Evance Aveva
RAIS wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Evans Aveva, alikaa rumande kwa siku mbili baada ya kushikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kutokana
na amri ya kukamatwa iliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru).
Taarifa za kukamatwa kwa Aveva zilianza kuenea juzi usiku huku kukiwa
na sintofahamu kubwa juu ya chanzo cha bosi huyo wa klabu kigogo cha
soka nchini kulala rumande. Hata hivyo, jana vyombo vya dola vilianza kufunguka na kueleza
masuala mbalimbali yaliyosababisha kushikiliwa kwa Aveva ingawa muda wa
asubuhi maofisa wa polisi na Takukuru walishindwa kuweka bayana sababu
hasa ya kumshika bosi huyo.
Baadaye Takukuru walisema kwamba uchunguzi unaendelea lakini Aveva
anashikiliwa kwa madai ya matumizi mabaya ya ofisi ingawa Ofisa Habari
wa Takukuru, Musa Milaba, hakutaka kuweka wazi zaidi.
baadae taarifa za udadisi zikabainisha kuwa kukamatwa kwa Rais huyo ni tuhuma za matumizi mabaya
ya fedha zilizotokana na mauzo ya mshambuliaji wao Mganda, Emmanuel
Okwi, aliyeuzwa katika klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka 2009.
Simba walipokea zaidi ya Sh milioni 600 kutoka kwa klabu ya Etoile baada ya kuuzwa kwa dola 300 za Kimarekani. Inadaiwa kwamba, fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti ya klabu ya
Simba na baadaye kuhamishwa na kupelekwa katika akaunti ya mtu binafsi
ambaye ni mwanachama wa klabu hiyo.
Chanzo: Bingwa
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog