Facebook Comments Box

Friday, January 3, 2014

BENKI KUU YA TANZANIA YATOA SARAFU YENYE THAMANI YA SHILINGI 50,000 YA PAMOJA

PROFESA BENNO NDULU - GAVANA WA BENKI KUU YA TANZANIA

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa sarafu maalumu ya kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye thamani ya sh 50,000.

Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, alisema kuwa sarafu hiyo iliyotengenezwa kwa madini ya fedha kwa asilimia 92.50, imetolewa kwa ajili ya kumbukumbu tu na haitaingizwa katika mzunguko wala kutumika kwa kulipia malipo ya aina yoyote.




Sarafu hii imetolewa maalumu kama maadhimisho ya miaka 50 ya mapinduzi ya Zanzibar, haitatumika kwa manunuzi.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki ya BoT ilimnukuu Profesa Ndulu akisema sarafu hiyo imetolewa kwa idadi ya vipande 3,000 kwa ajili ya tukio hilo na kuwahimiza wananchi kuinunua kwa ajili ya kumbukumbu hiyo.


Kwa mujibu wa Gavana, kutolewa kwa sarafu hiyo kunakwenda sambamba na utaratibu wa Benki Kuu kutoa sarafu maalumu za aina hiyo kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya matukio mbalimbali muhimu ya kitaifa na kimataifa.


Kwa kawaida, baada ya muda, thamani ya sarafu kama hizi huongezeka na kuwa na faida zaidi kwa wanaozimiliki,” alisema Profesa Ndulu.

Gavana Ndulu alieleza sarafu hizo zitapatikana Januari 5 kwa bei ya sh 50,000 katika matawi ya benki za biashara zitakazokuwa zimepata sarafu hizo kutoka Makao Makuu ya Benki Kuu, Dar es Salaam na matawi ya Benki Kuu yaliyoko Zanzibar, Arusha, Mbeya na Mwanza.

Benki za biashara zinaweza pia zikasambaza sarafu hizi kupitia matawi yake,” alisema gavana na kuongeza taarifa za usambazaji zitatolewa na benki hizo.

Katika sarafu hiyo, upande wa mbele unaonesha sura ya hayati Sheikh Abeid Aman Karume na maandishi yanayosomeka: ‘Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi’. 

Upande mwingine wa sarafu unaonesha nembo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, maandishi yanayosomeka: “Miaka Hamsini ya Mapinduzi”, thamani ya sarafu na miaka 1964-2014.


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU