Tarehe 29 Machi 2013, mnamo saa mbili na nusu asubuhi jengo linalojengwa kwenye kiwanja namba 2032/73 Mtaa wa Indira Gandhi lilianguka kutokana na sababu ambazo bado hazijathibitishwa kitaalam na mamlaka husika. Shirika la Nyumba la Taifa linasikitika sana kutokana na kuanguka kwa jengo hilo pamoja na maafa yaliyotokana na tukio hilo la kusikitisha. Pia Shirika linatoa pole kwa wale wote waliofikwa na msiba uliotokana na ajali hii.
Mradi huu wa ubia kati ya NHC na M/s Ladha Construction Limited ya Jijini Dar Es Salaam ulianza kutekelezwa tarehe 4 Februari 2008 ambapo Shirika la Nyumba litakuwa na hisa asilimia 25 na mbia ana asilimia 75 mara baada ya mradi kukamilika. Kwa mujibu wa sera ya ubia iliyoanza kutumika mwaka 1993 na kuhuishwa mwaka 1995 na 2005, Shirika la Nyumba la Taifa lilikuwa likitoa ardhi ambayo ilikuwa ikihesabika kama asilimia 25 ya mtaji wake kwenye jengo husika na mbia alikuwa akipata asilimia 75.
Kwa mujibu wa mkataba huo mbia mwendelezaji M/s Ladha Contruction Limited kama walivyo wabia wengine, anapaswa kabla ya kuanza ujenzi kupata vibali kutoka kwenye mamlaka husika na kuwa na wataalam wa ujenzi na washauri waliokubalika na kuthibitishwa na mamlaka husika. Aidha, mbia huyu akishapata wataalam hao ndiye anayehusika kuingia nao mikataba ya kazi ya kujenga na kusimamia ubora wa jengo husika kwa mujibu wa sheria. Katika mradi huu mbia mwendelezaji aliajiri wataalamu wote waliosajiliwa na Mamlaka husika ambazo ni CRB, ERB, AQRB na Mansipaa husika na mamlaka nyinginezo. Kwa kuwa ujenzi ulikuwa bado haujakamilika, Shirika lilikuwa bado halijapata asilimia 25 ya umiliki wake.
Pia tunapenda kuufahamisha Umma kuwa, Shirika la Nyumba la Taifa, lilisimamisha utoaji wa miradi mipya ya ubia mwaka 2010 ili kuweza kutathimini mafanikio na changamoto za utekelezaji wa miradi ya ubia na hivyo kuwezesha kutengeneza sera mpya. Kama sehemu ya zoezi hilo, shirika pia lilifuta jumla ya mikataba 64 ambayo ilikuwa imesainiwa lakini haijaanza ujenzi.
Katika sera mpya ambayo utekelezaji wake utaanza hivi karibuni Shirika litahusika moja kwa moja katika kuteuwa mjenzi mtaalam (contractor), msimamizi mtaalam wa mradi husika (consultant) na kusimamia kikamilifu shughuli zote za ujenzi.
Tunapenda kuufahamisha umma kuwa taarifa zaidi zitatolewa baada ya vyombo husika kuwasiliana na mjenzi wa mradi huu. Aidha, taarifa zinaweza kupatikana moja kwa moja kutoka M/s Ladha Construction Limited ambaye ndiye mbia mwendelezaji aliyekuwa anasimamia ujenzi huu.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO NA HUDUMA KWA JAMII S.L.P. 2977 Simu: 2851590 DAR ES SALAAM
Telegrams : "NYUMBA" TANZANIA
Fax 2851442
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog