu imeridhika kwamba shambulio hilo
lililenga kuwaua viongozi wakuu wa CHADEMA akiwamo Mwenyekiti wa Taifa
Mheshimiwa Freeman A. Mbowe na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini na Mjumbe
wa Kamati Kuu, Mheshimiwa Godbless J. Lema na viongozi na wanachama
wengine wa CHADEMA waliohudhuria Mkutano wa kufunga kampeni za udiwani
katika Jiji la Arusha pamoja na kuvuruga Uchaguzi huo na kuinyima
CHADEMA ushindi mkubwa;
Kamati Kuu imeridhika kwamba ushahidi
uliopo wa vielelezo na wa mashuhuda wa shambulio unaonyesha ushiriki wa
moja kwa moja wa Jeshi la Polisi katika shambulio hilo;
Kamati
Kuu imefadhaishwa na kauli ya Serikali bungeni iliyolenga kulikosha
Jeshi la Polisi kwa kuhusika kwake na shambulio hilo dhidi ya CHADEMA na
wananchi wa Jiji la Arusha na kuilaumu CHADEMA wakati CHADEMA ndio
mhanga wa shambulio hilo;
Kamati Kuu imeshangazwa na kitendo
cha Serikali kupuuza maafa yaliyowafika wananchi wa Arusha kwa kushindwa
kushiriki katika mazishi ya wahanga wa mauaji ya Soweto na
kuwashambulia kwa mabomu ya machozi, vipigo na maji ya sumu waombolezaji
waliokusanyika kuwaaga marehemu waliouawa kwenye shambulio;
Kamati Kuu imesikitishwa na Rais Kikwete kuendelea kukaa kimya juu ya
shambulio la Arusha na kushindwa kwake kuunda Tume huru ya Kimahakama
kuchunguza kwa uwazi shambulio hilo. Aidha, Kamati Kuu inaamini kwamba
ukimya huu wa Rais Kikwete na kushindwa kwake hata kuwatembelea wafiwa
na wahanga wengine wa shambulio hilo ni ushahidi mwingine wa kuhusika
kwa vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali katika kupanga na
kutekeleza shambulio la Arusha;
Kamati Kuu imefadhaishwa na
kitendo cha Bunge la Jamhuri ya Muungano kuendelea na vikao vya Bunge
kama kawaida; kukataa kutoa mchango wowote kwa wahanga na kushindwa
kupeleka ujumbe wa Bunge kuwatembelea na kuwafariji wahanga na
waathirika wa shambulio kinyume na utaratibu uliozoeleka wa Bunge
kutambua na kushiriki katika majanga na misiba ya aina hii.
Kamati
Kuu inautaka uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano uwaeleze
Watanzania kama maafa ya shambulio la Arusha yalikuwa na tofauti yoyote
na maafa ya shambulio la bomu la Olasiti, au na maafa ya mabomu ya Gongo
la Mboto, ajali ya MV Skargit au maafa mengine yaliyosababisha Bunge la
Jamhuri kuahirisha shughuli zake, kutoa michango kwa waathirika pamoja
na kupeleka ujumbe wa Bunge kuwafariji wafiwa na wahanga wa matukio
hayo;
Kutokana na maelezo hayo hapo juu Kamati kuu imeazimia kuwa:
•
Iwapo Rais ataendeleza msimamo wa kutokuunda tume huru ya kimahakama,
Ushahidi uliopo juu ya tukio la kurushwa Bomu Arusha utawekwa wazi muda
utakapofika kwa wananchi wa Tanzania; vyama na mashirika ya kiraia ya
haki za binadamu hapa nchini na ya nje ya nchi; ofisi za kibalozi za
mataifa rafiki na Tanzania pamoja na jumuiya ya kimataifa ili
yaishinikize Serikali kuunda Tume huru ya Kimahakama kuchunguza
shambulio hilo na matukio mengine ya mauaji yenye sura ya kisiasa ambayo
yamehusishwa na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama vya
Serikali au vya Chama cha Mapinduzi;
2:0. Hali ya Wananchi wa Mtwara.
Kamati
kuu imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa juu ya unyanyasaji,
utesaji, ubakaji na uonevu wanaofanyiwa wananchi wa Mtwara hivi sasa na
vyombo vya dola huku serikali ikikaa kimya juu ya jambo hili bila
kukemea. Kamati kuu imejadili kwa kina namna wananchi wa Mtwara
wanavyofanyiwa na vyombo vya dola na kufikia maazimio yafuatayo;
Vyombo vya dola vitimize wajibu wake wa kulinda amani na mali ya raia
na siyo kuwatesa na kuwapiga wananchi kwa kuwasababishia vifo kinyume na
Haki za Binadamu.
Serikali iwasikilize wananchi wa Mtwara na
siyo kutumia ubabe, unyanyasaji, uonevu na mateso kama mbinu za
kuhalalisha kukubalika kwake kwa wananchi.
Rais Kikwete
alitangazie taifa “hali ya hatari” kwa mkoa wa Mtwara kama anaona kuwa
Mtwara ni hatari kwa kiasi hicho cha kulitumia JWTZ kuzunguka mitaani na
silaha za kijeshi ili taifa liweze kujua,Aidha kama jeshi la polisi
limeshindwa kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria atangaze
kulivunja jeshi hilo mara moja.
Serikali iunde tume huru ya
kuchunguza matukio ya mauaji,ubakaji,utesaji na ukiukwaji wa haki za
binadamu yaliyofanywa na vyombo vya dola na waathirika wote waweze
kufidiwa kwa mujibu wa sheria.
3:0. Kauli ya Waziri Mkuu.
Kamati
Kuu imejadili kwa kina kauli ya Waziri Mkuu Bungeni kwamba ni sahihi
kwa Jeshi la Polisi nchini kuwapiga Wananchi wote wanaotumia haki zao za
Kikatiba kupinga sera au maamuzi ya Serikali. Kamati Kuu imeazimia
kuwa:
Kauli ya Waziri Mkuu imekiuka Katiba na sheria za nchi
yetu zinazokataza Jeshi la Polisi kutumia nguvu dhidi ya raia wasiokuwa
na silaha na ambao wanatumia haki zao za kikatiba kufanya maandamano;
Kamati Kuu inaamini kwamba kauli ya Waziri Mkuu inatoa Baraka kwa Jeshi
la Polisi kuendeleza vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya wananchi
ambayo yamelifanya Jeshi la Polisi la Tanzania kutangazwa kuwa moja ya
majeshi katili ya polisi katika Afrika Mashariki;
Kamati Kuu
inaungana na wananchi, taasisi na mashirika ya kitaifa na kimataifa
ambayo yamelaani vikali kauli hiyo ya Waziri Mkuu na inawataka wananchi,
taasisi na mashirika hayo kuendelea kumlaani vikali Waziri Mkuu kwa
kauli hiyo;
Kamati Kuu inaamini kwamba Waziri Mkuu amepoteza
sifa za kuendelea kuwa Waziri Mkuu na inaungana na wananchi na taasisi
ambazo zimedai Waziri Mkuu awajibike au awajibishwe kutokana na kauli
yake hiyo. Aidha, Kamati Kuu inawaelekeza Wabunge wote wa CHADEMA
washirikiane na Wabunge wengine wote wenye mapenzi mema na nchi hii na
ambao wanaamini katika utawala wa sheria waanzishe mchakato wa kumpigia
kura ya kutokuwa na Imani Waziri Mkuu kupitia Bunge;
Kamati Kuu
imewataka Jeshi la Polisi kama sehemu ya jamii ya watanzania kupuuza
kauli ya Waziri Mkuu katika utekelezaji wa kazi zao kwa kuwa kauli hiyo
ni ya uvunjifu wa Katiba na Sheria na inachochea uvunjifu wa amani.
4:0. Uchaguzi wa Madiwani.
Kamati Kuu imepokea taarifa kuhusu ushiriki wa CHADEMA katika Uchaguzi wa Madiwani uliofanyika tarehe 16/06/2013 katika kata 22.
Kamati Kuu imeipongeza Sekretarieti na uongozi wa Kanda mbalimbali za
CHADEMA kwa maandalizi mazuri katika Uchagzuzi huo uliosababisha CHADEMA
kuwapokonya CCM ushindi katika kata 4 ilizokuwa imeshinda katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Kamati Kuu imewapongeza wananchi kwa
kuipatia CHADEMA kura asilimia (47.7%) dhidi ya CCM (49%) na (3.3%) za
CUF.
Kamati kuu imesikitishwa na vitendo vya fujo
walivyofanyiwa viongozi, wagombea pamoja na Wanachama mbalimbali katika
sehemu mbalimbali palipo fanyika Uchaguzi. Kamati Kuu imesikitshwa na
kulaani vitendo hivyo vikiwemo vya watu kukatwa mapanga , kuchomwa visu
na kubakwa kwa akina Mama na vijana wahuni walioandaliwa na Chama cha
Mapinduzi.
Kamati Kuu imelaani vitendo hivyo vya kinyama vilivyofanywa mbele ya jeshi la polisi na Wakuu wa Wilaya.
Ili kukabiliana na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM
dhidi ya wagombea, Wanachama na viongozi wa CHADEMA, Kamati Kuu imeagiza
kwamba kitengo cha ulinzi cha Chama “Red Brigade” kiimarishwe zaidi kwa
kuhakikisha kuwa vijana wote wa Red Brigade Nchi nzima wanapewa mafunzo
maalum ya UKAKAMAVU yatakayoandaliwa katika Makambi maalum katika mikoa
yote.
Kamati Kuu imejadili maandalizi ya Uchaguzi wa madiwani
katika kata nne (4) katika Jiji la Arusha. Kamati Kuu imepokea kwa
masikitiko taarifa juu mipango inayofanywa na jeshi la polisi kwa
kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo na viongozi
wengine wa CCM mkoani Arusha katika kuhujumu zoezi la Uchaguzi kwa
kuwatisha wapiga kura kwa kutumia polisi na vijana wa Green Guard siku
ya uchaguzi.
Kamati Kuu inamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP)
kuchukua hatua stahiki kuzuia harakati za polisi na CCM za kuvuruga
Uchaguzi na kutaka kujipatia ushindi kwa njia za hila. Aidha Kamati kuu
imelitaka jeshi la polisi kuheshimu maadili ya uchaguzi yaliyosainiwa na
Serikali, Tume ya uchaguzi na vyama vya siasa.
Kamati Kuu
imesikitishwa na Tume ya Uchaguzi kushindwa kuwazuia CCM kuendelea na
kampeni za Uchaguzi huku wakiwa wamezuia kampeni hizo kwa vyama vingine.
Kamati Kuu imeendelea kuwapa pole wananchi wa Arusha kwa matukio mabaya
wanaofanyiwa na serikali ya CCM mkoani humo, na imewapongeza kwa
kusimama kidete katika kulinda haki na ukweli.
Kamati Kuu
imewaomba wananchi wa Arusha wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura
tarehe 14 Julai 2013, na imewataka wabunge wote washiriki katika
kusimamia zoezi la upigaji kura na uhesabuji kura siku ya Uchaguzi na
wananchi wajitokeze kwa wingi kulinda kura bila hofu.
5:0. Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kamati
Kuu imejadili kwa kina sana maudhui yaliyomo katika Rasimu ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba;
• Kamati Kuu imetambua kazi kubwa iliyofanywa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba katika kukusanya na kuchambua maoni ya wananchi na
kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya;
• Hata hivyo, Kamati Kuu imetambua
na kuainisha mapendekezo mengine ya msingi ambayo yanastahili
kuboreshwa zaidi katika Rasimu hiyo;
• Msimamo na maazimio ya
Kamati Kuu juu ya Rasimu ya Katiba Mpya yameainishwa na kuchapishwa
katika kijitabu maalumu ambacho kitazinduliwa katika Mkutano wa hadhara
utakaofanyika siku, tarehe na mahali patakapo tangazwa hapo baadaye.
Imetolewa na:
……………………….
Freeman A. Mbowe, (MP)
Mwenyekiti Taifa
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog