Facebook Comments Box

Tuesday, November 6, 2012

HATIMAYE SERIKALI YASEMA TPI WALITENGENEZA ARV FEKI

LICHA ya wamiliki wa kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI) kukana kutengeneza na kusambaza dawa bandia za kupunguza makali ya UKIMWI, serikali imethibitisha kuwa kiwanda hicho ndicho kilitengeneza dawa hizo aina ya TT-VIR 30 yenye toleo Na OC.01.85. Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, akisema kuwa serikali itawachukuliwa hatua za kisheria wote waliohusika katika suala hilo. Alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa suala hilo hatari linapatiwa ufumbuzi wa kudumu na kuzuia lisitokee tena, kabla ya kuchukua hatua hizo za kisheria uchunguzi unafanywa kupitia vyombo vya usalama. Dk. Rashid alikiri kuingia katika mzunguko kwa dawa hizo bandia lakini akawatoa hofu wagonjwa wote wanaotumia (ARV’s) kuwa dawa zinazopatikana kwenye vituo vya kutolea huduma hiyo kwa sasa ni salama na zenye viwango vinavyotakiwa. “Tunatoa wito kwamba waendelee kutumia dawa hizo kama wanavyoshauriwa na madaktari… kupitia Wizara ya Afya, serikali imehakikisha uwepo wa dawa za kutosha na kupunguza makali ya ukimwi katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya,” alisema. Dk. Rashid alifafanua kuwa Wizara ya Afya hununua dawa hizo kupitia Bohari ya Dawa (MSD), ambayo imepewa jukumu la kununua, kuzitunza na kusambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya. Alisema kwa hapa nchini kuna kiwanda kimoja tu cha TPI kinachotengeneza dawa hizo na kwamba zile za bandia zilibainika mwanzoni mwa Agosti mwaka huu katika ukaguzi wa kawaida wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) katika Hospitali ya Tarime. Alisema baada ya ukaguzi na uchunguzi kwenye vituo vyote vya huduma za afya katika mkoa wa Mara na nchi nzima ilibainika kuwa dawa yenye jina la biashara TT-VIR 30 toleo namba 0C.01.85 ni bandia. Alisema pia ilibainika kuwa nyaraka zilizokutwa katika Bohari ya Dawa (MSD) zinaonyesha kuwa TPI iliiuzia MSD dawa hiyo bandia toleo namba 0C.01.85. Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa uchunguzi ulibaini kuwa dawa hiyo bandia ilikuwa na dawa zenye rangi tatu tofauti, njano, nyeupe na vidonge vya rangi mbili tofauti za pinki na nyeupe. Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo wa Afya, dawa zilizokuwa na rangi ya njano, zilikuwa na kiambata cha Efaverenz badala ya viambata aina ya Nevirapine, Lamivudine na Stavudine vinavyopaswa kuwemo. Aidha vidonge vyenye rangi nyeupe na vile vyenye rangi ya pinki na nyeupe vilikuwa na viambata vinavyotakiwa kuwepo yaani Nevirapine, Lamivudine na Stavudine kama ilivyokuwa kwenye lebo. Akielezea kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali baada ya matokeo hayo ya uchunguzi alisema ni pamoja na kusimamisha mara moja matumizi ya dawa hizo aina ya TT-VIR 30 toleo Na 0C.01.85. Hatua nyingine ni pamoja na kusitisha uzalishaji wa dawa zote katika kiwanda cha TPI Ltd hadi uchunguzi wa suala hilo utakapokamilika ikiwa ni pamoja na kujiridhisha tena ubora wa dawa inazozalisha. Alisema pia vigogo wa MSD akiwamo mkurugenzi wake walisimamishwa na kwamba wizara imeunda timu ya wataalamu kwa lengo la kufuatilia mwendelezo wa tiba na matunzo kwa wagonjwa wa UKIMWI.

Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU