Facebook Comments Box

Saturday, January 12, 2013

KAMA TANZANIA HAINA DINI NI HUKO BARA SIYO ZANZIBAR- PROF ABDUL SHERIF

Prof Abdul Sherif

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetahadharishwa isilete hoja ya nchi kutokuwa na dini katika katiba ya nchi kwani Wazanzibari hawatakubali kupokonywa haki zao za kidini kama Mahakama ya Kadhi.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar, Professa Abdul Sherif muda mfupi baada ya kutoka kwenye meza ya utoaji wa maoni mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaliofanyika juzi katika ukumbi wa Eacrotanal Mjini Unguja ambapo aliwasilisha maoni ya Baraza la Katiba Zanzibar.

Professa Sherif amesema mabadiliko ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanayofanyika yazingatia suala la dini kwani katiba ya Tanzania inazungumzia serikali haina dini lakini katiba ya Zanzibar haina kifungu hicho na hivyo suala la dini waachiwe watu wenyewe badala ya kuingizwa katika katiba.

Alisema huenda kuingizwa kifungu hicho kunaweza kuleta matatizo hasa kwa kuzingatia Zanzibar ina asilimia 99 ya waislamu na hivyo hawawezi kukubali kufutwa mahakama yao ya kadhi ambayo wameikuta tokea miaka kadhaa ya wazazi wao.

“Kuwepo kwa kifungu cha katiba kuhusu dini kunaweza kuchochea suala hata la mahakama ya kadhi nadhani wazanzibari hawatakubali kuambiwa mahakama ya kadhi ifutwe sasa sisi tunashauri suala hili lisiingizwe katiba katiba” alishauri.

Professa Sherif ambaye ni bingwa wa historia na ameshawahi kupokea tunzo mbali mbali duniani kutokana na mchango wake mkubwa katika kuandika vitabu kadhaa vya historia amesema wazanzibari wana haki ya kuwa na mahakama ya kadhi kutokana na kuwa idadi yao ni kubwa na hivyo wana haki ya kujiamulia mfumo wa wanaoutaka katika kuendesha nchi yao.

Aidha alisema miaka kadhaa wazanzibari wameishi bila ya kutokea ugomvi wa aina yoyote kuhusiana na dini na ndio maana hata wakati wa utawala wa Uingereza kuna makanisa makubwa yalijengwa Zanzibar ambapo wakati huo wakristo walikuwa wachache mno lakini kutokana na kuheshimu dini nyengine utawala wa Sultan ambaye ni muislamu alithubutu kutoa kibali cha kujengwa makanisa.

“Miaka yote wazanzibari hawajawahi kugombana kwa habari ya dini wanagombana kwa mambo mengine lakini sio dini wamekuwa na uvumilivu mkubwa na kushirikiana na ndio maana kuna mahekalu, misikini na makanisa lakini watu wake hawagombani” alisema Professa Sherif.

Akizungumzia masuala mengine kwa ujumla alisema bunge la Tanzania halikuwa na haki wala mamlaka ya kupunguza au kuongeza mambo ya muungano ambao yalikubaliwa katika hati ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar zilipoungana ambapo awali yalikuwa mambo 11 tu.

Professa Abdul Sherif amesema mambo yaliongezwa yamefanyika kinyume cha sheria na hivyo yalioongezwa yote yamekuwa batili kwa mujibu wa sheria kwa kuwa bunge halikuwa na madaraka hayo.

Katika hatua nyengine Chama Cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kimependekeza katika katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwepo kwa mfumo wa serikali pamoja na kuwepo kwa fursa ya mgombea binafsi kuwania uongozi wa nchi badala ya mfumo uliopo sasa.

Akiwasilisha maoni yake mbele ya tume ya mabadiliko ya katiba jana, Katibu wa chama hicho, Mussa Kombo alisema mfumo wa kuwepo kwa serikali tatu ndio utakaofaa kwa sasa pamoja na kupendekeza kuwepo kwa mgombea binafsi katika kuwania nafasi za urais nchini.

Alisema mfumo wa serikali tatu utasaidia kuondosha manungunuko na malalamiko yasiokwisha kati ya pande mbili hizo ambapo kwa miaka kadhaa sasa serikali imeshindwa kutafanyia kazi mambo ya kero za muungano.

“Sisi kama ZLS tunaona mfumo wa serikali tatu ndio unaofaa kwa sasa kuingizwa katika katiba mpya kuwepo na serikali ya Zanzibar na kuwepo na serikali nyengine jina lolote litakaloitwa na pia kuwepo na serikali ya muungano ambayo hiyo itakuwa ni ndogo itashughulikia masuala ya muungano tu” alisema Mussa nje ya mkutano wa utoaji wa maoni yaliofanyika ukumbi wa Eacrotanal Mjini Unguja.

Kombo alisema katiba mpya ianishe waziwazi hizo serikali tatu na mamlaka zake ili kusiwepo na utata kwani mfumo uliopo sasa haujaelezwa kikamilifu katika katiba na hivyo kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka pande mbili zilizoungana.

Aidha alisema ZLS imeona kuwepo na mgombea binafsi atakayewania nafasi ya urais kwani imani yao ni kwamba anaweza kupatikana kiongozi mzuri atakayetokana nje ya chama cha siasa.

“ZLS tunaamini tunaweza kupata kiongozi nje ya chama” alisema Kombo na kuongeza kwamba mambo mengine waliopendekeza na ZLS kuingizwa katika katiba mpya ni suala la uraia, ulinzi, sarafu, na uhamiaji ambayo yote yawe ni ya muungano na mambo mengine yaliobaki yasiwe na muungano.

Kombo alisema mambo ambayo sio ya muungano yanapaswa kuamuliwa kwa pamoja na kwa ridhaa ya pande mbili zilizoungana huku kila serikali iwe na chombo chake cha maamuzi ambapo walipendekeza kuwepo na bunge la Zanzibar, bunge la bara au vyovyotelitakavyotwa na kuwepo na bunge la pamoja.

Alisema tabia ya serikali ya upande mmoja kujiamulia na serikali ya pili kushindwa kutoa maamuzi haipendezi na hivyo wameshauri jambo lolote liamuliwe kwa pande mbili tena kwa makubaliano.

Akizungumzia suala la haki za binaadamu kuingizwa katika katiba Professa Chris Peter Maina wa Kituo Cha Huduma za Sheria Zanzibar, alisema haki zote za binaadamu ziwekwe katika katiba ikiwa pamoja na haki ya kupata elimu na afya iwe ni ya lazima pamoja na ile haki ya msingi ya kuishi.

Professa Maina alisema katika mpya ianishe haki ya kutumikishwa kwani kumekuwepo na tatizo kubwa la watu kuchukuliwa na kupelekwa nje ya nchi kutumikishwa na hivyo katiba iseme wazi kwamba haki hiyo ni ya msingi, ikiwa pamoja na haki ya kuandamana

Pia alipendekeza katika katiba mpya kuwepo na uhuru wa vyombo vya habari badala ya katiba ya sasa inavyosema uhuru wa kupata habari peke yake.

Mambo mengine aliyotaka yawemo katika katiba ni uhuru wa fikra na maoni iwe ni pake yake na uhuru wa dini na imani huku akipendekeza haki ya kupiga kura kwa watu waliofungwa au waliopo rumande na kulindwa kwa mali iliyopatikana kihalali.

Maoni mengine ya kituo hicho cha huduma za sheria ni pamoja na kuwepo wimbo wa taifa na alama za utaifa, lugha ya taifa, katiba iwe ndio juu ya kila kitu, ulinzi wa katiba na pia katiba ianishe nani mtanzania na aelezwe katika katiba.



Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU