Facebook Comments Box

Tuesday, November 6, 2012

HII NDIO SIRI NDANI YA SIMBA



Kipa wa Simba,Juma Kaseja.

KOCHA MKUU wa Simba, Milovan Cirkovic ameapa kuendelea kumtumia kipa Juma Kaseja mechi zote huku bosi wa makipa, James Kisaka naye akiweka wazi hali ya mambo na kilichotokea Simba ikaondoka kileleni mwa Ligi Kuu Bara.

Milovan ametamka hivi: "Sijui kitu gani tumekutana nacho maana tunarekebisha makosa kwenye mazoezi wakiingia uwanjani kwenye mechi wanarudia tena, nashindwa kuelewa."

Lakini Kocha wa Makipa, Kisaka amesema bao alilofungwa, Juma Kaseja na Hussein Javu wa Mtibwa Sugar na timu yake kulala mabao 2-0 juzi Jumapili ni makosa yake na sasa kazi aliyonayo ni kurudisha imani kwa mashabiki wake ingawa amesisitiza hajashuka kiwango na kuwataka mashabiki wakumbuke fadhila.

Milovan amesema ataendelea kumtumia kwenye kikosi chake kwa sababu anaamini ndiye kipa bora zaidi ya wote. Kisaka amesema kutokana na uzoefu wake na idadi ya mabao 10, Kaseja aliyofungwa katika mechi za Ligi Kuu Bara ni uzembe wa mabeki na makosa ya kawaida.

"Wanaposema, Kaseja ameshuka kiwango siyo kweli kwa sababu aina ya mabao aliyofungwa si makosa yake ni safu nzima ya ulinzi. Kwanza Simba ilikuwa na tatizo la beki, mabao yaliyofungwa yalikuwa yanasababishwa na beki. Pili, kumekuwa na makosa ya kutoelewana kwa safu nzima ya ulinzi," alisema Kisaka.

"Lakini hili la pili tulilofungwa na Mtibwa linaweza kuwa ni makosa yake kwa sababu alienda kucheza mpira kwa kupiga chenga na adui akatumia udhaifu mwanya huo kumnyang'anya na kufunga.

"Unajua mashabiki wamekuwa wakisubiri kuona ubaya tu wazungumze na hawakumbuki fadhila ambazo Kaseja alizifanya kwa kipindi chote cha ushindi. Kaseja alifanya juhudi binafsi tukashinda beki ilikuwa haieleweki lakini hilo hawajui na kuangalia kosa hili la leo na kumpa wakati mgumu kufanya kazi ya ziada ili kurudisha imani kwa mashabiki wake.

"Naamini, Kaseja ndiye kipa bora zaidi ya wote kikosini ndiyo maana nampa nafasi ya kudaka mechi zote, makosa yanatokea ni hali ya kawaida hata hivyo nitaendelea kumtumia kwenye mechi zangu," aliongeza Milovan.
Hata hivyo, Kaseja aliyekuwa katika wakati mgumu na huzuni, aligoma kuzungumza lolote.

Matokeo hayo ambayo yaliipa Yanga mwanya wa kuongoza ligi yalimtoa machozi Kaseja haswa baada ya mashabiki kuonyesha kutokuwa na imani naye na kumuimbia nyimbo za kumdhihaki.

Hali halisi
Kwa mujibu wa duru za ndani ya Simba, uwezekano wa Milovan kukaa benchi la ufundi kwenye mzunguko wa pili wa ligi ni mdogo kwa kuwa hajatimiza malengo ambayo uongozi ulimtaka kushinda mechi zote nne dhidi Azam, Polisi Morogoro, Mtibwa na Toto African.

Aliishinda Azam mabao 3-1, akatoa suluhu na Polisi kabla ya kufungwa mabao 2-0 na Mtibwa juzi Jumapili na Jumapili ana kibarua cha Toto jijini Dar es Salaam.

Msimu uliopita Moses Basena alitimuliwa Simba baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza akiwa na pointi 28 wakati Milovan akishinda mechi ya mwisho atamaliza na 26.

Habari zinapasha kuwa viongozi wa juu wa Simba jana Jumatatu walijadiliana hali ya mambo ingawa hawakutaka kutoa ufafanuzi wowote.

Hali ya kutoaminiana na pia kutopendana kwa baadhi ya wachezaji, chokochoko za ndani ya uongozi imedaiwa kuwa ni chanzo cha matokeo hayo ingawa wachambuzi wa mambo wanaeleza sare za Simba ni kutokana na uchakavu wa viwanja na morali ndogo ya timu.

Simba imetoka suluhu mechi mbili za Tanga dhidi ya Coastal Union na JKT Mgambo, kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya timu dhaifu na inayochukia kushinda mechi ya Polisi Morogoro na juzi juzi huko huko Morogoro ikapigwa mabao 2-0 na Mtibwa.

Habari za ndani zinadai baadhi ya wachezaji wamekuwa wakiogopana kwa imani za kishirikina na wengine hawaongei kabisa wala kupeana pasi uwanjani.

Habari zinadai pia hata kucheza mechi nyingi kwa Kaseja peke yake hakuwafurahishi baadhi ya wachezaji ambao wanadai amechoka ndiyo maana inafika wakati anafungwa magoli laini ambayo Wilbert Mweta asingefungwa.

Suala la Kaseja limeonekana gumu kwani viongozi pamoja na makocha wanamkubali mno na wala hawana mpango wa kumweka benchi licha ya kelele za wanachama.

Jingine kubwa ni kwamba baadhi ya wachezaji wanadai kocha Milovan anaingiliwa na baadhi ya viongozi ambao wanamlalamikia kwa kutotoa nafasi kwa wachezaji wengi vijana na badala yake kuendelea kung'ang'ania walewale.


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU