JESHI la Polisi mkoani Lindi,limezuia kufanyika kwa maandamano ya
kuunga mkono majirani zao wa Mtwara,kupinga kusafirishwa kwa njia ya
bomba la gesi asilia,kutoka mkoani humo kupelekwa Jijini Dar es salaam
kwa ajili ya kufufua umeme utokanao kwa rasilimali hiyo.
Kwa mujibu wa barua kutoka Ofisi ya Jeshi hilo,ambayo inaonyesha
kukosewa kwa mwezi na mwaka,yenye kumbukumbu LND/271/VOL.1/17 ya
Decemba 17/2012,na mwandishi wa habari hizi kupata nakala yake,na
kusainiwa na Kamanda George Mwakajinga,imepelekwa kwa vyama vinne vya
siasa.
Vyama vilivyopelekewa barua za zuio la maandamano hayo ni pamoja na
Chama cha mapinduzi (CCM), (CUF), CHADEMA na NCCR-MAGEUZI.
Kwa mujibu wa barua hiyo,inawataka viongozi wa vyama hivyo vinne vya
siasa kuchukua hatua mapema ya kuwasihi na kuwaelimisha wanachama wao
kwanza, kwa ujumbe wa gesi kama ulivyotolewa na wananchi wa mkoa wa
Mtwara.
“Napenda kuchukuwa nafasi hii kuwaandikia kuwakumbusha tarehe kuwa 04/01/2013,siku ya Ijumaa mkuu wa mkoa wa Lindi,Ludovick Mwananzila
alipata fursa ya kuwaalika wadau wote,wazee wa mji wa Lindi,viongozi
wa madhehebu ya dini na vyama vya siasa,alizungumzia na
kufafanua mwelekeo na msimamo wa Serikali katika suala la gesi na jinsi
mkoa unavyochangia pato la Taifa kwa gesi ya Songosongo na jinsi
anavyojiandaa kwa ugunduzi mpya kwenye kina kirefu cha bahari ya Hindi
wilaya ya Kilwa”Imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Aidha,barua hiyo imeeleza kwamba Jeshi hilo la Polisi,lisingependa
kukwaruzana na jamii katika maandamano hayo ya barabarani kwa hoja za
kisera za kiuchumi ambazo ni za ki-Taifa, zinazoweza kuzungumzika
katika mifumo mingine ya kiutawala kama vile katika vikao vya Bunge.
“Tunaomba ushirikiano na ushirikishwaji wa Jamii katika utii wa
sheria bila Shuruti katika kudumisha amani na utulivu ndani ya mkoa wa
Lindi”Imeeleza barua hiyo.
Baadhi ya viongozi na wanachama wa vyama vilivyopelekewa barua
hizo,wamemuomba kamanda huyo wa Polisi mkoani hapa,George
Mwakajinga,kutoupotosha umma juu kauli yake,kwani maandamano
yanayotarajiwa kufanywa ni kuunga mkono jirani zao wa Mtwara katika
kutetea gesi iliyogunduliwa huko kutopelekwa nje ya mkoa huo kwa njia
ya Bomba,na sio kupinga kauli ya mkuu wa mkoa wa Lindi.
“Sisi tunawaunga mkono jirani zetu wa Mtwara, juu ya kuondolewa gesi
kupelekwa Dar es salaam,kwani huo ni uonevu na unyang’anyi mkubwa
unaofanywa na hawa viongozi wetu waliopo madarakani”
“Kwani sisi watu wa mikoa ya kusini tumeikosea nini hii Serikali,kama
ni gesi tumewapa kutoka Songosongo Kilwa,licha ya wenzetu kuizuia kwa
njia ya kiustaarabu,yaani kuifikisha mahakamani,lakini
tuliwaachia na Kilwa kukosa kiwanda cha mbolea kama ilivyokuwa
imepangwa,sasa leo wanataka kuihamisha ya Mtwara tuendelee kuwa
masikini”Walisema viongozi na wanachama hao.Januari 04 mwaka huu,viongozi wa Chama cha wananchi (CUF) mkoani
Lindi, wakiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja vya
Sera,Manispaa ya Lindi,Walitoa wito kwa wananchi kushiriki katika
maandamano yatakayofanyika Februari 23 mwaka huu,ili kuwaunga mkono
jirani zao wa mkoa wa Mtwara,kupinga uamuzi wa Serikali kusafirisha
gesi kwa njia ya bomba na kuipeleka Jijini Dar es salaam kwa ajili
ya kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme.
Mambo mengine yaliyotajwa na viongozi hao ni pamoja na kuwepo kwa
mfumo wa ununuzi wa mazao kwa utaratibu wa mfumo wa Stakabadhi
ghalani, kwa maelezo kwamba umekuwa hauwasaidii walengwa (wakulima) na
badala yake umekuwa ukiwasaidia wachache
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog