Benson Mollel wa kwanza kushoto akiwa katika moja ya shughuli za UVCCM mkoani Arusha |
MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM) taifa, kupitia Mkoa wa Arusha, Benson Mollel (26) amekutwa
amefariki dunia ndani ya Hoteli ya Lush Garden Business, iliyopo Mtaa
wa Jacaranda katikati ya Jiji la Arusha.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema Mollel alikutwa
akiwa amekufa jana mchana na kwamba tukio hilo limezua hofu kwa wakazi
wa Jiji la Arusha, huku wakijiuliza chanzo cha kifo chake.
Kifo cha mwanasiasa huyo mchanga ambaye pia
alikuwa ni mfanyabiashara wa madini mkoani hapa, kimezusha maswali mengi
wakati wengine wakihusisha tukio hilo na masuala ya kisiasa na upande
mwingine wakidai ni masuala la kibiashara.
Hisia hizo zinatokana na ukweli kwamba Arusha ni
jiji lenye hekaheka za kisiasa hasa ndani ya CCM ambapo Mollel alikuwa
mmoja wa vinara wake.
Polisi waliwasili hotelini hapo saa 8.00 mchana na
kuupakia mwili wa marehemu kwenye gari na kisha kuupeleka Hospitali ya
Mount Meru kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya wa Arusha (OCD), Gilles
Muruta akizungumza katika eneo la tukio alisema: “Tunachunguza tukio
hili ambalo ni la ghafla.”
Akizungumzia kifo hicho, Katibu Mkuu wa UVCCM,
Martin Shigela alisema: "Tumepokea kwa masikitiko kifo cha Mollel
japokuwa sifahamu nini hasa kimejiri huko."
"Kuna rafiki yake alinipigia simu kuniarifu kuhusu
kifo hicho na nikawaambia kama UVCCM Taifa tupate maelezo kamili na
tujue nini cha kufanya. Iwapo familia itakuwa na mipango yoyote
watutaarifu," alisema Shigela.
Baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wa madini
mkoani Arusha walionekana nje ya hoteli hiyo baada ya taarifa za kifo
hicho kusambaa na wengine walishindwa kujizuia kisha kuangua vilio.
Miongoni mwao ni kada wa Chadema, James ole Millya
na diwani wa CCM Kata ya Mlangarini, Mathias Manga. Katibu Mwenezi wa
CCM wa Mkoa wa Arusha, Isaack Kadogoo ambaye pia alifika eneo hilo
alisema kwamba wamepokea taarifa za tukio hilo kwa mshtuko mkubwa.
Uongozi wa hoteli hiyo haukuwa tayari kulizungumzia kwa madai kwamba limefikishwa katika vyombo vya usalama.
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani
ya hoteli hiyo vilidai marehemu aliwasili usiku, juzi Jumamosi hotelini
hapo akiongozana na mwanamke aliyetambulika kwa jina la Nancy na
kuchukua chumba namba 208.
SOURSE: MWANANCHI
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog